Gyokeres akataa kutabiri atakapocheza 2025/26

Muktasari:
- Gyokeres ambaye ameendelea kuonyesha kiwango bora baada ya kufunga hat-trick katika mchezo Ligi Kuu Ureno dhidi ya Moreirense na Sporting iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, hadi sasa amefunga mabao 47 katika michuano yote.
LISBON, URENO: STRAIKA wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres amekataa kutabiri juu ya wapi anaweza kutua dirisha lijalo la majira ya kiangazi akisisitiza 'hakuna anayeweza kutabiri kitakachotokea.'
Gyokeres ambaye ameendelea kuonyesha kiwango bora baada ya kufunga hat-trick katika mchezo Ligi Kuu Ureno dhidi ya Moreirense na Sporting iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, hadi sasa amefunga mabao 47 katika michuano yote.
Vilevile, hiyo ilikuwa ni hat-trick yake ya tano kufunga msimu huu mojawapo ni ile dhidi ya Manchester City katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mshambuliaji huyu aliyejiunga na Sporting akitokea Coventry City wakati Ruben Amorim akiwa kocha, sasa anahusishwa na kujiunga na klabu kubwa za Ulaya dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 ameendelea kuwa kimya kuhusu mustakabali wake na kusisitiza hawezi kutabiri kinachoweza kutokea kutokana na wingi wa timu zinazomhitaji.
"Hakuna anayeweza kutabiri kitakachotokea, tunafurahia wakati huu ambao tunao kwa sasa.”
Miongoni mwa timu ambazo anahusishwa nazo sana ni pamoja na Manchester United ambaye tetesi za kujiunga nao zimezidi baada ya Amorim kujiunga na timu hiyo, hivyo ushawishi wake kwa staa huyu unatajwa kama sababu moja wapo ya kufanikisha dili hilo hususani katika wakati huu na wana uhitaji mkubwa wa mshambuliaji mpya kutokana madhaifu ambayo yapo kwenye eneo lao la ushambuliaji.
Arsenal ni timu nyingine inayohusishwa na staa huyu ili kuondoa madhaifu ambayo yamekuwepo kwenye kikosi chao msimu huu yaliyochangiwa na kukosa kusajili mshambuliaji wa kati mwaka jana.
Dirisha lililopita la majira ya baridi, The Sun iliripoti kuwa klabu hiyo iko tayari kumuuza iwapo watapokea ada kati ya kati ya Pauni 55 hadi 70 milioni ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wake lakini staa huyu alipoulizwa kuhusu makubaliano hayo lakini alijibu:
"Siwezi kusema lolote kuhusu hilo."