Prime
JICHO LA MWEWE: Mayele ni Shabani Nonda aliyechelewa safarini

Muktasari:
- Kuna wale kama kina Jammie Vardy wa Leicester City ambao walichelewa kuchomoza katika soka. Yaani uhatari wao umekuja baadaye zaidi. Kadri anavyocheza ndivyo anavyozidi kuchomoza. Vardy alianza kutamba Ligi Kuu akiwa na miaka 26.
FISTON Kalala Mayele ni mtu hatari, lakini maisha yake ya soka yananichanganya kidogo. Huwa najiuliza kama alikuwa hatari kama alivyo akiwa DR Congo. Kuna wachezaji huwa wanachelewa kidogo kuanza kuwika.
Kuna wale kama kina Jammie Vardy wa Leicester City ambao walichelewa kuchomoza katika soka. Yaani uhatari wao umekuja baadaye zaidi. Kadri anavyocheza ndivyo anavyozidi kuchomoza. Vardy alianza kutamba Ligi Kuu akiwa na miaka 26.
Hata hivyo, kwa uhatari ambao nauona kwa Mayele kama mshambuliaji, nadhani alipaswa kuondoka DR Congo akiwa na umri wa miaka 20 na kwenda kuiteka dunia nyingine ya soka. Angeweza kwenda kwa wakoloni wao Ubelgiji na kuwateka kama Mbwana Samatta alivyofanya.
Yanga walimchukua kutoka DR Congo akiwa mfungaji bora namba mbili wa Ligi ya DR Congo. Alipokuja nchini wote tulishuhudia namna alivyokuwa mfungaji hatari. Hata hivyo, alikuwa nchini akiwa na miaka kama 27 hivi. Muda wote huo alikuwa anafanya nini DR Congo?

Sasa ana umri wa miaka 30 anatamba katika kikosi cha Pyramids cha Misri. Anafunga mabao kadri anavyojisikia katika Ligi Kuu ya Misri, pia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa. Hata hivyo, naamini Mayele anaweza kuwa Nonda Shabani aliyechelewa.
Wakati mwingine wachezaji wanakuwa na bahati tofauti. Nonda Shabani 'Papii' alikuja hapa mwaka 1994 kucheza Yanga na hakuwa mshambuliaji tishio kama Mayele alivyokuwa katika wakati wake hapa nchini. Nonda alikuwa anasugulishwa benchi na Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ pamoja na James Tungaraza ‘Boli Zozo’.
Kama alidanganya umri au vinginevyo, lakini Nonda alikuja nchini na pasipoti nzuri. Ilionekana aliondoka nchini kwenda Vaal Professional ya Afrika Kusini akiwa na miaka 18 tu. Ilikuwa ni bahati yake alitamba katika mechi moja tu dhidi ya Vaal Professional katika michuano ya CAF na hao wakubwa wakamuona wakamchukua.

Baada ya kutamba msimu mmoja pale Afrika Kusini alitimkia Ulaya kucheza FC Zurich ambako alionyesha makali kabla ya kutimkia kwingineko. Kuanzia hapo Nonda alitamba Ufaransa, Italia, England na Uturuki.
Mayele alikuwa wapi katika umri wa miaka 19? Ni swali ambalo najiuliza. Safari ya Mayele ilipaswa kuishia Ulaya. Kwa aina yake ya ushambuliaji sidhani kama ameanza kuwa hatari ukubwani. Kuna namna alikwamisha maisha yake ya mpira DR Congo kwa muda mrefu.
Kama angekuja Yanga akiwa na miaka 20 kisha akaenda Pyramids akiwa na miaka 22 nadhani safari ya Mayele ilipaswa kuishia Ulaya hasa katika nyakati hizi ambazo dunia ina ukame wa washambuliaji kama yeye. Hata hivyo, kwa sasa Mayele ana miaka 30 na sioni kama anaweza kununuliwa na timu za Ulaya.

Mara nyingi timu za Ulaya huwa zinatazama mambo mengi kabla ya kumnunua mchezaji. Zinamtazama mchezaji kama anaweza kuuzika tena. Lakini wanaangalia muda ambao mchezaji anaweza kuzoea soka la kwao. Kwa Mayele inaonekana kama vile safari imechelewa. Jua limeanza kuzama na hayo yote mawili hauwezi kuyapata katika umri wa miaka 30. Alikuwa wapi?
Wakati Nonda akiingia Ulaya na miaka 19, Mbwana Samatta aliingia Ubelgiji akiwa na miaka 23. Yeye mwenyewe anakiri alichelewa kucheza soka la Ulaya kwa kuingia na umri huo. Vipi kwa Mayele mwenye umri wa miaka 30? Sidhani kama safari itakuwepo tena. Ni wazi atakuwa amechelewa.
Vyovyote ilivyo, Ulaya haikubarikiwa kumuona mshambuliaji huyu hatari na ni kitu ambacho unaweza kusema ni bahati mbaya tu. Mayele ni hatari na ana uwezo wa kucheza mifumo mingi ya makocha wengi wa kileo.

Anaweza kukaa na mpira mguuni, anaweza kufungua nafasi kwa haraka na ana jicho la kutupia. Ni mtu hatari ambaye unawatazama washambuliaji wengi wa Ulaya kuwa hawana uwezo kama wake ila waliwahi kwenda huko.
Mmoja wa wachezaji wenye bahati ni pamoja na Cedric Bukambu ambaye anamuweka Mayele katika kikosi cha timu ya taifa. unapowatazama wote wawili unagundua kuwa Mayele ni hatari kuliko Bukambu lakini Bukambu ana wasifu mkubwa ambao unasababisha ampige benchi Mayele.
Hata hivyo, tukiachana na masuala ya Ulaya bado naona Mayele anaweza akaanzisha vita zaidi katika soko la ndani ya Afrika. Kwa mtazamo wangu yeye ndiye mshambuliaji bora wa ndani barani Afrika kwa sasa.

Nadhani Pyramids wanaweza kujikuta katika vita na ndugu zao wengine kama Zamalek na Al Ahly au Waarabu wengine wenye hela kutoka Tunisia na Morocco. Kuwa wakati hawa wakubwa huwa wanatunishiana misuli na kutoa kiasi cha dola milioni 3 kwa ajili ya kumtaka Mayele kinaweza kuwa kitu cha kawaida tu. Bahati nzuri kwa Pyramids ni kwamba na wao wana hela.
Kitu cha msingi zaidi ni tofauti na wachezaji wetu wengi nchini, Mayele bado hayupo kwao. Walau alitoka zake DR Congo akaja zake Tanzania na sasa yupo Misri. Lazima anakunja kitita kizuri cha pesa kwa sasa akiwa na Pyramids. Kama atasaini mkataba mpya mwishoni mwa msimu huu kama alisaini mkataba wa miaka miwili hapo awali basi bado atakunja kitita kirefu. Soko lake limekwenda juu zaidi.
Anaweza akajuta kwa kutocheza Ulaya lakini ni wazi soko la Misri limempatia pesa maradufu na mwisho wa safari yake hawezi kujuta kuamua kuwa mwanasoka. Waarabu wanalipa vizuri.