Watkins, Marcus Rashford kupishana Man United

Muktasari:
- Ripoti zinaeleza, Man United haina mpango wa kumuuza Rashford ingawa inaweza kufikiria kumwacha aende Villa anayoichezea kwa mkopo ikiwa timu hiyo itakubali kuwapa Watkins.
MANCHESTER United inaangalia uwezekano wa kufanya mabadilishano na Aston Villa na inataka kumtumia Marcus Rashford ili wampate Ollie Watkins.
Ripoti zinaeleza, Man United haina mpango wa kumuuza Rashford ingawa inaweza kufikiria kumwacha aende Villa anayoichezea kwa mkopo ikiwa timu hiyo itakubali kuwapa Watkins.
Watkins ni mmoja ya mastaa waliolivutia sana benchi la ufundi la Man United kiasi cha kuwa tayari kufanya mabadilishano na tangu kuanza msimu huu amecheza mechi 46 za michuano yote, akafunga mabao 16 na kutoa asisti 13.
Tangu ajiunge na Villa kwa mkopo dirisha la majira ya baridi mwaka huu, Rashford ameonyesha kiwango cha kuvutia ambacho kimesababisha Villa kuhitaji kumpa mkataba wa kudumu.
Mkataba wa Watkins unamalizika mwaka 2028, wakati ule wa Rashford ukimalizika mwaka 2028.
Antoine Griezmann
MSHAMBULIAJI wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann, 34, yuko katika hatua za mwisho kusaini mkataba mpya utakaomwezesha kuitumikia timu hiyo hadi Juni 2027.
Awali staa huyu wa kimataifa wa Ufaransa alikuwa akihusishwa kuondoka kujiunga na moja ya timu katika Ligi Kuu ya Marekani. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026 na amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Kocha Diego Simeoni na timu ya taifa ya Ufaransa.
Andre Onana
VIGOGO wa Manchester United wapo tayari kumwachia kipa wao raia wa Cameroon, Andre Onana, 29, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiwa timu hiyo itapokea kiasi kisichopungua Pauni 20 milioni dirisha lijalo.
Onana ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, anahusishwa kuondoka kutokana na kiwango alichoonyesha hivi karibuni ambacho kimesababisha lango la mashetani hao wekundu kuruhusu mabao mengi.
Lorenzo Lucca
MANCHESTER United inaendelea kufanya mazungumzo na mshambuliaji wa Udinese, Lorenzo Lucca, 24, ambaye inataka kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Fundi huyo wa kimataifa wa Italia, amelivutia benchi la ufundi la Man United kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu na Kocha Rubben Amorim anataka kutengeneza kikosi cha ushindani msimu ujao na Lucca anahusishwa nao.
Ryan Gravenberch
Kiungo wa kati wa Liverpool, Ryan Gravenberch hana mpango wa kuondoka katika viunga vya Anfield hivi karibuni licha ya wakala wa mchezaji huyo kutoka Uholanzi, hivi karibuni kuweka wazi ana ndoto ya kuichezea Real Madrid.
Ryan aliyesajiliwa na Liverpool katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2023, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na amekuwa hapati nafasi ya kutosha ya kucheza.
Alex Remiro
MKURUGENZI wa michezo wa Barcelona, Deco, ameanza mazungumzo na wawakilishi wa Real Sociedad ili kuipata saini ya kipa wao, Alex Remiro, mwenye umri wa miaka 30, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Barca inamwangalia kipa huyu kama mbadala wa kipa wao raia wa Ujerumani Marc-Andre ter Stegen, 32, ambaye amekuwa akisumbuliwa sana na majeraha ya mara kwa mara.
Dejan Kulusevski
TOTTENHAM imeanza mazungumzo na wakala wa kiungo wao raia wa Sweden, Dejan Kulusevski, 24, ili kumsainisha mkataba mpya na kumzuia asiondoke dirisha lijalo na vigogo kibao wameonyesha nia ya kumsajili zikiwamo AC Milan na Napoli.
Kocha wa Spurs, Ange Postecoglu bado ana mipango na Dejan na hataki kuona akiondoka.
Mark Flekken
BAYER Leverkusen inamevutiwa na kiwango cha kipa wa Brentford, Mark Flekken, mwenye umri wa miaka 31, na wanataka kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Ripoti kutoka Sky Sports zinaeleza, Brentford inahitaji kiasi kisichopungua Euro 15 milioni ili kumuuza staa huyu wa kimataifa wa Uholanzi ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.