MASHIMO: Straika KenGold anayetembelea nyota ya CR7

Muktasari:
- Nyota huyo aliyeipandisha KenGold Ligi Kuu Bara msimu uliopita kisha kushuka nayo msimu huu, amepiga stori na Mwanaspoti na kuelezea safari yake ya soka na malengo aliyojiwekea pia, huku akivutiwa sana na uchezaji wa Cristiano Ronaldo ‘CR7’.
LICHA ya KenGold kushuka daraja msimu huu kutoka Ligi Kuu Bara hadi Ligi ya Championship, ila miongoni mwa nyota wa timu hiyo waliofanya vizuri, hutoacha kumtaja mshambuliaji wa kikosi hicho, Mishamo Michael Daudi kutokana na uwezo alionao.
Nyota huyo aliyeipandisha KenGold Ligi Kuu Bara msimu uliopita kisha kushuka nayo msimu huu, amepiga stori na Mwanaspoti na kuelezea safari yake ya soka na malengo aliyojiwekea pia, huku akivutiwa sana na uchezaji wa Cristiano Ronaldo ‘CR7’.
SHABIKI WA CR7
Mishamo ambaye msimu huu amechangia mabao saba ya Ligi Kuu Bara na kikosi hicho baada ya kufunga matano na kuasisti pia mawili, anasema mshambuliaji anayemvutia sana ni nyota wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, Cristiano Ronaldo.
“Napenda aina ya uchezaji wake kwa sababu ni mchezaji anayejituma sana uwanjani, kwangu ni mtu ninayemkubali kutokana na jinsi anavyopambana, kiukweli ni kivutio kwa wachezaji wengi wenye ndoto za kufika mbali kwenye soka,” anasema Mishamo.
KOCHA ASIYEMSAHAU
Nyota huyo anasema licha ya kufundishwa na makocha wengi katika karia yake ya soka, ila moja ya kocha ambaye hatokaa pia akamsahau ni Benedicto Milana, kutokana na kumfundisha misingi ya uchezaji, jambo lililochangia kufika hapa alipo leo.
“Milana alianzisha timu ya vijana mtaani kwetu na kuanzia hapo akakusanya watoto wengi na kuanza kuwafundisha nikiwemo pia namimi, kiukweli nilipata misingi mizuri ya soka, jambo ambalo ataendelea kubaki katika kumbukumbu za maisha yangu.”

ANGEKUWA MWALIMU
Anasema kama asingekuwa mchezaji basi angekuwa ni mwalimu darasani, kwa sababu Babu yake aliyechukua jina hilo alifanya kazi hiyo, ingawa anashukuru kwa fursa nyingine aliyoipata na anaendelea kuifanyia kazi ili kufika mbali zaidi ya alipo.
“Malengo yangu mwanzoni yalikuwa niwe mwalimu wa kufundisha wanafunzi darasani kwa sababu ya ushawishi na kazi pia ya babu kabla sijajikuta nikiangukia katika soka, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii nyingine aliyonipatia,” anasema.
CHANGAMOTO
Katika maisha ya binadamu yoyote, changamoto ni sehemu ya kawaida na ndivyo ilivyomtokea pia Mishamo anayeweka wazi moja ya jambo asilolisahau ni kitendo cha kutembea umbali mrefu kwenda mazoezini, kwani kipindi hicho hakuwa hata na nauli.
“Nilikuwa natoka umbali mrefu sana kwa kutembea ili kwenda mazoezini kwa sababu sikuwa na hela ya kupanda gari, kiukweli ilikuwa inaniuma lakini nashukuru ilikuwa pia njia ya kunikuza kiakili, ili nipambanie malengo niliyojiwekea maishani.”
AUTAMANI UFUNGAJI BORA
Mishamo anasema moja ya malengo yake makubwa katika karia yake ya soka ni kuibuka siku moja mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, licha ya kutambua haitokuwa rahisi kutokana na ushindani mkubwa uliopo, ingawa ni deni analoendelea kuishi nalo.
“Malengo yangu ni kuibuka mfungaji bora siku moja na nitaendelea kuishi na ndoto hiyo nikiamini nitaitimiza hata nikiwa na timu nyingine tofauti na hii niliyopo, hii itanipa pia motisha ya kupambana ili nifike mbali zaidi,” anasema Mishamo.

