Prime
Fainali CAFCC: Tripu hii, ngoja tuone!

Muktasari:
- Timu hiyo imetinga hatua hiyo baada ya kupata ushindi wa jumla wa bao 1-0 dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, ikishinda nyumbani bao 1-0 lililofungwa na Jean Charles Ahoua, kisha kutoka suluhu ugenini.
SIMBA imekata mzizi wa fitina. Imetinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kusota kwa muda mrefu.
Timu hiyo imetinga hatua hiyo baada ya kupata ushindi wa jumla wa bao 1-0 dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, ikishinda nyumbani bao 1-0 lililofungwa na Jean Charles Ahoua, kisha kutoka suluhu ugenini.
Simba ilianza kuondoa gundu la kushindwa kuvuka robo fainali kwenda nusu kwa kuizima Al Masry ya Misri baada ya kuanza kwa kupoteza ugenini 2-0 na kushinda nyumbani ziliporudiana pia kwa mabao 2-0, yaliyowekwa kimiani na Ellie Mpanzu na jingine la Steven Mukwala.
Mabao hayo yaliiweka Simba katika nafasi nzuri ya kufuta gundu lililodumu kwa misimu sita iliyopita ikikwamia hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF kuanzia Ligi ya Mabingwa hadi hiyo ya Shirikisho tangu 2018-2019.
Kama hujui kabla ya mechi hiyo dhidi ya Al Masry, Simba ilishacheza robo fainali nne za Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023 na 2023-2024 sambamba na moja ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2021-2022, huku 2019-2020 ikitolewa mapema.

Matokeo iliyopata Simba imeifanya irejee tukio ililowahi kulifanya mwaka 1993, ilipofika fainali ya Kombe la CAF (haipo kwa sasa) na kupoteza mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast kwa mabao 2-0 ikiwa nyumbani baada ya suluhu ya ugenini jijini Abdijan, Ivory Coast.
MAAJABU YA 1993
Unaweza kudhani ni utani, ila yale maajabu ya yaliyotokea 1993 yametokea msimu huu kuanzia hatua ya robo fainali hadi kufika fainali.
Ndiyo, kama hujui, katika michuano hiyo iliyotokana na Kombe lililotolewa na aliyekuwa Mwanasiasa na Mfanyabiashara maarufu wa Nigeria, Chief Moshoodi Abiola (sasa marehemu) mwaka 1992, Simba ilitinga nusu fainali kwa kuing'oa klabu kutoka Afrika Kaskazini kama ilivyotokea msimu huu kwa Al Masry na hata hata kutinga fainali kwa kuitoa timu ya Ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Simba iliitungua USM El Harrach ya Algeria kwa kuifunga jumla ya mabao 3-2, ikianza na ushindi wa mabao 3-0 nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), kisha kwenda kulala ugenini 2-0 na kuwashangaza Waalgeria.

Kilichotokea 1993 ni kama tu ilivyotokea msimu huu kwa Simba kuwaduwaza Al Masry ya Misri ambao iliyoambulia penalti moja tu kati ya tatu ilizopiga baada ya kipa Moussa Camara wa Simba kupangua mikwaju miwili ya Al Masry kwenye Uwanja wa Mkapa. Simba ilianza kulala ugenini 2-0 na kushinda nyumbani idadi kama hiyo ndipo ikaamuliwa penalti na Mnyama kutumia 4-1.
Kazi aliyoifanya Camara ni kama tu ilivyokuwa kwa 1993, wakati kipa Mohammed Mwameja alipofanya kazi kubwa kuikatili Al Harrach akiivusha Simba hadi nusu fainali.
Katika mechi ya kwanza nyumbani iliyopigwa Septemba 5, mabao mawili yalifungwa na Edward Chumila na jingine la Abdul Ramadhan 'Mashine' na kuihakikishia Simba tiketi ya nusu, licha ya kulala 2-0 ugenini iliporudiana na Al Harrach Septemba 18, 1993.
YAPENYA COSAFA
Ushindi huo wa 3-2 ulioivusha Simba hadi nusu fainali, uliifanya ipangwe kukutana na timu ya Atletico Sport Aviacao (ASA) ya Angola ambayo ni klabu kutoka Ukanda wa Soka wa Kusini mwa Afrika (COSAFA).
Kumbuka tu, msimu huo Aviacao ilikuwa ikishiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo ya CAF iliyokuwa ndiyo kwanza ina msimu wa pili tangu ilipoasisiwa 1992 na iliitoa Gor Mahia ya Kenya kwenye robo kwa penalti 4-2 baada ya matokeo ya jumla kuwa 0-0.

