Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HISIA ZANGU: Kama Unguja haijaacha tabasamu, Mnyama anaweza kucheka Durban

HISIA Pict

Muktasari:

  • Kabla ya hapo, awali Simba walilazimika kusubiri dakika kadhaa bao la Ahoua kuhalalishwa na VAR na hivyo kupata bao lao pekee dhidi ya wageni wao Wasauzi katika Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar. Mpira ulipomalizika kwa ushindi

DAKIKA za jioni, Jean Charles Ahoua alimzunguka kipa wa Stellenbosch, Oscarine Masuluke na kisha kuupiga mpira nje ya nyavu. Alipaswa kuupiga mpira ndani ya nyavu. Lango lilikuwa wazi. Na kama Ahoua angeuweka mpira ndani ya nyavu Simba ingekuwa imekaribia kucheza dhidi ya RS Berkane pambano la fainali.

Kabla ya hapo, awali Simba walilazimika kusubiri dakika kadhaa bao la Ahoua kuhalalishwa na VAR na hivyo kupata bao lao pekee dhidi ya wageni wao Wasauzi katika Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar. Mpira ulipomalizika kwa ushindi mwembamba wa bao moja uwanja wa Amaan mashabiki waliondoka kimyakimya uwanjani.

Watu wawili watatu walidai kwamba lilikuwa kosa kupeleka mechi uwanja wa Amaan. Nadhani kwa sababu imani na Uwanja wa Mkapa imekuwa kubwa zaidi. Wawili wanne wakaishia kumtukana mtangazaji wa mechi za Azam TV, Gharib Mzinga kwamba ana nuksi na mechi zao. Sijui anahusikaje na matokeo ya uwanjani. Sijui yeye ndiye aliyemsajili Leonel Ateba. Sijui. Ahoua naye akatukanwa zaidi.

HIS 01

Sina cha kusema sana kuhusu Ahoua kwa sababu itakuwa marudio. Mpaka leo ameendelea kuwachanganya Simba kuhusu yeye ni mchezaji wa namna gani. Ukienda katika namba zake unaona kwamba ni mchezaji bora. Ukimtazama kama alivyo hauoni kama ni mchezaji bora. Inategemea unataka nini kutoka kwake. Unachokiona kwa macho yako au unachokiona katika namba zake.

Bao hilo alilokosa liliwafanya mashabiki wengi wakiri kwamba mechi ya pili imewekwa rehani kutokana na ushindi mwembamba wa Simba pale Amaan. Inawezekana, lakini pia sidhani kama ni kitu rahisi Simba kuondolewa katika mashindano licha ya kushinda ushindi huo.

Dakika 90 za Durban zitakuwa mechi nyingine nzuri ya soka. Ambacho itaondoka nacho Simba ni hali ya kujisikia wako nyumbani. Basi. Sioni kama kutakuwa na mabadiliko makubwa ila uhuru wa kuwa nyumbani utaondoka kisaikolojia.

HIS 02

Bahati nzuri kwa Simba wanakwenda kucheza na timu ambayo ina mashabiki katika jukwaa moja tu. Stellenbosch sio Kaizer Chiefs wala Orlando Pirates. Ni timu tu ya miaka ya karibuni ambayo haina mashabiki wake wafia timu.

Inanikumbusha mechi ya Yanga dhidi ya Marumo Gallants iliyopigwa Uwanja wa Royal Mafokeng pale Rustenburg. Yanga walikuwa kama wapo nyumbani namna Watanzania walivyoujaza uwanja dhidi ya timu ambayo haina mashabiki wengi wa asili pale Afrika Kusini. Wakashinda 2-0.

Katika Uwanja wa Mosses Mabhida pale Durban Simba wanaweza kujaza nusu ya uwanja huo mzuri, kisha rafiki zetu Stellenbosch wakajaza nusu ya jukwaa moja. Utapigwa mpira mwingi pengine kuliko ilivyokuwa Uwanja wa Amaan.

