Havertz alivyomhonga Sophia medali ya UEFA

Muktasari:
- Mafanikio hayo yana maana kwa Havertz ila maana kubwa ipo kwa ubavu wake wa kushoto, yaani mkewe Sophia Weber, 24, ambaye kamhonga vingi tangu 2018 ikiwamo medali yake ya michuano hiyo kama zawadi ya bethidei.
Kati ya mafanikio makubwa katika soka ngazi ya klabu kwa kiungo mshambuliaji wa Ujerumani, Kai Havertz, 25, anayekipiga Arsenal FC kwa sasa, ni kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA) 2020/21 huko Porto, Ureno.
Mafanikio hayo yana maana kwa Havertz ila maana kubwa ipo kwa ubavu wake wa kushoto, yaani mkewe Sophia Weber, 24, ambaye kamhonga vingi tangu 2018 ikiwamo medali yake ya michuano hiyo kama zawadi ya bethidei.
Havertz alikuwamo katika kikosi cha Chelsea FC kilichoivaa Manchester City katika fainali ya UEFA 2020/21 iliyochezwa Estadio do Dragao na kuhudhuriwa na mashabiki takribani 14,000 kutokana janga la Corona wakati huo.

Fainali hiyo iliyopigwa Mei 29, 2021, Havertz alifunga bao pekee la ushindi dakika za mwishoni kipindi cha kwanza na hivyo kuipatia Chelsea ubingwa wa pili wa UEFA baada ya kufanya hivyo msimu wa 2011/12.
Sophia, mzaliwa wa Ujerumani anayejishughulisha na mitindo na ushawishi wa chapa mtandaoni, alikuwapo katika fainali hiyo ya aina yake na kupiga picha ya ukumbusho pamoja na Havertz wakiwa wameshikilia kombe hilo.

Cha kufurahisha ni kwamba picha hiyo ilipigwa siku moja baada ya Sophia kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, kwa hiyo kitendo cha kumshuhudia mumewe akifunga katika fainali hiyo ilikuwa ni zawadi kubwa kwake.
Usiku huo wa baridi kali ya Ulaya, Chelsea iliondoka uwanjani na kombe lake, huku Havertz akiondoka na medali yake, hakuna ubishi kuwa mtu wa kwanza kuivaa baada yake ni Sophia ambaye alizaliwa Mei 28, 2000.

Mrembo huyo amekuwapo katika safari ya mafaniko na hata panda shuka za Havertz katika soka kwa kipindi chote, anastahili chochote kile kizuri kutoka kwake, iwe ni mkufu wa Tanzanite kutokea Mererani au safari ya kula ngisi na pweza huko Kizimkazi.
Uhusiano rasmi wa wawili hao ulianza mwaka 2018 wakati Havertz akichezea Bayer Leverkusen alipohudumu kati ya 2016 hadi 2020 akiichezea timu hiyo ya Ujerumani mechi 118 na kufunga mabao 36.
Hata hivyo, vyanzo vingine zinaeleza kuwa Sophia na Havertz walifahamiana kitambo kidogo na walikuwa na urafiki mzuri wa faragha ila mwaka 2018 ndipo wakaamua kuweka wazi jambo hilo kwa umma na mengine sasa ni historia tu.
Baada ya Havertz kuachana na miamba hiyo ya Bundesliga hapo mwaka 2020 na kujiunga na Chelsea, mabingwa wa EPL mara sita, naye Sophia alihamia London na kuwa mshangiliaji mkubwa wa mchezaji huyo ndani na nje ya uwanja.
Ni mwaka huo huo Sophia alijiunga na mtandao wa kijamii wa Instagram ambao anautumia kutangaza kazi zake za urembo na mitindo akiwa na wafuasi zaidi ya 540,000 huku akitumia jina la Sophia Havertz badala ya Sophia Weber.

Ingawa hakuna taarifa nyingi kuhusu maisha yake binafsi na shughuli zake kwa ujumla ila amewahi kufanya kazi na chapa ya mavazi ya Lunilou na Puma huku utajiri wake ukikadiriwa kufikia Dola 1 milioni kwa mwaka 2024.
Sophia na Havertz walichumbiana Julai 2023 na kuthibitisha hilo kupitia chapisho lao la Instagram, na mwaka mmoja baadaye, yaani Julai 18, 2024 wakafunga ndoa ikiwa ni muda mfupi baada ya kumalizika michuano ya Euro iliyofanyika nyumbani kwao Ujerumani.
“18.07.24 - pamoja milele,” wawili hao wali-andika Instagram wakiambatanisha na picha zao za harusi na kupokea jumbe nyingi za pongezi kutoka kwa wafuasi na mashabiki wao.
Hata hivyo, wiki moja kabla ya ndoa yao ambayo ilikuwa ya faragha zaidi ikihudhuriwa na marafiki, watu wa karibu na familia yao, walifanya tafrija ya kipekee katika kisiwa cha Ibiza nchini Hispania.
Sophia amekuwa msaada wa mara kwa mara kwa Havertz katika maisha yake yote hasa katika nyakati ngumu uwanjani, na kwa upande wake Havertz amewahi kumshukuru Sophia kwa hilo akimtaja kama mtu muhimu kwake katika vipindi vigumu vya soka.
Novemba 2024 wawili hao walitangaza kuwa wanatarajia mtoto wao kwanza ambaye bado hajazaliwa. Sophia alitumia Instagram na kusema, “Baraka yetu kubwa zaidi,”. Kisha akapokea pongezi nyingi kutoka kwa wenza wa wachezaji maarufu.

Miongoni mwa waliompongeza Sophia ni pamoja na mke wa nahodha wa Arsenal na timu ya taifa ya Norway, Martin Odegaard, Helene Spilling ambaye alisema wana shauku kubwa ya kumuona mtoto huyo.
Wengine waliotoa pongezi zao ni mpenzi wa mchezaji wa Arsenal, Bukayo Saka, Tolami Benson, mke wa golikipa wa Bayern Munich, Manuel Neuer, Anika, na mke wa beki wa zamani wa Chelsea, Andreas Christensen, Katrine.
Ni wazi kuwa mtoto huyo atazaliwa wakati bado Havertz anaichezea Arsenal ambayo alijiunga nayo mwaka 2023 akitokea Chelsea, na hadi sasa ameicheza mechi 58 na kupachika wavuni mabao 22 akiwa na jezi ya washika mitutu hao wa London.
Ikiwa Arsenal inayosaka taji lake la kwanza la EPL tangu 2004 itatwaa ubingwa huo msimu huu, basi hiyo itakuwa zawadi kubwa kwa mtoto wake huyo japo ni ngumu.