Haitofautiani kabisa na msimu huu, kwani Simba sasa ilikutana na Stellenbosch ya Afrika Kusini ambao ni klabu kutoka Ukanda wa Cosafa pia, lakini ikishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.
Stellenbosch iliiduwaza waliokuwa watetezi, Zamalek kwa kuitungua kwa bao 1-0 ziliporudiana jijini Cairo, baada ya awali kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza.
Kama ilivyokuwa mwaka 1993 kwa Simba kuanzia nyumbani dhidi ya Aviacao, ndivyo ambavyo hata safari hii ilivyokuwa kwa kuikaribisha Stellenbosch Aprili 20 na kushinda bao 1-0 na kwenda kutoka suluhu ugenini kama ilivyotokea dhidi ya Aviacao mwaka 1993.
Katika mechi ya kwanza nyumbani iliyochezwa Oktoba 17, 1993, Simba ilipata ushindi wa 3-1, mawili kupitia tena Chumila na jingine lililokuwa la pili la kujifunga, huku bao la kujifuta machozi la Aviaco likifungwa na Nello.

Timu hizo zilipoenda kurudiana Oktoba 31, Simba ikiwa ugenini ililazimisha suluhu na kutinga fainali.
Katika mechi zote mbili, kazi kubwa ilifanywa na kipa Mwameja aliyeokoa michomo mikali ya kina Otis Mongaa Libengue 'Libengue', Keleki wa Keleki, Lolo, Maneco, Manuel Domingos Martin 'Manuel', Mariano, Miramba, Nzinga Lubusa, Nello na Yanda, huku kipa Kanka Vemba akijaribu kuipigania timu bila mafanikio kuwazuia Wekundu isivuke.
Mwameja aliwakatisha tamaa Waangola wakiwa kwao, kiasi mashabiki wa timu hiyo kufikia hatua ya kumrushia mawe na takataka nyingine zilizosababisha mara kadhaa pambano hilo kusimamishwa na dakika 90 ziliiisha kwa Aviacao iking'oka kwa mabao 3-1 na kutinga fainali dhidi ya Stella.
Hapo ndipo kumekuwa tofauti, kwani safari hii Simba imekutana na RS Berkane inayokea Afrika Kaskazini na sio klabu ya Ukanda wa Afrika Magharibi kama ilivyotokea 1993 na kupoteza kwa matokeo ya jumla ya 2-0.

Kama Simba itabeba taji hilo mbele ya Berkane, basi itaivunja rekodi ya watani wao Yanga iliyocheza fainali msimu wa 2021-2022 dhidi ya USM Alger ya Algeria na kulikosa taji kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini.
Yanga ilipoteza nyumbani kwa mabao 2-1, lakini ikaenda kushinda ugenini jijini Algiers kwa bao 1-0 lililotokana na na penalti ya aliyekuwa beki wa timu hiyo, Djuma Shaban na kufanya matokeo ya jumla kuwa mabao 2-2 na wenyeji kutawazwa mabingwa wapya.

KIKOSI CHA 1993
Simba iliyotinga fainali za Kombe la CAF 1993 kilikuwa chini ya Kocha Abdallah 'King Mputa' Kibadeni na Etenne Eshente raia wa Ethiopia aliyekuwa kocha msaidizi, huku meneja wa timu akiwa ni Abdulrahman Muchacho.
Nyota wa kikosi hicho walikuwa ni pamoja na makipa Mohammed Mwameja, Mackezie Ramadhan na Offen Martin, Kassongo Athuman, Razack Yusuf 'Careca', George Masatu, Seleman Pembe, Fikiri Magosso, Idd Seleman 'Meya' a.k.a Nyigu na George Lucas 'Gazza'.
Wengine ni Abdul Ramadhan 'Mashine', Damian Kimti, Ramadhan Maufi 'Lenny', Edward Chumila, Dua Said, Malota Soma 'Ball Juggler', Twaha Hamidu 'Noriega' , Deo Mkuki, Godwin Aswile 'Scania', Hussein Masha 'Smart Boy', Abuu Omar, Joachim Masumbuko, Nico Kiondo, Bakar Idd 'Beka Jo', David Mihambo, Mbuyu Yondani, Michael Paul 'Nylon', Thomas Kipese 'Uncle Tom', Feruzi Teru na Rashid Abdallah.
KIKOSI CHA SASA
Kwa msimu huu Simba inanolewa na Kocha kutoka Afrika Kusini, Fadlu Davids akisaidiwa na mzawa, Seleman Matola, nyota na nahodha wa zamani wa kikosi hicho kama ilivyokuwa kwa King Kibadeni aliyeiongoza Simba ya 1993, huku meneja akiwa Patrick Rweyemamu.
Makipa ni Moussa Camara, Ally Salim, Hussein Abel na Aishi Manula, huku mabeki ni; Karaboue Chamou, David Kameta 'Duchu', Hussein Kazi, Shomary Kapombe, Abdulrazak Hamza, Fondoh Che Malone, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Kelvin Kijili na Valentin Nouma.
Wengine ni; Fabrice Ngoma, Joshua Mutale, Omary Omary, Jean Charles Ahoua, Debora Mavambo, Augustine Okejepha, Mzamiru Yasin, Yusuf Kagoma, Kibu Denis, Awesu Awesu, Ladack Chasambi, Edwin Balua, Ellie Mpanzu, Steven Mukwala, Valentino Mashaka na Leonel Ateba.