Badru arejea London kivingine, akichimba mkwara mzito

Muktasari:
- Badru ambaye aliwahi kuzinoa timu kama Gwambina FC, Mtibwa Sugar na pia aliyekuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu za vijana za Azam FC, ameandika ukurasa mpya wa maisha yake ya ukocha kwa kutua London, Uingereza.
MAKOCHA wengi wa Kitanzania wamekuwa na ndoto ya kufanya kazi nje ya nchi hasa barani Ulaya lakini ni wachache ambao wamefanikisha hilo na mmoja kati yao ni Mohammed Badru.
Badru ambaye aliwahi kuzinoa timu kama Gwambina FC, Mtibwa Sugar na pia aliyekuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu za vijana za Azam FC, ameandika ukurasa mpya wa maisha yake ya ukocha kwa kutua London, Uingereza.
Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti, Badru anafichua kuwa yupo kwenye mchakato wa kuingiza falsafa yake ya ukufunzi kwenye soka la vijana nchini humo, baada ya kupata nafasi katika klabu ya May & Baker FC 693 timu kongwe inayoshiriki ligi (Level 4) nchini Uingereza, maarufu kama Essex Senior League, sambamba na Kombe la FA.
“Kwa sasa nimerudi Uingereza baada ya kupata kazi ya kufundisha timu ya pili, U23, U18 na U16. Lengo langu ni kuhakikisha ninaweka falsafa yangu ya ufundishaji kwa vijana na kuhakikisha wanaelewa mfumo sahihi wa uchezaji,” anasema Badru.
Badru anasema kuwa nafasi hiyo ameipata baada ya kufanya majaribio ya kiufundi ambayo alifaulu, na sasa anapata jukwaa la kujipima zaidi katika mazingira mapya yenye ushindani mkubwa na changamoto halisi za ukocha barani Ulaya.
“Baada ya kumaliza kozi ya CAF B, pia nimepata nafasi ya kusoma UEFA B, mwaka huu nilihisi nahitaji changamoto mpya. Nilihitaji kujiweka sehemu yenye ushindani ili niweze kujipima uwezo wangu. Ndio maana nikarudi Uingereza kwa sasa hapa ndipo ninapopata nafasi ya kujifunza zaidi na kukua kitaaluma,” anaongeza Badru.
Klabu yake mpya, May & Baker FC 693, ina historia ndefu na ya mafanikio katika mji wa London. Imetoa wachezaji wengi waliopitia mfumo wake wa soka la vijana na kuuza vipaji hivyo kwenye timu mbalimbali kubwa nchini humo.
Kwa mujibu wa Badru, hiyo ni fursa adhimu kwake sio tu kuendeleza vijana bali pia na kuwapa nafasi vijana wetu wa Kitanzania na kuonyesha kuwa makocha kutoka Afrika Mashariki, hususan Tanzania, wana uwezo wa kufanya makubwa hata katika mazingira yenye ushindani mkubwa.
“Hii timu ni ya muda mrefu, na ina mfumo imara sana wa kukuza na kuuza vipaji. Naamini kupitia nafasi hii, nitajifunza mengi, lakini pia nitawasaidia vijana kufika mbali zaidi,” anasema.
Uamuzi wa Badru kuhamia London haukuwa wa ghafla. Kwa muda mrefu amekuwa akitafuta mazingira yatakayompa changamoto mpya na fursa za kitaaluma. Aliamini kuwa kufundisha soka la vijana katika mazingira yaliyoendelea zaidi ni hatua muhimu kuelekea kuwa kocha kamili wa kimataifa.
Kwa kocha huyu aliyejikita zaidi katika ufundishaji wa falsafa ya ‘total football’, anakiri kuwa mazingira ya Uingereza yanamuwezesha zaidi kutumia mbinu zake za kisasa kama ilivyokuwa Azam.
“Ninapata fursa ya kufundisha vijana ambao tayari wanaelewa misingi mingi ya soka. Nikiwa kocha, hii inanipa nafasi nzuri sana ya kushirikiana nao, kuwajenga kiakili na kiufundi,” anaeleza.
Badru ana matumaini kuwa mafanikio yake Uingereza yatafungua milango kwa makocha wengine wa Kitanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Anaamini kuwa kama atafanya kazi nzuri na kuweka alama, basi mfumo wa soka la Uingereza unaweza kuanza kufungua macho kwa vipaji vya ukocha kutoka bara la Afrika.
Kwa sasa, Badru anajikita kikamilifu katika kazi yake mpya, akiwa na ndoto ya kufikia ngazi ya juu zaidi na huenda siku moja tukamwona akisimama kwenye benchi la moja ya timu kubwa za madaraja ya juu zaidi kama League Two, One na hata Championship.
“Safari bado ni ndefu, lakini nimeanza. Kitu muhimu ni kuwa nimeamua kujitoa kikamilifu. Najua haitakuwa rahisi, lakini kila siku najifunza jambo jipya,” anahitimisha.
MAFANIKIO YAKE
Moja ya mafanikio yake ni kuteuliwa kuwa Kocha Bora wa Mwezi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ndani ya mwezi Machi 2021 alipokuwa akiinoa Gwambina FC.
Ndani ya msimu huo alijiunga na Mtibwa Sugar na kusimama kuiokoa timu hiyo dhidi ya janga la kushuka daraja.
Mafanikio mengine ya kipekee ya Badru ni katika ngazi ya maendeleo ya vijana. Alipokuwa Azam FC, alisimamia uundwaji wa mfumo wa vijana kuanzia U12 hadi U15 vikundi ambavyo vilikosekana kabla ya yeye kuingia klabuni.
Alifanya kazi hiyo kwa bidii, akianzisha mfumo wenye misingi ya falsafa ya kiufundi aliyoiweka kwa vitendo, na kuvifanya vikundi hivyo kuwa msingi imara wa kizazi kipya cha Azam.
Matokeo ya kazi yake hiyo yalionekana pale ambapo alifanikiwa kumuibua mchezaji kijana kutoka kikosi cha U17 hadi kuuzwa kwenye Ligi Kuu ya Marekani katika timu ya Vancouver. Mchezaji huyo, anayejulikana kama Cyprian Thobias Kachwele ni ushahidi wa uwezo wa Badru kuona kipaji, kukilea na kukiweka sokoni kwa mafanikio makubwa.
Si hilo tu, Badru pia alihusika moja kwa moja katika kupeleka vijana wa makundi mbalimbali kwenye timu za taifa za vijana, jambo ambalo ni adimu kwa makocha wa vijana wengi nchini. Alisimamia mafunzo na maandalizi ya makundi tofauti na kuhakikisha wanakuwa tayari kimwili, kiakili na kiufundi kwa soka la kimataifa.
Zaidi ya hapo, Badru alishiriki mchakato uliowezesha klabu kubwa ya Sweden, AIK (Allmanna Idrottsklubben) inayoshiriki Ligi Kuu ya Sweden kufunga mkataba wa kibiashara na Azam FC kwa lengo la kukuza na kuuza vipaji vya vijana.
Katika kipindi cha miaka mitatu akiwa Azam, Badru aliongoza timu yao ya U17 kwenye mashindano mbalimbali bila kupoteza mchezo hata mmoja. Hii ni rekodi ya kuvutia inayoonyesha uthabiti wa mbinu zake, uwezo wa kimkakati na kazi kubwa aliyoweka katika kukuza vipaji.
Na katika uendelezaji wa vipaji ndani ya klabu, Badru pia alipandisha wachezaji kadhaa kutoka kikosi cha U17 hadi U20, na wengine walipewa nafasi kwenye kikosi cha wakubwa cha Azam.