Chamou Karaboue alivyopunguza presha Simba

Muktasari:
- Huu ni msimu wake wa kwanza kuichezea Simba akisajiliwa kutokea Racing Club d’ Abidjan ya Ivory Coast kwa mkataba wa miaka miwili.
HAIKUWA kazi nyepesi kwa beki wa Simba, Chamou Karaboue kupata nafasi kwenye kikosi hicho mbele ya mabeki, Che Malone Fondoh na Abdulrazack Hamza ambao ndio walinzi tegemeo wa kati.
Huu ni msimu wake wa kwanza kuichezea Simba akisajiliwa kutokea Racing Club d’ Abidjan ya Ivory Coast kwa mkataba wa miaka miwili.
Tangu ametua kikosini hapo amekuwa akiishia kukaa benchini kutokana na mabeki wenzie Malone na Hamza kumzidi kete kwa kiwango na ubora wanaounyesha kikosini hapo.
Awali, wengi walitarajia angeingia katika kikosi hicho moja kwa moja kutokana na usajili wake kuvuma akisifika kwa umahiri wa kucheza mipira ya juu na uwezo wa kushambulia aliounyesha akiwa Ivory Coast.

Hata hivyo, mambo yakabadilika mapema tu kabla hata msimu haujaanza kutokana na kutowavutia wengi kwa kile alichokionyesha katika mechi ya kirafiki ya tamasha la Simba Day 2025, ambayo Wekundu wa Msimbazi waliifunga APR ya Rwanda 2-0.
Badala yake, Hamza akaingia kwenye kikosi hicho kutokana na utulivu, uwezo wa kunyang’anya mpira na hesabu za kukabiliana na washambuliaji hasa ana kwa ana (1v1).

Tangu hapo Chamou aliendelea kukaa benchini na kupewa mechi kadhaa kutokana na eneo hilo kutendewa haki na mabeki wenzie.
Februari 26, mwaka huu Che Malone aliumia na kocha Fadlu Davids akawa hana chaguo jingine zaidi ya kumuanzisha Chamou ambaye hakuanza vizuri lakini alipata nafasi kadhaa na Mwanaspoti limekuchambulia namna beki huyo alivyotuliza presha baada ya Simba kumkosa Che Malone ambaye ni tegemeo eneo la beki wa kati.
PRESHA YA CHE MALONE
Kama kuna kitu kilikuwa kinawaumiza vichwa Simba ni baada ya beki wao tegemeo, Che Malone kukosekana hasa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho ambapo Simba ilishinda 1-0 dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali.
Che Malone aliumia katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC uliopigwa Februari 26 na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 na kutolewa katika dakika ya 20.

Presha ilianzia kufuatia mechi na Yanga Machi 8 ikielezwa kuwa nyota huyo angeukosa mchezo huo wa dabi kutokana na majeraha aliyoyapata.
Chamou alikuwa haaminiki. Beki mwingine wa kati, Hussein Kazi haamini tangu aliposababisha Simba ikafungwa na Yanga. Kukosekana kwa Che Malone na huku pia kipa Moussa Camara alikuwa majeruhi, ikadaiwa mitaani kwamba ndio chanzo cha Simba kuikacha mechi ya dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga kwa madai ya kuzuiwa kufanya mazoezi kweye uwanja wa mechi siku moja kabla ya mchezo.
Baada ya Che Malone kuumia ni kama Simba iliingia presha ya kumkosa beki huyo raia wa Cameroon. Kuna mechi kocha Fadlu Davids alimchezesha kiungo wa ulinzi, Yusuph Kagoma katika nafasi ya beki wa kati.
Hata hivyo, Chamou alipokuja kupewa nafasi ameituliza presha Msimbazi na kuisaidia timu hiyo.

ALICHOFANYA
Tangu aumie beki huyo maarufu kama ‘Ukuta wa Yeriko’, Simba ilicheza mechi mbili za Ligi Kuu bila uwepo wake na Chamou akaonyesha kiwango bora cha kutoruhusu bao dhidi ya Coastal Union timu hiyo iliposhinda mabao 3-0 na ilipoichakaza Dodoma Jiji 6-0.
Kiujumla Chamou amecheza mechi nane za mashindano yote baada ya Che Malone kuumia akicheza dakika 680 na kuruhusu mabao manne.
Kumbukumbu nzuri kwa wana Simba ni baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye mchezo muhimu wa marudiano wa robo fainali dhidi ya Al Masry ambao Wekundu walishinda 2-0 Kwa Mkapa na kufanya matokeo ya jumla ya 2-2 baada ya kufungwa 2-0 katika mechi ya ugenini, Misri. Simba ikatinga nusu fainali kwa penalti 4-1.
Chamou alituliza presha kwenye mchezo huo Kwa Mkapa akizuia mashambulizi ya Al Masry na akakaba kwa nidhamu kubwa tena dhidi ya Stellenbosch katika nusu fainali ya kwanza Simba ikishinda 1-0 kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar.

MSIKIE FADLU
Akizungumzia juu ya pengo aliloziba Che Malone, kocha Fadlu alisema ana kikosi cha wachezaji bora ambao wana uwezo wa kuamua mechi ingawa awali majeraha ya Malone yalimshtua kutokana na umuhimu wake kwenye kikosi hicho. “Majeraha ya Che Malone yalinishtua kidogo lakini najua nina kikosi kikubwa na naamini uwezo wa Chamou, unaweza kuona kwenye mechi alizoanza ameonyesha kiwango kikubwa,” alisema Fadlu.