Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Buriani Uncle Lundenga, tangulia kamanda!

LUNDENGA Pict

Muktasari:

  • Mratibu huyo wa zamani wa shindano la urembo la Miss Tanzania, aliyekumbwa na mauti baada ya kuugua kwa muda mrefu atakumbukwa kwa mengi katika tasnia ya urembo, muziki pamoja na michezo.

UNCLE ameondoka. Uncle anazikwa kesho Jumatatu. Ndio Hashim Lundenga amefariki dunia jana Jumamosi na kesho anatarajiwa kuzikwa kwenye makaburi ya Kidatu, wilayani Kilombero mkoani Morogoro.

Mratibu huyo wa zamani wa shindano la urembo la Miss Tanzania, aliyekumbwa na mauti baada ya kuugua kwa muda mrefu atakumbukwa kwa mengi katika tasnia ya urembo, muziki pamoja na michezo.

Ukiacha kuwa muasisi wa Chama cha Disko Tanzania (TDMA) na mmoja wa vigogo wa Yanga na timu ya Kimara Stop Over, Uncle Lundenga anakumbukwa kupitia Shindano la Miss Tanzania aliloliasisi mwaka 1994 kabla ya mwaka 2018 kuwekwa mikononi mwa mshindi wa taji hilo wa mwaka 1998, Basila Mwanukuzi.

Kama mmoja ya waandishi waandamizi wa habari za michezo na burudani, kifo cha Lundenga kimenishtua, hata kama nilikuwa nafahamu juu ya kuugua kwake.

Nakumbuka nilifanya mahojiano kwa mara ya kwanza na Uncle Lundenga mwaka 1995 wakati wa msigano wa mashindano yake.

LUNDE 04

Wakati huo Emily Adolf alitwaa taji la Miss Tanzania 1995, lakini akaishia kufukuzwa shule. Hatua ile ilimchanganya sana Lundenga.

Emily alikuwa mwanafunzi wa Sekondari ya Central Dodoma. Alitumia nafasi ya likizo kushiriki kwani wakati huo wanafunzi wengi walikuwa likizo ya nusu mwaka.

Emily alizua balaa hilo kutokana na serikali kukataza wanafunzi kushiriki mashindano ya urembo, lakini Emily alijipenyeza hata kutwaa taji la Miss Tanzania japo alikuja kugundulika.

Kulikuwa na mvutano mkali kwamba Emily aende tu, lakini eneo jingine lilitaka aachwe amalize masomo yake. Hata hivyo, Emily alimaliza kidato cha nne, ila katika shule nyingine.

Lundenga alinieleza mengi ikiwemo mwanzo wa mashindano yenyewe na changamoto zake.

Aliniambia kuwa mwaka 1967 mashindano ya urembo yalifanyika na mshindi alikuwa ni Theresa Shayo, lakini mwaka 1968, Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu Youth League) iliyapiga marufuku ikiwemo maonyesho ya mavazi, klabu za usiku zilifungwa na TYL ilisema inataka Watanzania kuishi kwa utamaduni wao, hayo ni utamaduni wa Magharibi.

LUNDE 03

Hata hivyo, ilipofika mwaka 1994 mashindano hayo yalifufuliwa na Lundenga baada ya kuwepo kwa uchumi huru.

Rais Ali Hassan Mwinyi alitangaza uchumi huria kwamba kila mwenye uwezo wa kuingiza bidhaa, huduma kutoka nje, kuwekeza ilikuwa ruksa.

Hapo ndipo ilipoanza Miss Tanzania na mshindi wa mwaka huo 1994 alikuwa Aina Maeda.


CHANGAMOTO

Lundenda anasema kuwa kufanya shindano la Miss Tanzania kuna changamoto nyingi, kwamba kwanza inaanza kwa wazazi, lakini pia wadhamini.

Wazazi wengi hawakuyaelewa mashindano yenyewe na kukataza watoto wao kushiriki  ikijumlishwa na agizo la serikali kupiga marufuku wanafunzi kushiriki.

LUNDE 02

Mara kadhaa katika mahojiano mengine anasema ili kuwafanya wazazi waelewe, walianza kuweka zawadi kubwa ikiwemo mshindi kupata gari na kuwaeleza kuwa anakuwa mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya dunia, Miss World Beauty Pageant.

Changamoto nyingine ilikuwa wadhamini. Alinieleza kuwa kuwaweka kambini wasichana 25 mwezi mmoja siyo masihara kwani inahitajika fedha za kutosha.

