DAKIKA ZA JIOOONI: JKT Tanzania mipango imewalipa

Muktasari:
- Katika kuzichanga karata hizo, kocha wa timu hiyo, Ahmed Ally akatua kikosini hapo na sera moja ya, kama timu haiwezi kufunga mabao ya kutosha, basi isiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nyingi. Hali hiyo ndiyo imeendelea kuibeba JKT Tanzania na kuonekana kuwa ngumu kwa wapinzani.
KILICHOTOKEA msimu uliopita kwa JKT Tanzania ni kama kimekuwa funzo kubwa kwa timu hiyo msimu huu baada ya kuzichanga karata zao mapema na mipango imewalipa.
Katika kuzichanga karata hizo, kocha wa timu hiyo, Ahmed Ally akatua kikosini hapo na sera moja ya, kama timu haiwezi kufunga mabao ya kutosha, basi isiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nyingi. Hali hiyo ndiyo imeendelea kuibeba JKT Tanzania na kuonekana kuwa ngumu kwa wapinzani.
Kocha huyo alitua kikosini hapo Juni 2024, akaanza kuiandaa timu katika maandalizi ya msimu huu na hadi sasa amekuwa miongoni mwa makocha watatu ambao wamesalia na timu walizoanza nazo. Wengine ni Fadlu Davids (Simba) na Mecky Maxime (Dodoma Jiji).
JKT Tanzania licha ya kwamba haipo nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, lakini imekuwa na maajabu yake ndani ya uwanja kiasi cha kuifanya kubakisha hatua chache za kuwa salama zaidi.

Umoja uliopo ndani ya timu hiyo kuanzia safu ya beki hadi ushambuliaji, ndiyo unaibeba zaidi na huu ni msimu wa pili kushiriki Ligi Kuu Bara.
Wakati msimu uliopita 2023/24 ikimaliza nafasi ya 13 kwenye msimamo na kulazimika kucheza mechi za mtoano 'play off' kupambania nafasi ya kubaki kwenye ligi, kikosi hicho kilikuwa kinanolewa na Malale Hamsini ambaye alifanikiwa kuibakisha timu.
Msimu huo JKT Tanzania ilimaliza na pointi 32 katika mechi 30, ikishinda sita, sare 14 na kupoteza 10. Ilifunga mabao 21 na kuruhusu 30.
Kuanzia hapo, JKT Tanzania imejengwa upya kupitia Ally ambaye hivi sasa katika mechi 25 zikibaki tano kumaliza msimu, amezifikia pointi za msimu uliopita (32), huku pia akipunguza mabao ya kufungwa na kufikia 21, huku akiongeza mabao ya kufunga ambayo ni 22. Inashika nafasi ya saba kwenye msimamo.
Ukweli usiopingika ni kwamba, kocha huyo wa zamani wa Tanzania Prisons, ameibadilisha kwa kiasi kikubwa JKT Tanzania kupitia sera yake ya 'tusipofunga, tusifungwe' ambapo kikosi hicho kimepoteza mechi moja pekee nyumbani msimu huu kama ilivyo Simba.

Kati ya timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, JKT Tanzania na Simba pekee ndizo zimepoteza mechi moja nyumbani msimu huu jambo linalomuweka Kocha Ally katika nyakati nzuri kwenye majukumu yake. Katika mechi 13 za nyumbani, imeshinda nne, sare nane na kupoteza moja.
Wakati kocha ufundi wake ukiwa hivyo, ndani ya uwanja kuna wachezaji wanaongoza safu ya ushambuliaji vizuri kwa kupachika mabao. Katika mabao 22 ya JKT Tanzania, Edward Songo amefunga matano, Najim Magulu (2), Said Juma (2) na John Bocco (2), pia beki wao Wilson Nangu anayo mawili, hivyo anaifanya kazi ya kulinda na kufunga.

HUYU HAPA KOCHA
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally anasema: "Nimeitengeneza timu kwa uwiano sawa kama haifungi mabao mengi basi isifungwe mabao mengi, ndio maana mtu yeyote kikosini anaweza kufunga, mfano beki Nangu ana mabao mawili, nafanya hivyo kuondoa mzigo kwa washambuliaji."
Kocha huyo anasema mechi zilizosalia anaamini zitawafanya wamalize nafasi za juu zaidi ya hiyo ingawa hakuwa tayari kusema ni ipi, kikubwa anachosisitiza ni kuhakikisha wachezaji wanafanya kazi bila msongo wa mawazo.
"Kitu kikubwa ninachowafundisha wachezaji ni kuhakikisha wanafanya kazi bila presha, wanapoingia uwanjani wawe na moyo wa kujitolea kwa ajili ya timu na ndicho wanachokifanya, wakati mwingine wakongwe waliopo kama Bocco anasaidia hamasa kwa wachezaji wenzake," anasema kocha huyo.

Kwa upande wa straika Edward Songo anayeongoza kwa mabao kikosini hapo, anasema: "Japokuwa ligi ilipofikia ni ngumu, lakini tutapambana kadiri tuwezavyo kufikia malengo yetu, ingawa naona msimu huu tupo vizuri tunaweza tukapata pointi zaidi ya 32 ambazo tulimaliza nazo msimu uliyopita."
Mtazamo wake haujatofautina na wa winga wa timu hiyo, Shiza Kichuya anayesema: "Ni msimu mzuri na mgumu, jambo la msingi tunatamani kumaliza nafasi tano kama siyo sita za juu."

MECHI ZILIZOSALIA
TZ Prisons v JKT Tanzania (Aprili 18)
JKT Tanzania vs Simba (Mei 5)
JKT Tanzania vs Fountain Gate (Mei 13)
Pamba Jiji vs JKT Tanzania (Mei 21)
Mashujaa vs JKT Tanzania (Mei 25)