Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bilishanga: Mwanamke wa kisasa ni zaidi muonekano

Muktasari:

  • Mei 2025 hakuanzisha kituo cha Muda Modeling kwa bahati mbaya.

MWANAMKE kuna jambo la kujifunza ili kupandisha thamani ama hadhi yako, kuonekana wa kisasa zaidi, kama anavyoelekeza mkufunzi wa wanamitindo nchini, Conrad Dagulas Bilishanga mwenye umri wa miaka 25.

Mei 2025 hakuanzisha kituo cha Muda Modeling kwa bahati mbaya.

Bilishanga ni msomi wa ngazi ya shahada ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia. Chuo hicho kwa jina lililosajiliwa kinajulikana kama Dk Salim Ahmed Salim Centre For Foreign Relations kilichopo Dar es Salaam, Tanzania.

Katika mahojiano na Mwanaspoti anasema elimu ya masuala ya uongozi, mawasiliano na usimamizi wa kimkakati inamsaidia katika kazi zake na lengo ni kuona wanawake wa Kitanzania wanatambua fursa zilizopo katika mitindo huku akisisitiza wawe ni watu wa kupenda kujifunza vitu chanya vitakavyoletea mabadiliko katika maisha yao.

“Katika familia yetu tumezaliwa watoto sita, mimi ni wa mwisho na mwanaume pekee. Wakati nayatambulisha maono yangu hayakupokelewa kirahisi na wazazi wangu hadi walipojilidhisha, kwa sasa wananisapoti.

“Natambua itanichukua hadi miaka 10 ya kujulikana kwa ukubwa, kwa sasa naendelea kuwasilisha mawazo yangu, lakini ipo siku legasi yangu itatajwa kwa ukubwa ndani na nje,” anasema na kuongeza:

“Tunapokea wasichana kuanzia umri wa miaka 16 na kuendelea, kwa sasa tuna idadi ya watu 47. Niliona fursa ya wanawake wengi wa Tanzania wanapenda urembo ila hawana misingi sahihi, muonekano pekee bila elimu na maono hauwezi kuwapa fursa ya kipato na kuongeza thamani zao.

“Baada ya kumaliza chuo nilipata muda wa kwenda kujifunza mambo ya umodo katika taasisi mbalimbali, ndipo nikaanzisha chuo cha mafunzo. Natambua mwanamke akielimishwa katika nyanja mbalimbali basi tutakuwa na jamii bora zaidi.”

Anasema kwa upande wake anasimamia zaidi katika uongozi na mipango, akisaidiana na mkufunzi wa miondoko Pato Adam ambaye ni maarufu zaidi mitandaoni kutokana na miondoko yake akiwa anawafundisha warembo.

“Kuhusu Pato ndiye anayedili na kuwafundisha namna ya kutembea, ujue mwanamke lazima atambue kuna aina tofauti ya mwendo kulingana na sehemu anayokwenda,” anasema na kuongeza:

“Mfano anapokuwa ofisini kuna mwendo na mavazi yake, inapotokea kaalikwa katika makongamano mbalimbali ya kijamii kuna staili yake, anapokuwa katika majukwaa ya urembo pia lazima azingatie vitu muhimu, mfano kujiamini, uelewa, mvuto wa mavazi bila kusahau utulivu na heshima.”

Anasema jukwaa la urembo ni pana, ukiachana na mashindano ya urembo, wengine wanaweza wakawa wabunifu wa mavazi ama kuwatangazia wengine mavazi na wakapata ajira ya kujitegemea kiuchumi, jambo analosisitiza litasaidia kuwa na jamii bora.

“Kuna msemo unasema kama mama atakuwa na furaha basi ulimwengu una furaha, mwanamke ana majukumu ya kuiandaa jamii yenye uelewa, ndiyo maana tunajitahidi kuwapa maono makubwa ya kutojichukulia kawaida na watu wasio na thamani mbele ya jamii inayowazunguka,” anasema.

Anasema japokuwa soko la umodo Tanzania ni changa akitofautisha na nchi zilizoendelea Afrika kama Nigeria na Ghana, imani yake miaka ijayo ni mapinduzi ya bendera ya nchi kutajwa katika ubora wa tasnia hiyo.

“Vipaji vingi Tanzania vinatokana na fasheni, shoo, matangazo ya bidhaa na matukio ya mitindo, lakini miundombinu ya kitaalamu kama vituo na menejimenti ndiyo vinaanza kujengwa taratibu,” anasema na kuongeza:

“Pamoja na hayo yote, Tanzania ina vipaji vikubwa ambavyo vimefanikiwa kimataifa kama Miriam Ondemba, Flaviana Matata na Herieth Paul, jambo linaloonyesha kuwa uwezo wetu ni mkubwa ila tunahitaji mafunzo ya kitaalamu, uwekezaji na majukwaa ya kuonyesha vipaji vya vijana wenzetu wa Kitanzania ili soko liweze kufikia ushindani wa kimataifa zaidi.”