Itakumbukwa mwaka 1994 alipata udhamini wa sabuni ya Palmolive na shindano lenyewe kuitwa hivyo, Palmolive Miss Tanzania 1994, lakini waliishi katika ugumu kutokana na wadhamini na wenyewe kutolielewa shindano lenyewe.

Mwaka 1996 Kampuni ya Sigara kupitia Aspen ilidhamini kwa kushirikiana na White Sands Hotel ambako ndiko warembo walikuwa wakiishi.

Hata hivyo, shindano hilo lilieleweka na kupata umaarufu hata wadhamini kugombania udhamini kila mwaka. Ilifika hatua shindano lilinunuliwa zimazima na wadhamini.


RAFIKI WA WANAHABARI

Mafanikio ya warembo mbalimbali yametokana na kazi ya wanahabari kuripoti na kuandaa mashindano.

Lundenga na Kamati ya Miss Tanzania, aliyavunja mashindano vipande na kuanzia ngazi ya vitongoji kwani alisema ndiko kwenye warembo.

Aliwapa ujasiri waandishi wa habari kuandaa huku akiwasapoti kwa kutembelea kila hatua ya maandalizi.

Mfano mzuri ni Jokate Mwegelo aliyetokea Kitongoji cha Kurasini 2006, ametokana na waandishi wa habari, Benny Kisaka, Mobhare Matinyi (sasa Balozi) na Juma Pinto.

Hawa walikuwa na kampuni yao BMP Promotion na ndio waliomtoa Jokate kutoka Miss Changombe.

Wanahabari wengine waliokuwa mawakala ni Robert Komba na Joseph Kapinga waliokuwa wakiandaa Miss Songea.

Mimi (Ibrahim) nilikuwa mnufaika pamoja na Tom Chilala na Victor Robert Willy  (Miss Magomeni), Khadija Khalili (Miss Higher Learning), Vicky Kimaro na Zena Chande waliandaa Miss Ukonga.

Aidha Jackson Kalikumtima aliyekuwa Habari Corporation kitengo cha matangazo aliandaa Miss Ilala na ndiye aliyemuibua Hoyce Temu Miss Tanzania 1999.

Pia Asma Makau aliyekuwa Mtangazaji Redio Uhuru alikuwa mwandaaji wa Miss Tanga na kumuibua Moona Khoja na Mussa Juma aliandaa Miss Arusha. Hapo sijamtaja Somoe Ng’itu na Miss Chang’ombe wala Majuto Omary aliyekuwa muandaji wa Miss Sinza.

Lundenga alikuwa rafiki mkubwa wa waandishi wa habari, aliishi nao kama chanzo cha habari, kama kaka lakini mara nyingi alikuwa mshauri hasa masuala ya kijamii.

Aidha, Lundenga aliyekuwa shabiki wa Yanga kindakindaki hakuwa akipenda kuona mwandishi wa habari anabaki na uandishi pekee, alipenda kuona wanakuwa na chaneli mbalimbali za mapato.

LUNDE 01

MISS WORLD

Miaka yote, hamu kubwa ya Lundenga ilikuwa kuona Miss Tanzania anatwaa taji la Miss World hatua ambayo hawakuwahi kuifanya hadi ameondoka duniani.


Aliumizwa sana baada ya mrembo wake kushindwa ama kutolewa raundi za awali.

Kutokana na hali hiyo, alilazimika kwenda kwenye mojawapo ya shindano la dunia, kwani alikuwa haamini kushindwa kwa kuwa mrembo wake ni mzuri na ameandaliwa ikiwemo kuwa na kipaji.

Yapo mengi. Lundenga ameondoka na alama yake. Huwezi kuizungumzia Miss Tanzania bila kumtaja Lundenga, Bosco Majaliwa na Albert Makoye ambaye naye ni marehemu.

Lundenga ambaye amekabidhi kijiti kwa Basila Mwanukuzi (Miss Tanzania 1998) kama mwandaazi wa shindano, amefariki dunia Jumamosi ya Aprili 19, 2025 akihitimisha maisha yake ya duniani.

Kwa mujibu wa Majaliwa, Lundenga amefariki kutokana na tatizo la kiharusi (stroke) ambayo ameishi nayo kwa miaka minne.

Lundenga anatarajiwa kupumzishwa katika nyumba yake ya milele kesho Jumatatu makaburi ya Kidatu, Kilombero mkoani Morogoro, lakini ataendelea kukumbukwa kwa kila alilolifanya katika nyanja za michezo na burudani. Tangulia Uncle Lundenga, tangulia kamanda, kwani sisi tupo nyuma yako, kwa vile ni hakika kila nafsi itaonja mauti.