BANKA: Kagoma anajua na Simba inabeba!

Muktasari:
- Hapa namzungumzia, kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Mohamed Banka aliyefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti na kufunguka mambo mengi, ikiwamo kuweka bayana namna anavyokunwa na kiwango cha kiungo wa sasa wa Simba, Yusuf Kagoma.
ENZI zake za uchezaji alisifika kwa mchezo wa akili, mbinu na maarifa na kudumu kwa muda mrefu kama mmoja wa viungo bora wa kati katika soka la Tanzania.
Hapa namzungumzia, kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Mohamed Banka aliyefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti na kufunguka mambo mengi, ikiwamo kuweka bayana namna anavyokunwa na kiwango cha kiungo wa sasa wa Simba, Yusuf Kagoma.
Pia amefichua anavyoiona Simba iliyopo nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kama ina nafasi kubwa ya kuandika historia iwapo itavuka hatua hiyo na kwenda fainali, mbali na kueleza namna wachezaji wa sasa walivyo katika nafasi nzuri ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Banka anasema wachezaji wa sasa wana nafasi kubwa ya kupata dili za kucheza nje kama ilivyo kwa Mbwana Samatta (PAOK) na Simon Msuva (Al-Talaba SC) walioonyesha mfano wa kuigwa. Endela naye...!

SOKA LA NJE
Banka anasema kuna haja wachezaji kutumia fursa wanazozipata ili kuandaa maisha yao ya baadaye watakaporejea mtaani.
“Mpira una muda mfupi, wajifunze kwa watu waliowatangulia wapo ambao walijipanga na wanaishi vizuri na wale ambao maisha yao ni magumu,” anasema.
Jambo jingine analosisitiza wachezaji ni kuachana na uvivu badala yake wajue hakuna njia mbadala ya kufanya wawe bora zaidi ya mazoezi na kujifunza: “Hakuna cha uchawi wala nini ukiona mchezaji anafanya vizuri ni mtu wa mazoezi.”
ISHU YA DABI
Akiwa Yanga alikocheza msimu wa 2005 hadi 2007, anasema mastaa wa Simba waliokuwa tishio katika mechi za dabi ni Emmanuel Okwi, Mussa Mgosi, Seleman Matola, Ulimboka Mwakingwe, Haruna Moshi ‘Boban’, Nico Nyagawa, Shekhan Rashid na Juma Kaseja.
“Nilipohamia Simba msimu 2008-2011 sikuwa na hofu kabisa na mechi za dabi kwani tayari nilikuwa na uzoefu ingawa kulikuwa na wachezaji hatari kama Idd Chuji, Boniface Ambani na wengine wengi ambao ukikutana nao uwanjani wanakuwa wasumbua,” anasema Banka.
Kuhusiana na maandalizi ya dabi anakiri Yanga kwa upande wa viongozi wanakuwa presha zaidi kuliko Simba isipokuwa kiufundi kwa maana ya wachezaji na benchi la ufundi hakuna utofauti, kila upande unakuwa makini kuhakikisha mashabiki wanatoka na kicheko.

“Kipindi nacheza Yanga ilikuwa chini ya aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo marehemu Yusuf Manji, hivyo wakati wa maandalizi ya dabi haikuwa ishu wachezaji kukaa hoteli zaidi ya mbili, tofauti na Simba ikichagua hoteli moja inakuwa hiyo hiyo hadi siku ya mechi,” anasema.
Baada ya kuulizwa katika klabu hizo kongwe ni ipi ambayo alivuna pesa ndefu anaitaja Simba ndiyo ilimpa maslahi yaliyochangia kuimarisha uchumi wake.
“Zamani tulikuwa tunapewa pesa za viingilio vya getini, kuna wakati mashabiki wanaovutiwa na kazi zako haikuwa shida kwao kukupa dolari, au Sh1 milioni wakati mwingine chini ya hapo, sasa ilikuwa ni akili ya mchezaji kufikiria kesho yake,” anasema Banka na kuongeza;
“Kuna tajiri mmoja kila baada ya mechi alikuwa anamwambia Juma Kaseja atupeleke kwake, tulikuwa wachezaji kama wanne hivi kwa furaha anatupa dolari za kutosha ambazo zilikuwa zinatusaidia kujikimu, wakati mwingine unasahau kuutumia mshahara kabisa.”
KILICHOMUONDOA YANGA
“Kwanza mkataba wangu ulikuwa umemalizika sasa viongozi wakawa wananichukulia poa na kuona kiwango changu cha kawaida, wakati huo Simba ikaniita na kufanya mazungumzo, nikakubali na kusaini mkataba, nikawa nacheza kwa kiwango cha juu, Manji akawauliza kipi kilitokea hadi Banka akaondoka,” anasema na kuongeza;
“Kuna viongozi wa Yanga walinipigia simu na kuniuliza kwa nini nimeondoka nikawajibu ‘sikuongezewa mkataba’.”

