DANNY: Nilipewa simu nikasaini dili Simba

JANA tulianza kukuletea mfululizo wa mahojiano na Danny Mrwanda akazungumzia mambo mbalimbali ikiwemo rasilimali zake. Endelea na sehemu ya pili ambapo anasema kilichomtoa Simba na kumpeleka Rwanda kucheza soka la kulipwa ni tuhuma za kuchezaji chini ya kiwango dhidi ya Yanga.
“Mechi ile ilifanyika Morogoro, Simba tulishinda kwa penalti ila nilikosa, kabla ya mechi kuna maneno yalivumishwa wachezaji watano tumepewa pesa na Yanga, iliniumiza sana ukizingatia mimi nilicheza kwa moyo Simba, wakati ule tulilipwa pesa kwa kuunga unga, mwenyekiti akiwa Wambura.
“Iliniumiza mchezaji unajitolea lakini watu wanakuona msaliti, tuhuma zile ndizo zilichochea niende Police Rwanda, niliwambia sina tena morali ya kucheza Simba, hivyo nikaondoka.
“Nikiwa Rwanda walifuatilia na kugundua sio kweli, ndiyo sababu nilivyorudi walinipokea tena,” anasema.
KURUDI LIGI KUU
“Kubaki Ken Gold msimu ujao sina uhakika kwa asilimia 100, lolote linaweza kutokea, nimekuwa na msimu mzuri Ken Gold, wamenipa nafasi ya kufanya shughuli zangu nyingine nje ya soka.
“Unafahamu kwa sasa tunatafuta riziki ndogo ndogo, hivyo sina sababu za kuanza purukushani za ligi kuu kama vile kwenda kambini saa 12 asubuhi na mambo kama hayo, hivyo nimeona kwa utaratibu huo tutagombana ndiyo sababu nimeamua nikae kwenye timu ambayo inanielewa.
“Ikitokea timu ya Ligi Kuu, inanihitaji, tukikubaliana ikanipa nafasi ya kufanya kazi zangu nyingine, japo siyo tageti lakini ikitokea nitaangalia na ofa yenyewe.”
KUSAIDIA YANGA
Kumewahi kuwa na tetesi za Mrwanda kuisaidia Yanga ambayo ilikuwa imekwama kifedha.
Huku akicheka Mrwanda anasema hivyo vitu vinatokea, sio kwa Yanga tu hata Majimaji ilishawahi kukwama ikiwa Shinyanga akaisaidia. “Sio vizuri kuyazungumzia hayo kwa kuwa yalishapita, lakini wakati mwingine nikitoa kuna watu wana nirudishia pesa yangu, hivyo nisilizungumzie sana hilo.”
MAPRO ANAOWAKUBALI
Katika usajili wa Mapro, Mrwanda anasema wapo waliokuja nchini wanaonyesha kweli wamekuja kikazi akimtolea mfano Chriss Mugalu.
“Huyu ni aina ya wachezaji ambao mimi kama mshambuliaji najua umuhimu wake japo baadhi ya watu wanamuona hana msaada lakini ukimuweka eneo lake anafanya kitu kinaonekana.
“Pia Bwalya, Banda, Haruna Niyonzima na baadhi ya wachezaji walikuja na kufanya kitu, sio mchezaji kama Morrison (Bernard) binafsi naona kama anatufanyia drama kwenye soka letu,” anasema.
“Kuna wachezaji wanakuja nchini sisi ndiyo tunawapa kiburi, nchi nyingine hawaruhusu, nakumbuka wakati niko Vietnam kuna mchezaji raia wa Brazil alikuwa mfungaji bora misimu mitatu, alileta ukorofi FA ya kule haikumruhusu kucheza tena pale, aliondoka.
“Hapa kwetu kuna wachezaji tunawalea sababu tu ya siasa zetu za mpira, lakini tunao wachezaji wengi wenye kiwango zaidi ya Morrison, kama vile Nkane au Ngushi leo ukisema uwape nafasi na kuwaamini watafanya vizuri sana, tatizo ni kuwaamini,” anasema.
KILICHOMTOA SIMBA KWENDA YANGA
Mrwanda ambaye alicheza Yanga msimu mmoja anasema; “Simba ni timu ambayo nilipokuwa nikipata nafasi ya kwenda nje ya nchi wananiruhusu na nikirudi wananipokea, nilipotoka Vietnam nilikuwa na ofa kwenye timu tatu, lakini niliipa kipaumbele Simba,”.
“Vitu nilivyohitaji wanifanyie kwenye mkataba wangu walishindwa, Yanga walikuwa tayari hivyo nikaenda huko,” anasema Mrwanda ambaye ni miongoni mwa wachezaji waliocheza nje kwa mafanikio. “Wakati huo natoka AFC Arusha, sikuwa naangalia maslahi, nilitakiwa na Simba na Yanga, ndoto yangu ilikuwa ni kucheza nje ya nchi, nikaambiwa kama unahitaji kutoka nenda Simba,” anasema.
ASAJILIWA KWA SIMU YA MOTOROLA
Kwa miaka ya 2000, simu ya mkononi ilikuwa ni dili, ukiwa una miliki simu unaonekana wakishua, bila kujali ni aina gani ya simu, hata usajili wa Mrwanda ulinogeshwa na simu ya mkononi ya motorola.
“Alinipa Kaburu wakati ule, nikawa napewa mshahara wa Sh 120,000 kwa mwezi na pesa ya usajili niliyopewa ilikuwa Sh 3 Milioni.
“Nilitoka AFC Arusha hakuna mshahara wala nini, labda siku tukicheza na Simba au Yanga tunapewa posho Sh 50,000, hivyo kujiunga Simba sikuangalia masilahi, zaidi nilitaka kutoka.”
