Hawa hapa wakali wa kutupia NBA

Muktasari:
- Msimu huu wa 2024-25 umejaa vipaji vilivyobobea katika maeneo mbalimbali ya ufyatuaji wa mikwaju, kila mmoja akiwa na mchango wa aina yake kwa timu yake.
TEXAS, MAREKANI: KATIKA mpira wa kikapu, hakuna silaha kali kama uwezo wa mchezaji kufunga kwa usahihi - iwe ni kupitia mapigo ya karibu na kikapu au kwa mitupo ya mbali ya pointi tatu.
Msimu huu wa 2024-25 umejaa vipaji vilivyobobea katika maeneo mbalimbali ya ufyatuaji wa mikwaju, kila mmoja akiwa na mchango wa aina yake kwa timu yake.
Tukiangazia vipengele vinne vya msingi vya upigaji wa mikwaju kumalizia ndani ya rangi (paint), mitupo ya mbali kupitia pasi (catch-and-shoot), mitupo ya mbali kwa kujiandalia (pull-up 3s), na mid-range (pull-up 2s) tunapambanua wachezaji waliotamba zaidi hadi kufikia mwanzoni mwa mwezi huu, Aprili, 2025.
Obi Toppin: Mfalme wa Mikwaju ya Ndani ya PainT
Katika eneo la karibu na kikapu maarufu kama paint ambapo nguvu, kasi na wakati sahihi vinahitajika, nyota wa Indiana Pacers, Obi Toppin, ameibuka kuwa bora kuliko wote.
Akiwa na urefu wa futi 6 na inchi 9, Toppin amefunga kwa asilimia 74.1 ya mashuti yake 251 aliyopiga ndani ya paint. Takwimu hizi si tu zinamweka kileleni msimu huu, bali pia zinampa hadhi ya kuwa mmoja wa wamaliziaji bora zaidi katika historia ya hivi karibuni.
Ingawa uwezo wake wa kufunga nje ya paint umeshuka, Toppin amekuwa silaha muhimu kwa Pacers, akionyesha ukuaji mkubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo alifikia asilimia 61.9.
Taurean Prince: Mwamba wa Mikwaju ya Catch-and-Shoot
Kwenye eneo la mitupo ya mbali kupitia pasi maarufu kama catch-and-shoot 3-pointers mchezaji wa Lakers, Taurean Prince, amekuwa kivutio.
Amefunga mitupo 124 kati ya 245 aliyojaribu sawa na asilimia 50.6 kiwango cha juu mno ikizingatiwa wastani wa ligi ni asilimia 37.4.
Prince anafaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na nafasi anazopata pembezoni mwa uwanja, ambapo asilimia 51 ya mashuti yake ya mbali yametokea kona za uwanja (corner threes), eneo lenye mafanikio makubwa kwa wapigaji hodari wa pointi tatu.
Zach LaVine: Moto wa Mikwaju ya Pull-up 3s
Wachezaji wanaoweza kujiandalia nafasi na kupiga mitupo ya mbali (pull-up 3-pointers) huongeza sana thamani ya mashambulizi ya timu. Na hakuna anayefanya hivyo kwa mafanikio kama Zach LaVine wa Chicago Bulls.
Kwa asilimia 42.4 ya mafanikio katika mashuti 276 ya pull-up 3s, LaVine amepaa hadi kuwa kinara wa eneo hili.
Uwezo wake wa kubadili mwelekeo na kuachia shuti kwa kasi umekuwa mwiba kwa timu pinzani, na msimu huu amevuka kiwango chake cha juu cha awali cha asilimia 39.0 alichokifikia msimu wa 2020-21.
Jaren Jackson Jr.: Mtawala wa Mid-Range (Pull-up 2s)
Ingawa mitupo ya kati ya uwanja (mid-range shots) haitiliwi mkazo na timu nyingi kwa sababu ya thamani yake ndogo kulinganisha na mitupo ya pointi tatu, bado kuna nyakati ambapo ni lazima kufunga kwa hali yoyote.
Katika mazingira haya, Jaren Jackson Jr. wa Memphis Grizzlies ameonyesha umahiri wake. Akiwa na asilimia 56.7 ya mafanikio katika mashuti 157 ya pull-up 2s, amekuwa chaguo la kuaminika kila timu inapohitaji pointi za dharura.
Jackson, anayependelea kutumia ‘floaters’ kuliko mid-range safi, ameweka rekodi ya juu ambayo ni ya nne bora katika historia ya takwimu hizi zilizochukuliwa kwa miaka 12.
SANAA YA KUFUNGA
Msimu huu wa NBA umeonesha wazi kuwa mafanikio ya timu yoyote yanatokana kwa kiasi kikubwa na uwezo wa wachezaji wake kufunga.
Kutoka kwa Obi Toppin ndani ya paint, hadi LaVine na Prince kwenye mitupo ya mbali, kila mmoja ameonyesha kuwa mpira wa kikapu ni mchanganyiko wa nguvu, ustadi, akili ya haraka na mpangilio wa kimkakati.
Katika ulimwengu huu wa ushindani mkali, wachezaji hawa wameweka alama, na wameacha mashabiki wakiwa na sababu zaidi ya kupenda mchezo huu.