Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HISIA ZANGU: Baridi ya Morocco, Asante Msuva karibu Mwalimu

HISIA Pict

Muktasari:

  • Leo hali ya hewa katika Mji wa Oujda ambako pambano la Taifa Stars na Morocco linatazamiwa kuchezwa leo usiku ilikuwa nyuzi joto 11 tu. Kwa wanaolewa mambo haya ni baridi kali. Wachezaji wa Taifa Stars walikuwa na kazi ya kujikimbikiza uwanjani ili mradi wapate joto.

WAZUNGU wanapambana kuachana na baridi mwezi huu wa Machi. Wamorocco pia wanapAmbana kuachana na msimu wa baridi. Morocco na Hispania sio mbali. Kuna miji inaitwa Ceuta na Melilla imekaribiana na Hispania kwa kilomita 18 tu. Haishangazi kuona hali yao ya hewa ni moja.

Leo hali ya hewa katika Mji wa Oujda ambako pambano la Taifa Stars na Morocco linatazamiwa kuchezwa leo usiku ilikuwa nyuzi joto 11 tu. Kwa wanaolewa mambo haya ni baridi kali. Wachezaji wa Taifa Stars walikuwa na kazi ya kujikimbikiza uwanjani ili mradi wapate joto.

Wachezaji wa Stars walikuwa wanakimbilia basi kutoka katika uwanja wa mazoezi ili mradi wapate joto kidogo kutoka katika basi hilo. Basi lingefika hotelini lakini mwendo wa kutoka katika basi kuingia katika lango la hoteli wachezaji wangetimua mbio mpaka katika geti. Maisha haya yameendelea tu kunikumbusha baadhi ya vitu.

Simon Msuva amekaa hapa takribani miaka mitano. Ukiona mchezaji amedumu kukaa hapa kwa miaka mitano basi ujue ana moyo wa Simba. Ana moyo wa jiwe. Ana moyo wa chuma. Haishangazi kuona baada ya kucheza hapa amekwenda kwingine na kwingineko. Na sasa yupo Iraq. Anaonekana ni mchezaji mwenye akili za wachezaji wa Afrika Magharibi.

Kama ukimudu hali ya hewa ya hapa basi unaweza kumudu hali ya hewa ya popote pale. Nawajua wachezaji wengi wa Kitanzania ambao wasingemudu kuwa hapa kwa muda mrefu hasa kama wana ustaa mkubwa nyumbani kama ilivyo kwa Msuva. Yangekuwa maamuzi rahisi kurudi nyumbani kuendelea kucheza Yanga au kuhamia kwa watani.

JICH 01

Sifa za nyumbani ni tamu. Unakuwa staa mkubwa kuliko ukweli halisi. Lakini uzuri wa huku ni noti. Unapata noti nyingi lakini ambazo inahitaji uwe na moyo wa chuma. Hata wachezaji wa kigeni waliokuja Dar es Salaam na kusifiwa sana walishindwa maisha ya huku. Wakaungana na akili ya wachezaji wengi wazawa kugeuza katika jiji la Albert Chalamila.

Hali ya hewa ya huku imenikumbusha pia Mbwana Samatta na ile Genk yake. Nilikwenda kumtembelea kama mara mbili nikakutana na nyuzi joto 9. Katika uwanja wao wanaocheza mechi za nyumbani Cegeka Arena hali ni mbaya zaidi. Uwanja umezungukwa na miti na baridi imepitiliza. Niliwahi kuwafikiria wachezaji wa Tanzania kama wangeweza kumudu kucheza mazingira hayo.

Katika maisha hayo kipaji huwa kinawekwa kando halafu uvumilivu na hasira za maisha vinachukua mkondo wake. Kwa macho yangu, mwaka 2003 katika baridi kama hii pale Hong-Kong nimewahi kuwaona raia wa Afrika Magharibi wakilala nje kwa ajili ya kusaka maisha. Mchezaji wa Tanzania mwenye sifa nyingi uwanja wa Taifa hawezi kuvumilia hali hii.

JICH 02

Hata Afrika Magharibi kuna baadhi ya wachezaji hawawezi kuvumilia hali hii. Unakutana na mchezaji wa kigeni mwenye kipawa maridhawa akitamba katika uwanja wa taifa na kujiuliza kwa nini hakucheza Ulaya. Baadaye unapitia historia yake unaambiwa aliwahi kupita Ufaransa au Hispania. Unagundua labda na yeye uvumilivu ulimshinda.