Mpira wa siku hizi wa Afrika na dunia kwa ujumla haueleweki vyema. Hii ni mechi ambayo haitaamuliwa na mashabiki kama ambavyo mechi ya Unguja haikuamuliwa na mashabiki. Huenda Simba akashinda tena Durban. Huenda pia akafungwa.

HIS 03

Wiki moja iliyopita tuliambiwa habari za Remontada pale Santiago Bernabeu. Wakafunika na paa lao lakini Arsenal alikwenda tena hapo kimyakimya na akatupia mabao mawili huku Bukayo Saka akikosa penalti. Huenda zile tatu za mwanzo za Emirates zingejirudia.

Stellenbosch wameshatuonyesha ambavyo hawatabiriki katika michuano hii. Walitoka suluhu kwao wakaenda kushinda Misri. Simba walifungwa 2-0 pale Cairo wakaja kuzikomboa pale Temeke. Yanga alifungwa na USM Alger pale Temeke, akaenda kushinda Algers.

Kama Ahoua angefunga huenda angepeleka asilimia nyingi kwa Simba katika pambano la marudiano, lakini sasa ni muda wa kutazama mbele na kuchora ramani. Stellenbosch wataingia uwanjani na kufanya kile ambacho Simba walifanya Unguja.

HIS 04

Watacheza kwa kasi. Kisaokolojia pia watajiona wapo nyumbani japo ukweli Durban sio kwao. Kama wakifanikiwa kurudisha bao moja mapema, basi maisha yatakuwa magumu kidogo kwa Simba. Lakini kitu kinachofurahisha kwa timu zetu kubwa, Simba na Yanga ni kwamba na wao wanaweza kufunga popote katika mpira huu wa Afrika.

Zamani tulikuwa hatuwezi, lakini siku hizi tunaweza. Simba wanaweza kufunga bao Durban na wakamaliza mechi kiulaini tu. Inategemea ni namna gani wataanza kugundua makosa yao. Niliwahi kuandika hapa kwamba mbele Simba hawachezi mpira mwepesi.

Wanacheza mpira mwepesi kuanzia nyuma mpaka katikati. Mpira ukifika mbele wanacheza mpira mgumu kwa sababu kila mmoja anajiona kuwa ana haki ya kuwa mfalme katika eneo la mbele. Kama wakiurahisisha kwa kutazamana kwa haraka haraka Simba wana uwezo wa kufunga.

HIS 05

Simba pia wanaweza kupitishwa na sare ya namna yoyote pale Durban. Tatizo kubwa ni tamaa ya mashabiki kutaka kuhakikishiwa kupita kwa idadi kubwa ya mabao ya mechi ya nyumbani. Wakati mwingine mpira hauwi hivyo. Simba wanaweza kufunga zaidi Durban kuliko walivyofunga Unguja.

Lakini kwanza wawe wavumilivu kwa kasi ya Stellenbosch katika kipindi cha kwanza. Hawa jamaa inawezekana wameonekana wa kawaida pale Unguja, lakini katika ardhi ya Mandela wamekuwa wakifanya vyema katika mechi ngumu kama zile dhidi ya Kaizer Chiefs, Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates. Huenda wakawaandalia Simba zawadi ileile ambayo huwa wanaziandalia timu kubwa Afrika Kusini.

Vinginevyo fainali bado ipo katika mikono ya Simba. Litakuwa jambo bora kwamba ndani ya misimu mitatu Tanzania itakuwa imefanikiwa kufika fainali za Shirikisho mara mbili. Wakati mwingine itakuwa ishara kwamba kwa sasa sisi anga zetu ni Ligi ya Mabingwa Afrika zaidi kuliko Shirikisho.

Kwa Simba itakuwa bonasi zaidi kwa sababu watakuwa wamefika fainali huku wakiwa katika ujenzi wa timu. Kuna kundi la wachezaji wanacheza katika kikosi cha kwanza, lakini unaona kabisa hawana hadhi ya kucheza Simba. Muda si mrefu wataondoka na watakuja wengine wenye uwezo zaidi.