Guardiola alilia michuano ya UEFA

Muktasari:
- Guardiola ambaye amekisifu kikosi chake baada ya ushindi dhidi ya Everton wikiendi iliyopita, amesisitiza hana mashaka juu ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema mafanikio makubwa kwa kikosi chake kwa msimu huu ni kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Guardiola ambaye amekisifu kikosi chake baada ya ushindi dhidi ya Everton wikiendi iliyopita, amesisitiza hana mashaka juu ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
"Tabia ya kweli inaonekana unaposhinda, ukishindwa, watu husema hujui. Kile ambacho wachezaji hawa wamefanya kwa kipindi cha muongo mmoja, ninashukuru sana."
"Tulikuwa na kipindi kigumu zaidi msimu huu kwa sababu nyingi, hasa majeraha lakini tumekuwa imara kwa kiasi kikubwa na kuendelea mbele. Bila shaka, tuko mbali sana na Liverpool na Arsenal, lakini usiku wa leo (juzi) tumelala tukiwa nafasi ya nne."
"Tunahitaji kushinda Jumanne dhidi ya Aston Villa. Tuna mechi tatu nyumbani, mbili ugenini na tunatumai tunaweza kufanikisha hilo."
Guardiola pia alizungumzia kiwango cha kiungo wake, Nico O'Reilly ambaye katika mechi za hivi karibuni anamchezesha kama beki wa kushoto.
"Yeye ni kiungo mshambuliaji. Unapomtumia kama beki wa pembeni, huwa anakuwa na spidi kwenye suala la kushambulia na huwa anajitokeza mahali panapohitajika. Tazama alivyocheza dhidi ya Plymouth na pasi mbili za mabao dhidi ya Bournemouth."
"Katika timu hii inaonekana ukicheza kama beki wa kushoto, lazima ufunge. Josko (Gvardiol) alifanya hivyo hapo nyuma na sasa ni yeye. Kwa mchango wake, tunashukuru sana kwa sababu si beki wa kushoto halisi."