KIASI KIDOGO CHA USAJILI
Nyota huyo anasema moja ya kiasi kidogo cha fedha ambacho alisajiliwa na hatokaa akakisahau ni cha Sh50,000, wakati huo akiichezea Toto African FC ya jijini Mwanza, ingawa ilikuwa ni chachu ya kupambana ili kutimiza malengo aliyojiwekea.
“Kila mtu ana historia aliyoipitia au kuiweka, kwangu kiasi hicho hakikunivunja moyo kwa sababu naamini huwezi kufikia malengo bila ya kuhangaika, najivunia kwani niliamini kipaji changu kitanifikisha hapa nilipokuwa leo,” anasema Mishamo.
MECHI ASIYOISAHAU
Mishamo anasema moja ya mechi ambayo hatoisahau ni ile dhidi ya Dodoma Jiji ya msimu huu, iliyopigwa Oktoba 29, 2024 na kuisha kwa sare ya mabao 2-2, kwani alifunga mabao yote mawili ya KenGold, ukiwa ni msimu wake wa kwanza Ligi Kuu Bara.
“Hiyo ni mechi yangu ambayo sitokaa nikaisahau kwa sababu nilifunga mabao yote mawili lakini hilo la pili lilikuwa ni la kusawazisha dakika ya 90, kisha baada ya hapo nikachaguliwa mchezaji bora, kiukweli itabakia kwenye kumbukumbu zangu.”

BEKI YANGA AMPA MOTISHA
Nyota huyo anasema miongoni mwa mabeki waliomsumbua sana msimu huu ni beki wa kushoto wa Yanga, Chadrack Boka kutokana na kumjulia vizuri namna ya uchezaji wake, jambo lililompa shida kuipenya ngome ya kikosi hicho kwenye mechi zote mbili.
“Mechi hizo zote mbili za msimu huu dhidi ya Yanga nilitokea pembeni kwa maana nilichezeshwa winga namba saba, nilipata wakati mgumu sana kumpita Boka, japo ilinipa motisha ya kupambana na wachezaji wakubwa na wenye uzoefu zaidi,” anasema.
CHAMPIONSHIP KIBOKO
Anasema unapocheza Ligi ya Championship ni lazima uwe umejipanga vizuri kutokana na ushindani mkubwa uliopo huko, kwani unapaswa kuhakikisha unashinda mechi zako za nyumbani ili unapoenda ugenini utafute namna ya kupata angalau hata sare.
“Ligi Kuu Bara unatumia akili sana ila Championship ni tofauti kwa sababu ni lazima ujipange ndani na nje ili ufikie pia malengo yako, nimejifunza vitu vikubwa sana kutokana na kucheza madaraja yote mawili na kiukweli yamenikuza kiakili.”

PACHA NA EDGAR WILLIAM
Msimu wa 2023-2024, Mishamo aliisaidia KenGold kupanda Ligi Kuu Bara baada ya kumaliza na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji iliyomaliza ya pili na pointi 67, huku akitengeneza pacha kali ya ushambuliaji na nyota wenzake, Edgar William.
Edgar alimaliza kinara wa ufungaji bora akiwa na KenGold baada ya kufunga mabao 21, kiwango kilichomfanya kusajiliwa na Fountain Gate msimu huu, huku kwa Mishamo akimaliza msimu huo na mabao 10, akiendelea pia kusalia katika kikosi hicho.
“Ni kweli ni mchezaji tuliyezoeana nae na kitendo cha kuondoka kilinipa morali nikiamini naweza kuondoka kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine japo haikuwezekana, Edgar anabakia kama rafiki yangu wa kweli tuliyetimiza malengo pamoja.”
MALENGO YAKE
Baada ya KenGold kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship, nyota huyo anasema kwa sasa hajafanya uamuzi wa sehemu atakayochezea msimu ujao, ingawa anajivunia kukitumikia kikosi hicho licha ya kutotimiza malengo ya kukibakisha.
“Umekuwa msimu mgumu sana kwetu kwa sababu malengo yalikuwa kuendelea kubakia Ligi Kuu Bara ila imeshindikana, kwangu ni somo kubwa nililojifunza, japo baada ya msimu kuisha ndipo nitaamua kama nitabakia au nitatafuta changamoto kwingine.”