Prime
HISIA ZANGU: Ateba ni sehemu ya mchakato wa mabadiliko

Muktasari:
- Waliibadili Yanga kwa kiasi fulani kulinganisha na kule walikokuwepo. Baadaye, Hersi akaifanyia mabadiliko zaidi Yanga. Akawaleta Khalid Aucho na Yannick Bangala. Yanga ikawa tamu zaidi katika eneo la kiungo. Mukoko akaanza kusugua benchi. Baadaye akaondoka zake Yanga.
LABDA nitoe mfano kwa watani zao Yanga. Wakati ule Injinia Hersi Said akianza kuibadili Yanga aliwahi kuleta wachezaji wawili wa eneo la kiungo ambao kwa kiasi kikubwa waliibadili Yanga. Mukoko Tanombe na Zawadi Mauya.
Waliibadili Yanga kwa kiasi fulani kulinganisha na kule walikokuwepo. Baadaye, Hersi akaifanyia mabadiliko zaidi Yanga. Akawaleta Khalid Aucho na Yannick Bangala. Yanga ikawa tamu zaidi katika eneo la kiungo. Mukoko akaanza kusugua benchi. Baadaye akaondoka zake Yanga.
Kuna wakati katika kuunda timu imara ni mchakato. Namuona Leonel Ateba kama mchezaji ambaye yupo katika kipindi muhimu cha mchakato wa kuifanya Simba kuwa imara zaidi. Sio kwamba yeye ataibadili Simba, hapana, kuna mtu atatafutwa ambaye yupo juu zaidi.
Ateba ameipokea Simba kutoka kwa kina Papaa Jobe. Kama utawalinganisha wote wawili basi Ateba ni mzuri kuliko Jobe. Lakini kama unataka Simba iwe bora zaidi basi unahitaji mshambuliaji bora zaidi kuliko Ateba.

Ateba ana uzito, hana shabaha nzuri langoni na juzi tu, alikosa bao jingine dhidi ya Mbeya City nalilizidi kumfanya awe kichekesho kwa mashabiki wa Simba yenyewe na watani zao. Ana bahati Kocha wa Simba, Fadlu Davids anamuona Ateba kama chaguo la kwanza la ushambuliaji katika kikosi chake.
Hatujui kilitokea nini katika pambano la marudiano dhidi ya Al Masry, kocha Fadlu aliamua kumpanga mshambuliaji mwingine, Steven Mukwala mbele ya Ateba. Tunahisi huenda watu wenye nguvu waliingilia katika katika upangaji wa kikosi.
Sasa mashabiki wamekuwa wanampenda zaidi Mukwala kuliko Ateba. Kwa mtazamo wangu hapa ni mashabiki wanamwangalia zaidi mchezaji mwenye nafuu zaidi yao, lakini si kwamba Mukwala naye ni tishio kama alivyokuwa Meddie Kagere au John Bocco.
Wote wawili wapo katika mchakato wa ujenzi wa Simba. Baada ya uwepo wa mshambuliaji kama Jobe, kisha Ateba, lazima viongozi wa Simba watataka waende juu zaidi kwa kumchukua mshambuliaji ambaye yupo juu ya Ateba. Ni mchakato ule ule wa kina Mukoko.

Tatizo ni kwamba Afrika yenyewe ina washambuliaji wachache. Sio rahisi sana kumpata mshambuliaji kama Fiston Mayele kama ambavyo watu wanafikiri. Unahitaji kutuliza kichwa na kuwa makini. Hata Ulaya siku hizi washambuliaji wamepungua kwa kiasi kikubwa. Washambuliaji wenye uhakika wa kukupa mabao 20 ya Ligi na kuendelea ni wachache.
Katika ligi yetu pia maisha yamekuwa tofauti. Anaweza kuja mshambuliaji ambaye amefunga mabao 20 katika Ligi Kuu ya Rwanda, lakini akifika Tanzania anakuwa mshambuliaji wa kawaida tu ambaye hata kufunga mabao 10 ya ligi kwa msimu hawezi.
Tumeona mifano ya kina Michael Sarpong na Willy Onana. Walionekana kuwa moto katika Ligi ya Rwanda, lakini walipofika Tanzania wakaonekana washambuliaji wa kawaida ambao wasingekuwa msaada mkubwa kwa wakubwa wa Kariakoo.