KIPORO CHA DABI YA MACHI 8
Anatoa mtazamo wake wa mechi iliyoahirishwa ya dabi ya Machi 8 anaona ilizingatia kanuni za Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB): ”Ninachofahamu kanuni zinasema timu iliyopo ugenini itatumia uwanjani kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi, kipi kilifanya mabaunsa waizuie timu na wakati uwanja huo ni wa serikali, hivyo ni vitu vya hovyo vinavyotakiwa vikemewe kwa afya ya mpira wa miguu.
Anaongeza: “Kuna wakati mwingine wachezaji wanaweza wasifanye mazoezi badala yake wakaingia uwanjani kukagua ili kujiridhisha kabla ya kuingia kucheza na jambo hilo linafanyika duniani kote.”
SIMBA, YANGA CAF
Anasema akiuweka ushabiki pembeni kuna haja Yanga kujifunza jambo kwa Simba kuhusiana na ushiriki wa michuano ya CAF bila kujali utani wao wa jadi ambao unatakiwa kutumika kwa ligi ya ndani.
“Awali, Simba ilikuwa inafungwa mabao matano na timu za Kiarabu, ikaimarika ikawa inazifunga timu za Kiarabu mfano mzuri Al Ahly ya Misri ilifungwa bao 1-0 kwa Mkapa miaka minne iliyopita na ugenini Simba ikapoteza kwa bao 1-0,” anasema Banka na kuongeza;
“Hivi karibuni Simba ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Al Masry ugenini nyumbani ikashinda mabao 2-0 imepita kwa penalti na kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, japokuwa nakumbuka Yanga ilifika fainali katika michuano hiyo hiyo ikaenda kupoteza ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya USM Alger, kuna haja ya kukaa chini wawe na mipango thabiti.”
Kuhusu klabu hizo kongwe kuchukua taji la Afrika, anaamini zikijipanga kuna uwezekano mkubwa wa ndoto hiyo kuwa halisi, huku akiitaka Simba iweke mikakati ya kutinga fainali kwa mwaka huu itakuwa imejirahisishia njia ya ubingwa.
“Kitendo cha Simba kuingia nusu fainali, inatakiwa kila hatua iwe na mikakati yake, naamini unaweza ukawa mwaka wa kuandika historia kwa nchi yetu kwa taji la Afrika kutua Tanzania,” anasema.