Anasema pesa yote ya usajili huo aliwapa wazazi wake, wao ndio wakamgawia Sh 1.5 Milioni ambazo ndio alinunua kitanda alichoanzia maisha.
“Nilikinunua Sh 400,000 pale Keko, mpaka leo ninacho uwa nakipaka rangi tu, ni kitanda cha ukumbusho kwangu kwa kuwa ndio nimeanzia maisha siwezi kukitupa,” anasema.
UKIMCHEZEA FAULO, LAZIMA AILIPE
“Mimi sio muoga, nikichezewa faulo nitalipa tu, nakumbuka nikiwa Vietnam waliweka masharti nikipata kadi ambayo haikuwa ya lazima wananikata mshahara.
“Kuna muda unafanyiwa kitendo ambacho si cha uungwana uwanjani, lakini ukirudishia wewe ndiye unaonekana mkororofi, nilipokatwa mshahara mara mbili tatu kule ikabidi niwe mpole.
“Kuna mechi ya Simba na Yanga ilikuwa ngao ya hisani, Kessy Hassan akiwa Simba mimi niko Yanga alifanyia faulo ya makusudi, nilihamaki, ikabidi kocha anifanyie ‘sub’ mapema.
“Ingawa pia kuna dabi, nilipewa kadi nyekundu, sijui kama ilikuwa ni halali, Amri Maftah nilimmudu
kwenye 18 ile naenda kufunga akanichezea faulo, refa kasema nimejiangusha akanipa kadi nyekundu,” anasema.
USHIRIKINA MECHI ZA DABI
“Yamefanyika sana na ndivyo vitu vinachangia mechi ya dabi hiyo iwe mbovu, ilikuwa ikikaribia mechi hiyo kila kitu kinabadilika.
“Kuna muda wachezaji mnany-ang’anywa simu, viongozi walikuwa hawajui tu, kwa kufanya hivyo inamvuruga mchezaji kisaikolojia, anaweza kukosa nafasi ya wazi kwa kuwa wameshajengewa hofu.
“Nakumbuka nikiwa Simba, tuliweka kambi Ubungo Plaza kujiandaa kucheza na Yanga, alikuja mke wangu kunitembelea, nikiwa nazungumza naye, kuna komandoo amekaa pembeni anasikiliza mazungumzo yetu, kisa tu kuhofia hujuma.
“Huu sio mpira tena ni kama uko jela, pale akili ya mchezaji inavurugika, lakini pia masuala ya kishirikina, haikuwa Simba tu, hata Yanga walikuwa wakifanya, sisi wachezaji tunaelekezwa tu.
“Kuna muda mnaambiwa mkifika uwanjani eneo fulani msipite au muingie kwa staili ya namna ambavyo mnaelekezwa, lakini kuna muda tunafanya hayo na bado tunafungwa maana waganga nao ni wafanyabiashara,” anasema.
MAISHA WANASOKA NJE YA NCHI
Licha ya baadhi ya wanasoka wa Tanzania kukwaa kisiki wanapokwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na wengi wao kurudi nchini baada ya muda mfupi, Mrwanda anasema changamoto za kucheza nje ya nchi zipo nyingi.
“Unaweza kusaini mkataba wa kulipwa mshahara dola 10,000 lakini hiyo ni ya kwenye makaratasi, lakini unachokipokea kinaweza kuwa dola 4000 tu, makato kule ni makubwa.
“Kwa mshahara wa dola 4000, ukichanganya na gharama za maisha nje ya nchi zilivyo juu, mchezaji anaona bora arudi nyumbani apate timu ya kumlipa dola 2500 kwa mwezi akiwa nyumbani.
“Kuliko kucheza nje ili uonekane ili kuwafurahisha watu ni bora ukarudi nyumbani tu kucheza hapa, maisha ya soka nje ya nchi yanahitaji upambanaji,” anasema Mrwanda aliyewahi kucheza soka la kulipwa Kuwait, Vietnam, Sweden na Rwanda.
MIPANGO YA UKOCHA
“Niliwahi kufanya kozi kadhaa, japo ni kazi yenye presha sana tofauti na kuwa mchezaji.
“Unajua ukiwa uwanjani unacheza, ukikosea unaweza kujirekebisha, lakini kwenye ukocha unaona kabisa yule mchezaji anakosea ila huwezi kuingia uwanjani kumrekebisha, unabaki tu kutoa maelekezo ukiwa nje ya uwanja, ni kazi ya presha sana.”
KEN GOLD YAMPA PRESHA
Katika miaka 20 ya soka, Mrwanda anasema hajawahi kuumizwa na matokeo kama waliyowahi kupata timu yake ya sasa ya Ken Gold ilipofungwa na Mwadui.
“Ile mechi iliniumiza sana, sababu tulifanya kila kitu lakini tulifungwa kwa uzembe, utulivu wa kambi ulipotea, ilinifanya nipotee kwenye mazingira ya timu wiki nzima.
“Sikutaka kabisa kuonekana, ilikuwa ni mechi ambayo kiukweli tulifungwa kwa uzembe, sikuwa kuumizwa na matokeo ya mpira kama ya ile mechi, wakati huo Mwadui ikiwa inaning’inia mkiani,” anasema.
Msimu huu Mrwanda ameifungia Ken Gold mabao 13, mawili akifunga dhidi ya Transit Camp, matatu dhidi ya Mwadui na kwenye mechi dhidi ya Gwambina, JKT Tanzania, Mashujaa, DTB, Kitayose, Green Warriors, Pan African na African Lyon amefunga bao moja moja. Mwisho.