Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DAKIKA ZA JIOONI: KMC bado haieleweki

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Kiwango chao hicho kimeonekana kuwa hivyo ndani ya misimu saba ambayo timu hiyo imekuwa ndani ya Ligi Kuu Bara.

KUTOKA nafasi ya tano hadi hivi sasa kupiga hesabu za vidole kuepuka kushuka daraja, inadhihirisha wazi kwamba KMC imekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka.

Kiwango chao hicho kimeonekana kuwa hivyo ndani ya misimu saba ambayo timu hiyo imekuwa ndani ya Ligi Kuu Bara.

Sababu kubwa iliyo nyuma ya hilo kwa msimu huu, imeelezwa ni aina ya wachezaji wanaounda kikosi hicho ambapo wamekuwa hawana uwiano mzuri katika kufunga mabao na kuzuia nyavu zao zisitikiswe.

KMC iliyocheza mechi 25 msimu huu, imekusanya pointi 27 zilizotokana na kushinda mechi saba, sare sita na kupoteza 12, huku ikifunga mabao 20 na kuruhusu 38.

Katika orodha ya timu zilizoruhusu mabao mengi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, KMC ni ya tatu nyuma ya KenGold (48) na Fountain Gate (47). Suala la kutokuwa vizuri kwenye ulinzi, limekuwa likiitesa zaidi KMC kwa misimu minne mfululizo sasa.

Katika msimu ambao KMC ilikuwa bora zaidi, ni ule wa kwanza 2018-2019 ambapo kikosi hicho kilimaliza ligi nafasi ya nne ambayo hadi sasa wameshindwa kuifikia.

Msimu huo ubora wao ulionekana kwenye maeneo mengi kwani ilifunga idadi kubwa ya mabao (40) na kuruhusu machache zaidi (25) huku ikikusanya pointi nyingi (55).

Takwimu hizo zilikuwa bora kwa KMC, licha ya kwamba pia mechi zilichezwa nyingi (38) kulinganisha na sasa ambazo ni 30, lakini ukiangalia wastani ulikuwa mzuri.

Kwa sasa KMC imebakiwa na mechi tano zenye jumla ya pointi 15, hivyo ina hesabu kali kuhakikisha inazikusanya zote na kufikisha 42 ambazo zitawafanya si kubaki kwenye ligi bali kufikisha pointi ambazo imeshindwa kuzifikia kwa misimu mitatu mfululizo sasa.


HALI ILIVYO

Mwanzoni mwa msimu, KMC ilikuwa na Kocha Abdihamid Moallin ambaye katikati akatimkia Yanga, kisha Novemba 14, 2024, Kali Ongala alikabidhiwa mikoba yake.

Kocha huyo tangu akabidhiwe kikosi cha KMC, amekiongoza kwenye mechi 13 za ligi, akishinda tatu zote nyumbani na kupoteza sita, kati ya hizo nne nyumbani, huku sare ni nne.

Kwa jumla, KMC msimu huu kwenye ligi imecheza mechi 25, ikishinda saba, sare sita na kupoteza 12 ikikusanya pointi 27. kwa misimu minne ya hivi karibuni KMC imeonekana kusumbuliwa na safu ya ushambuliaji sambamba na ulinzi wakifunga mabao machache na kuruhusu mabao mengi.

Timu hiyo pia msimu huu haina rekodi nzuri mechi za ugenini ikiwa nafasi ya 12 kwa timu zilizokusanya pointi chache ugenini ambazo ni saba pekee. Imeshuhudiwa ikishinda mechi moja pekee ugenini na kupoteza saba kati ya 12, sare ni nne.

Ongala ana kazi kubwa ya kufanya, ukiangalia wastani wake wa kushinda hauridhishi kwani mechi tatu alizoshinda zimepishana muda mrefu.

Ushindi wa kwanza ulikuwa Desemba 16, 2024 wa bao 1-0 dhidi ya Pamba Jiji kupitia mfungaji Hance Masoud dakika ya 88. Baada ya hapo, akakaa kwa siku 56 ndipo Februari 10, 2025 aliposhinda tena mabao 2-0 dhidi ya Singida Black Stars kwa mabao ya Oscar Paul dakika ya 35 na 40, kisha Aprili 2 akaichapa Tanzania Prisons 3-2, wafungaji ni Shaban Idd Chilunda dakika ya 41 na 66, huku Ibrahim Elias akifunga dakika ya 55.