MO BANKA NI NDUGU
Jina la kiungo wa zamani wa Yanga lililokuwa linatumika kama a.k.a Banka (Mohammed Issa) ni halisi kama anavyosimulia mkongwe huyo kwamba ni ndugu yake.
“Halikuwa jina la utani, yule mimi ananiita mjomba kwa hiyo ni jina la ukoo, walipomsikia wakati amejiunga Yanga akitokea Ruvu Shooting wengi walijua kalichukua kutoka kwangu kama jina maarufu, ila kwa wengine wanaojiita hao ndio wanalitumia kutokana na kukubali kile nilichokionyesha nikiwa nacheza,” anasema Banka na kuongeza;
“Kwa sasa sijajua yupo wapi nina mpango wa kumtafuta, nizungumze naye maana bado ana umri wa kucheza mpira na ana kipaji kikubwa, kama yapo mambo yasiyo na sababu yanayoweza kuua kapaji chake nadhani tutayazungumza na kuyaweka sawa.”
KAGOMA MTU SANA
Anasema kwa nafasi aliyokuwa anacheza akimtazama kiungo namba sita wa Simba, Yusuph Kagoma anaona anafanya kazi kubwa ya kukaba mtu na mtu kitu ambacho ni adimu kwa miaka ya sasa kukutana na uchezaji wa aina yake.
“Jambo la msingi kwa Kagoma afanye sana mazoezi binafsi, ilikuwa hivyo kipindi chetu mimi, Juma Kaseja, Ulimboka, Boban, Mgosi kwa kifupi asilimia kubwa ya wachezaji wengi wa zamani tulikuwa hivyo, tunafanya mazoezi mara tatu kwa siku ukiachana ya asubuhi na jioni ya kocha tulitenga muda wetu wa ziada,” anasema na kuongeza;
“Ndio maana sijashangaa kabisa Kaseja kuaminiwa kupewa timu ya Kagera Sugar, tangu zamani ana sifa ya uongozi ndani yake na ndiye aliyekuwa kinara wa kutusisitiza kufanya mazoezi binafsi, katika timu ya maveterani wa Simba yeye ndiye kocha, hivyo naamini ataivusha timu salama isishuke Ligi Kuu na atakuwa sababu ya vijana wengi kuwapa misingi mizuri ya kuzifikia ndoto zao.”

Mbali na hilo anazungumzia jinsi ambavyo zamani vipaji vilikuwa vinapatikana ila kwa sasa asilimia kubwa wachezaji wanapewa maelekezo ya kufundishwa soka la kisasa zaidi.
“Mfano mimi kipaji changu kilikuwa kikubwa kutokana na bidii, nidhamu ya mazoezi na kuzingatia maelekezo ya makocha, ingekuwa nimepitia katika vituo kama ilivyo kwa wachezaji wa sasa nadhani ningekuwa bora zaidi ya kile nilichokifanya. Elie Mpanzu ndio maana ana mabadiliko makubwa, hakuna uchawi wala nini ni kujituma,” anasema.
Ujumbe wake kwa mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize anamtaka asipuuze dili zinazokuja mezani kwani mpira wa miguu ni wa kipindi kifupi kama hatafanikiwa kutengeneza pesa kipindi anachofanya vizuri, asije akajuta kwa miaka ya baadaye.
“Endapo kama kuna namna uongozi wake unaweka uzito, wamsaidie Mzize kwa ajili ya maisha yake ya baadaye, ili akija kushuka kiwango ama kustaafu maisha yake aje kulia kivulini, asilimia kubwa ya sisi wachezaji vipaji ndivyo vinavyobadilisha maisha yetu kiuchumi,” anasema.
Kuhusiana na Ligi Kuu anasema kwa sasa imepiga hatua kubwa kutoka na uwekezaji unaowasaidia kuwapa maisha mazuri wachezaji na kitendo cha kuonyeshwa ni rahisi kwao kupata dili nje.
“Mchezji ni rahisi kuonekana na timu za nje, tofauti na kipindi chetu ambacho michuano ya kimataifa ama ukicheza timu ya taifa ndio ilikuwa mojawapo ya njia ya kupata dili hizo, kuna wachezaji wengi wazuri wa ndani na nje ambao wanafanya makubwa, siwezi kutaja mmoja mmoja,” anasema akitaja dabi yake bora ilikuwa ya mwaka 2008 waliyoifunga Yanga mabao 3-0.
NI ANGA KWA ANGA
Anasema kwa sasa anafanya biashara zake, hivyo muda mwingi anasafiri kwenda Dubai na China kufuata mizigo, hivyo kuhusiana na masuala ya mpira kwake imebakia ushabiki pekee.
“Nilishauriwa na watu mbalimbali kuhusiana na kusomea ukocha, ila niliona nikistaafu uwanjani niwe nimeishia hapo badala yake niendelee na shughuli nyingine za biashara ambazo zinaniingizia kipato cha kujikimu kimaisha,” anasema Banka ambaye hakutaka kufafanua kabisa vitu alivyovifanya na pesa ya mpira wa miguu.
Banka alichukua ubingwa wa Ligi Kuu akiwa na Yanga 2005/06 na Simba msimu wa 2009/10.