Uzuri ni, wao hawakurudi nyumbani kwao. Wamekwenda ugenini kwingine ambako ni Dar es salaam na wanachota dola zao katika klabu za Kariakoo. Sio mbaya. Bado wapo nje ya nchi zao na wanapata pesa nyingi kuliko anbazo wangepata Abidjan. Kitu kizuri kuliko kutojaribu kabisa au kurudi nyumbani kupata dola chache.

Unapofika katika mazingira kama haya ndipo unapowaheshimu zaidi Samatta na Msuva. Unamheshimu pia Himid Mao ambaye ameendelea kumudu katika ukanda huu huu kule Misri ambako amekaa zaidi ya miaka sita kwa sasa. Nadra sana kuwa na wachezaji wa namna hii katika Jamii ya wachezaji wetu wengi ambao wamekulia katika ujamaa.

JICH 03

Afrika Magharibi ni kawaida kuwa na wachezaji wa namna hii. Inanikumbusha mwaka jana nilikwenda katika jiji la Kazan pale Urusi na hali ya hewa ilikuwa 'negative 16'. Bado watu weusi kutoka Afrika Magharibi walikuwa wanahaha kutafuta maisha mitaani. Hayo sio maisha ya Mtanzania wa kawaida ambaye ana uhakika wa kula milo mitatu kwa siku bila ya kufanya kazi. Mtanzania mjamaa.

Na sasa hapa Morocco tunaye kijana wetu, Seleiman Mwalimu. Yupo timu kubwa ya hapa, Waydad Casablanca. Sijamfahamu vema kitabia. Naambiwa yeye ndiye aliyeshinikiza vilivyo baada ya Waydad Casablanca kumtaka. Alipambana vilivyo kuhakikisha timu yake inamuuza kwenda Morocco baada ya ofa kupokelewa katika mikono ya Singida Big Stars.

Binafsi simfahamu vema lakini labda baada ya kuishi naye hapa kwa siku chache huenda nikamuelewa vemaa. Huwa tunaanza kupata picha ya kumuelewa mtu baada ya mazungumzo ya hapa na pale. Kuna mambo mawili inabidi ayapiganie. Kifupi ana kesi mbili za msingi za kuzipagania awe kama Msuva na Samatta.

JICH 05

Kwanza kabisa apiganie kuwa mchezaji wa kudumu wa Waydad Casablanca. Hawa kaka zake walimudu kesi hizi. Kuwa wachezaji wa kudumu na muhimu katika timu ambazo wanachezea. PAOK walijaribu kumpiga benchi Samatta lakini sasa hivi wameshindwa. Samatta anaonekana kushinda vita hii na amekuwa mchezaji bora wa klabu Februari.

Hili ni jambo gumu kwa Mwalimu. Hawa jamaa wana pesa nyingi na kwao kukatisha mkataba wa mchezaji ni jambo la kawaida tu. Wakati mwingine wapo tayari kukatisha mkataba wa mchezaji kisha wakakumbana na kesi ya FIFA kama ilivyotokea kwao kwa Msuva au kama Simba na Yanga wanavyofanya Tanzania.

Mwalimu inabidi apambane kweli kweli kuwa mchezaji wa kudumu wa Waydad. Hawa jamaa wana nafasi chache kwa wageni lakini pia kila siku jicho lao linaangalia kwingineko kaa mchezaji ambaye wanaamini anaweza kuwasaidia kuliko ambaye wako naye. Haya ndio yamekuwa maisha yao kila kukicha lakini pia ndio maisha ya klabu nyingi kubwa na ndogo duniani. Ndio maana kuna madirisha ya uhamisho.

JICH 04

Lakini baada ya hapo pia akomae na maisha ya nje ya uwanja. Haya maisha ya nje ya uwanja ndio ambayo yamewatenganisha wachezaji wa Afrika Magharibi na wachezaji wetu. Ndiyo ambayo yamewatenganisha kina Samatta na wachezaji wetu wengine wa ndani. Vipaji wengi wanavyo tatizo ni mapambano ya nje ya uwanja. Kujituma na kujitoa mhanga.

Kila la kheri kwake. Ni jambo jema kuwa na mchezaji wa aina yake nje ya nchi. Mchezaji ambaye ameanza kuja juu bila ya kupitia kwa wakubwa. Huenda kukosekana kwa ufalme wake katika soka la Tanzania kukamsaidia kwa kiasi kikubwa kutotamani kurudi nchini haraka. Inanikumbusha Nizar Khalfan ambaye wakati wake alicheza Ligi Kuu ya Marekani bila ya kupitia kwa timu za Kariakoo.