Siku hizi hata rafiki zetu Waganda wamekuwa hawatulishi wachache wakali kama ilivyokuwa zama za kina Emmanuel Okwi. Ndugu zetu Zambia nao walikuwa wanaonekana wapo juu zaidi yetu kiasi kwamba mchezaji staa kutoka Zambia angetamba moja kwa moja katika Ligi Kuu ya Tanzania. Sasa hivi wamebakia kutuletea kina Joshua Mutale.
Tukirudi kwa Ateba kuna maswali mawili ya kujiuliza. Kwa nini alicheza kipindi kifupi akiwa na USM Alger ya Algeria? Waliona nini kutoka kwake? Lakini hapo hapo tunaweza kujiuliza ni kwa nini kwa muda mrefu amecheza ligi kuu ya kwao?
Mshambuliaji yeyote hatari kutoka Cameroon, Nigeria, Ivory Coast, Mali na nchi nyingi za Afrika Magharibi inakuwa rahisi kutoka kwao na kutamba nje ya mipaka yake. Ukiona mshambuliaji anakaa zaidi kwao ujue kuna tatizo.

Pengine Simba hawakumchunguza sana Ateba kabla ya kuinasa saini yake. Huwa nina wasiwasi mshambuliaji wa Ghana mwenye umbo kubwa na zuri kisoka kama Sarpong anapocheza Ligi Kuu ya Rwanda akitokea Ghana.
Hawa jamaa wana soko zuri kuliko Mbwana Samatta anayetokea Tanzania. Ukiona bado yupo kwao basi ujue kuna tatizo mahala. Hii ni sayansi ndogo tu. Kaka zao walishatengeneza njia nyingi kwa kukuza ukubwa wa majina ya nchi walizotokea na inakuwa rahisi kwao kufikiriwa na timu yoyote ya Ulaya kuliko mchezaji kutoka Tanzania.
Nafikiri kuepuka gharama za kuvunja mikataba ni wakati sasa klabu zetu zikawa zinafanya uchunguzi wa kina kuhusu wachezaji. Klabu hazihitaji kukurupuka kwa sababu kwa sasa Tanzania imetengeneza jina zuri la soko la ndani la Afrika.

Bahati mbaya kwa viongozi wetu ni kwamba mara nyingi huwa wanaangalia wachezaji wa kuwasajili wakati dirisha la usajili limewadia. Muda sahihi wakati wa kutazama wachezaji wanaoweza kusaidia ni wakati Ligi mbalimbali zinaendelea.
Kitu cha ziada kabisa kwa sasa ni kutokurupukia baadhi ya wachezaji wanaotoka katika Ligi fulani au waliotamba katika ligi fulani. Kuna Ligi ambazo MVP wao hawezi kutamba katika soka la Tanzania na tumeanza kuzifahamu. Kuna mchezaji unaweza kumfuatilia kwa karibu na kugundua kuwa anaweza kuwa mkali huko alikokuwa lakini soka la Tanzania haliwezi.
Kwa sasa nadhani sehemu salama ambayo haituangushi mara kwa mara inaweza kuwa DR Congo. Kila ukichunguza wachezaji waliotoka Congo unagundua bado wapo juu kisoka kuliko sisi. Wanakuwawa na utimamu mzuri wa mwili na akili mara wanapokuja kucheza Tanzania. Kuna baadhi ya Ligi haziwezi kutupatia tena aina ya wachezaji wanaokuja kutamba nchini.