Safu ya ushambuliaji ya KMC inaendelea kuwa butu kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo walifunga mabao 27 na msimu huu wakiwa na mabao 20. Ukuta wa KMC pia umeendelea kuruhusu mabao mengi, msimu uliopita walifungwa 39, msimu huu wameruhusu mabao 38 zikibaki mechi tano.

Wanachokipitia sasa KMC ni sawa na msimu wa 2022/23 ambapo kwenye mechi 30 walizocheza msimu huo walikusanya pointi 32 ambazo ziliwafanya wawe nafasi ya 13 kwenye msimamo wakifunga mabao 25, hivyo safu yao ya ushambuliaji ni butu msimu wa tatu mfululizo.

Wakati msimu wa 2021/22 timu hiyo iliendelea kutokuwa bora kwenye safu zote za ushambuliaji na ulinzi kwenye mechi 30 walizocheza walifunga mabao 34 wakiruhusu 35 wakimaliza nafasi ya 10 kwenye msimamo.

MECHI ZA KUAMUA

Kutokana na kutokuwa na rekodi nzuri ugenini, ni wazi KMC inapaswa kucheza kikubwa nyumbani mechi mbili zijazo dhidi ya Dodoma Jiji na Simba kwani baada ya hapo, itaenda ugenini kucheza mechi tatu za kumaliza msimu.

Rekodi zinaonesha msimu huu ilipocheza duru la kwanza dhidi ya Dodoma Jiji, ilipoteza kwa bao 2-1, pia ikafungwa 4-0 na Simba. Mbali na hizo, dhidi ya timu ambazo itakwenda kucheza nazo ugenini, matokeo ya duru la kwanza yalikuwa hivi; KMC 0-2 Tabora United, KMC 0-0 Mashujaa na KMC 1-0 Pamba Jiji.


OSCAR PAUL

Huyu ndiye mshambuliaji anayeonekana kuibeba timu, licha ya namba zake kutokuwa nzuri kulinganisha na ushindani ulivyo kwenye ligi, lakini ndani ya KMC ndiye kinara wao akifunga mabao matano kati ya 20 yaliyofungwa na timu hiyo.

Mshambuliaji huyo ana kazi kubwa ya kufanya ili kuipambania timu hiyo kuongeza namba za mabao kwenye mechi tano zilizobaki, lakini safu ya ulinzi yenye wachezaji kama Andrew Vincent, Ismail Gambo na Hance Masoud nayo inahitaji kujitafakari.


MWENDO WAO KWENYE LIGI

KMC ilikuwa vizuri zaidi katika msimu wa kwanza ambapo nafasi ya nne iliyomaliza, imekuwa ndoto kwao hadi sasa ambapo inacheza katika nafasi za mbali sana, Msimu wa 2019-2020, 2022-2023 na 2024-2025 ilikuwa ya 13, huku 2021-2022 ikikamata nafasi ya 10. Kidogo 2023-2024 ilipanda hadi nafasi ya tano. 

MSIKIE ONGALA

Kocha huyo anasema tangu apewe majukumu ya kuiongoza KMC licha ya changamoto mbaya ya matokeo lakini anaona mabadiliko ambayo kimsingi yanampa matumaini ya kukwepa kushuka daraja kutokana na vijana wanavyopambana na tayari wameanza kuingia kwenye mfumo.

Anasema hata hivyo timu hiyo haikuwa vibaya kifundi, isipokuwa inakosa bahati katika kupata matokeo mazuri, jambo ambalo kwa sasa anaona wazi mambo yanaenda vizuri.

“Mapungufu yapo lakini pia kuna mengine mazuri, kwa hiyo mimi naangalia kipi nikiongeze na nipunguze nini, ila kwa ujumla timu ipo vizuri na ishu ya kushuka daraja haipo, licha ya kuwaacha wapinzani kwa poindi chache hatuwezi kufanya makosa yatakayotugharimu,” anasema.

Kocha huyo aliongeza kuwa mkakati wake ni kurekebisha haswa safu ya ulinzi na ushambuliaji ambayo ndio inahusika na ufungaji mabao lakini atafanyia kazi maeneo mengine ili kufikia malengo yao.

“Sehemu nitakayofanyia marekebisho haswa ni ushambuliaji japo wachezaji wote nitawapa maelekezo ili kufikia malengo yetu, mchezo wa mwisho (dhidi ya Tanzania Prisons) tumeshinda kwa idadi kubwa ya mabao lakini safu ya ulinzi imeniangusha kwa kuruhusu wapinzani kufumania nyavu zetu,” anasema kocha huyo.