VITU VYA KUZINGATIA

Anasema wanazingatia nidhamu, hofu ya Mungu, kujiamini, uwezo wa kujifunza na mtazamo chanya kuhusiana na tasnia hiyo.

“Ndiyo maana umodo siyo muonekano pekee, badala yake ni mchanganyiko wa kipaji, tabia ambayo itawafanya wazazi wengi ama jamii kubadili mawazo kuona umodo ni burudani ama wanawake wa aina fulani hivi,” anasema.

Anasisitiza kwamba mwanamke anapaswa kujithamini ndipo wengine wauone upekee wake.

“Ukiachana na wale ambao wanapenda umodo, hata wale ambao wana familia wana nafasi za kipekee za kujipenda na kuona wana thamani kubwa na wana weza wakatimiza ndoto zao za kile wanachokiona wana weza wakakifanya,” anasema.

Ana sema mwanamke anapaswa kujitafsiri na kurekebisha namna ya kutembea kulingana na mazingira aliyopo na siyo kila sehemu atembee kama anakwenda sokoni.

“Lazima kuwa na mwendo wa heshima na utulivu unaoonyesha weledi na umakini mkubwa, kujiamini pia wajue namna ya kuzungumza kwa mpangilio wa maneno na nyakati gani waseme nini na zipi wanyamaze,” anasema.

“Angalia wanawake maarufu duniani wanapopanda majukwaani huwezi kuona anatembea bila mpangilio ama kama anakimbizwa, lazima utaona umakini na utulivu wa hatua zake, ndivyo ilivyo katika majukwaa ya umodo, maana hadi anapanda kwenye maonyesho anakuwa anavaa analolitangaza, ili watu waweze kulizingatia ni mwendo na kujiamini kwake pamoja na nidhamu.”

Anawataja baadhi ambao kwa sasa wanafanya vizuri na wanao wafuasi wengi katika mtandao wa Instagram.

“Faidha Sanja, Lightness Joel Mgisha, Violet Ambros, Glory Sambo, Victoria Saulo, Dalce Kirigini wote wapo katika hatua ya ukuaji lakini tayari wam eanza kupata mwanga wa kuingiza kipato, hicho ndicho tunachokitaka,” anasema.


CHANGAMOTO

Anasema hakuna kazi inayokosa changamoto, kubwa anayokutana nayo ni uelewa mdogo katika jamii na kuchukulia kama burudani na siyo fursa ya kuingiza kipato.

“Mwanzoni kila jambo jipya linakuwa na mtazamo tofauti, muendelezo wa kile unachokifanya na matunda chanya ndivyo vitakavyowabadili. Mfano mzuri zamani wanawake walikuwa wakicheza mpira wa miguu walichukuliwa wahuni, kwa sasa inaonekana ni ajira. Ukiachana na hao wapo marubani, wanaoendesha magari makubwa, treni, kila nyanja tunatamani mwanamke awe na nguvu ya kujitegemea,” anasema na kuongeza:

“Mbali na kuwapa fursa wengine, kwangu binafsi imebadilisha maisha yangu, imenijengea nidhamu, uwajibikaji na mtazamo mpana, imenifanya niwe mtu mwenye maono makubwa, anayejali maendeleo ya vijana na kuwekeza kwenye vipaji vya wengine, imenipa fursa ya kukutana na watu tofauti, kujifunza zaidi na kukuza uelewa wangu kwenye tasnia hii ya mitindo, naamini nitaacha legasi ya kukumbukwa daima.”

Anasema: “Nimepata nafasi ya kuathiri maisha ya vijana wenzangu wengine kwa kuwaandaa kuwa wataalamu na sura bora za baadaye, jambo ambalo limeniongezea dhamira na heshima katika ndoto yangu, kikubwa nahitaji kujitoa zaidi kwa wengine.”

Anasema kwa sasa shughuli zao wanazifanyia Dar es Salaam, lakini ndoto ni kupanua wigo mpana zaidi.

“Lengo letu ni kuendelea kukua hatua kwa hatua na kuongeza ajira kadri shughuli zinavyopanuka na mahitaji kuongezeka.”

Anasema watu waliokuwa wanamvutia katika nyanja hiyo ni Larry Walker, mtendaji mkuu kutoka Law Models Academy ya Nigeria.

“Ndiyo maana Nigeria ina wabunifu wakubwa wa mitindo na mamodo wanaofanya vizuri, kwa sababu wengi wao wamepitia katika mafunzo,” anasema.

Mbali na kazi hiyo anajitambulisha ni shabiki wa Yanga na mchezaji anayemkubali ni Maxi Nzengeli.

“Japokuwa siyo mfuatiliaji kihivyo wa mpira wa miguu kutokana na ratiba zangu kunibana kwa kusimamia kazi na kuendelea kuongeza ujuzi kichwani, namkubali Maxi, nafanana naye kwa mbali pia ni mcha Mungu kama mimi.”