DAKIKA ZA JIOOONI: Namungo grafu inashuka

Muktasari:
- Takwimu zinaonyesha Namungo yenye maskani yake Ruangwa mkoani Lindi, grafu yake inashuka kila msimu tangu ilipoanza kushiriki 2019-2020.
HATA itokee miujiza kiasi gani, lakini Namungo haitaweza kuvuka pointi 40 katika mechi tatu zilizobaki. Hiyo inatokana na sasa kuwa nazo 31. Msako wa pointi hizo 40, unairudisha timu hiyo katika msimu wa 2022-2023 ilipomaliza ligi nafasi ya tano.
Takwimu zinaonyesha Namungo yenye maskani yake Ruangwa mkoani Lindi, grafu yake inashuka kila msimu tangu ilipoanza kushiriki 2019-2020.
Katika msimu huo wa kwanza unaweza kusema ndiyo ulikuwa bora zaidi kwao kwa kumaliza nafasi ya nne, kisha kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika 2020-2021.

Ushiriki wao wa kwanza michuano hiyo, ilipiga hatua kubwa sana kwa kucheza makundi lakini haikuwa na matokeo mazuri ikimaliza mkiani bila ya pointi ikipoteza mechi zote nne huku ikiondoka bila ya kufunga bao hatua ya makundi.
Namungo ile ya msimu wa kwanza ligi kuu, imekuwa ikienda ikishuka jambo ambalo linazua maswali mengi sana.

Msimu huu Namungo inapambana isiwe kwenye nafasi mbaya zaidi itakayowaweka kwenye hatari ya kushuka daraja. Baada ya Jumapili iliyopita kupata ushindi wa mabao 2-1 nyumbani, imefikisha pointi 31 katika nafasi ya nane kabla ya mechi za jana.
Ikiwa imebakiwa na mechi tatu, ili iwe salama zaidi bila ya kuangalia wapinzani wake wanafanyaje, Namungo inahitaji kushinda mechi zote jambo ambalo linabaki kuwa mtihani mzito kwa benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Mkuu, Juma Mgunda.
“Huu ni msimu dume, sio rahisi hata kidogo, ukiangalia kila timu unayokutana nayo ni bora, hakuna mechi ambayo una uhakika wa kukusanya pointi tatu bila ya maandalizi mazuri, licha ya hivyo nafurahi wachezaji wangu sasa wanafanya vizuri licha ya makosa madogo madogo yaliyopo,” anasema Mgunda huku akibainisha ugumu uliopo sasa unawafanya wajipange kwa kila hali ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kuicheza tena ligi msimu ujao.

“Hakuna mchezo rahisi, lakini kila kitu kinawezekana, mbinu na mikakati sahihi inahitajika ili kuisaidia Namungo kuendelea kubaki msimu ujao, ugumu upo na mikakati inaendelea ili kurekebisha makosa tuliyoyafanya katika mechi zilizopita,” anasema Mgunda.
Namungo ambayo sasa imeingia kwenye 10 bora katika msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kutoka kuichapa Mashujaa 2-1, mchezo ujao itakuwa ugenini Mei 13 mwaka huu dhidi ya Yanga, kisha itamalizia nyumbani dhidi ya Kagera Sugar (Mei 21) na KenGold (Mei 25).
“Kwa sasa imezaliwa ligi ndani ya ligi, hivyo mechi tatu zilizobaki tutakaa na uongozi kujua nini tufanye, lakini tutawapa mapumziko kidogo wachezaji baada ya hapo tutaendelea kuhakikisha michezo mitatu iliyobaki tunafanya vizuri na kumaliza vizuri ligi,” anasema Mgunda.

Msimu uliopita, Namungo ilimaliza ligi nafasi ya sita kwa kukusanya pointi 36. Pointi za Namungo zimekuwa zikishuka kila msimu tangu ianze kushiriki Ligi Kuu Bara 2019-2020, huku ikibadilisha nafasi kwa kupanda na kushuka.
Takwimu zinaonyesha Namungo msimu wa kwanza 2019-2020 ilimaliza nafasi ya nne kwa kukusanya pointi 64. Ndiyo msimu ambao ilikusanya pointi nyingi zaidi ambao pia ilicheza mechi 38 tofauti na sasa inacheza 30. Wastani wa kukusanya pointi kwa mechi ulikuwa 1.7.
Baada ya hapo, 2020-2021 ilishika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 43 kwa wastani wa 1.3 baada ya kucheza mechi 34. Kuanzia 2021-2022 hadi sasa 2024-2025, ligi imekuwa ikichezwa kwa mechi 30 kila timu.

Namungo katika msimu wa 2021-2022, ilimaliza nafasi ya tano na pointi 41 kwa wastani wa 1.4, kisha 2022-2023 ikakomaa nafasi ya tano kwa pointi 40 wastani 1.3. Msimu uliopita ilishuka hadi nafasi ya sita ikikusanya pointi 36 kwa wastani wa 1.2 unaofanana na msimu huu baada ya kucheza mechi 27 ikiwa na pointi 31.
Timu hiyo imekuwa haina uwiano mzuri wa mabao kwa misimu mitatu mfululizo sasa kwani inafunga machache na kuruhusu mengi jambo ambalo linaiweka kwenye hatari kubwa.
Tangu mara ya mwisho ifunge mabao 42 na kuruhusu 34 msimu wa 2021-2022 katika mechi 30, imeshindwa kurudia ubora huo wa kucheka na nyavu na sasa inacheza kwenye mabao chini ya 30, huku ikiruhusu zaidi na kujikuta ikimaliza msimu na deni.
Msimu uliopita ilifunga 27 na kuruhusu 29, hivyo ikawa na deni la mabao mawili. Kabla ya hapo, msimu wa nyuma yake ilifunga 29 na kufungwa 33. Kwa sasa imefunga 23 na kufungwa 33.
Kinachoifanya Namungo kutokuwa na makali kwenye ufungaji ni ubutu wa safu hiyo kwani kinara wake ni beki, Erasto Nyoni mwenye mabao manne. Nyoni jumla amehusika kwenye mabao sita kwani ametoa pia asisti mbili hivyo ndiye mwenye mchango mkubwa. Wanafuatia viungo Pius Buswita na Jacob Masawe kila mmoja akiwa na mabao matatu na asisti moja.

Mshambuliaji Fabrice Ngoy amefunga mawili kama ilivyo kwa kiungo Geofrey Julius.
Ukiangalia takwimu hizo za wafungaji, moja kwa moja utapata jibu namna Namungo inavyoteseka eneo la ushambuliaji.
Nyota wengine waliofunga ni Ibrahim Ali, Hassan Kabunda, Hamis Khalifa Nyenye, Salehe Karabaka, Djuma Shabani, Ritchi Nkoli, Daniel Amoah na Derick Mukombozi kila mmoja amefunga bao moja.