Prime
HISIA ZANGU: Uwanja wa Singida ni mwanzo wa matumizi ya akili ya kawaida?

Muktasari:
- Zamani niliwaza kwanini wakubwa wetu washindwe kujenga viwanja na kushirikiana na baadhi ya kampuni kama wabia. Inakuwa rahisi kwa wenzetu. Ama klabu inajenga uwanja kwa ushirikiano na kampuni moja kubwa na kisha uwanja unapewa jina la kampuni hiyo kwa mkataba wa miaka kadhaa.
NILIANDIKA hili miaka mingi iliyopita. Nilipoona kimya kinazidi kutanda nikadhani labda wazo langu lilikuwa la kipumbavu. Kwamba labda utekelezaji wake kwa hapa nchini ni jambo lisolowezekana.
Wiki ijayo Singida Black Stars watafungua uwanja mpya wenye uwezo wa kuchukua watu 30,000 waliokaa.
Zamani niliwaza kwanini wakubwa wetu washindwe kujenga viwanja na kushirikiana na baadhi ya kampuni kama wabia. Inakuwa rahisi kwa wenzetu. Ama klabu inajenga uwanja kwa ushirikiano na kampuni moja kubwa na kisha uwanja unapewa jina la kampuni hiyo kwa mkataba wa miaka kadhaa.
Au klabu inaweza kujitutumua kadri inavyoweza na kujenga uwanja wake kisha isiupe jina lolote na badala yake kuingia mkataba na kampuni fulani kuipa hadhi ya kuitwa jina la kampuni kwa mkataba mnono wa miaka kadhaa.

Simba na Yanga wangeweza kufanya hivi kabla ya Singida. Wana mamilioni ya mashabiki duniani kote na kampuni yoyote ambayo jina lake lingetumika kama jina la uwanja nadhani moja kwa moja lingepata nafasi nzuri ya kujitangaza ndani na nje ya uwanja.
Ni kama ambavyo Singida watafanya kupitia uwanja huu. Hauwezi kukwepa kuwataja au kuwasikia wawekezaji au wabia wao katika soka kwa sababu Singida, bado wapo wapo sana katika Ligi Kuu. Kila mmoja ametumia fursa ya mwenzake.
Sijui kama wabia hao wamehusika na ujenzi wa uwanja huu, au labda Singida walijitutumua wenyewe kisha wakaingia nao mkataba badae, vyovyote ilivyo ni lazima litakuwa dili zuri kwa pande zote mbili. Sifahamu ni mkataba wa miaka mingapi au mkataba wa maisha lakini vyovyote ilivyo ni lazima itakuwa dili zuri kwa pande zote mbili.

Muda mrefu sasa wazungu wamebadili akili kuhusu hili. Arsenal walipohama Uwanja wa Highbury wakajenga uwanja wao mpya unaochukua idadi ya mashabiki 60,000. Sisi mashabiki wa Arsenal tulikuwa tunasubiri kwa hamu jina la uwanja mpya. Baadaye tukaambiwa uwanja utaitwa Emirates.
Kwa mujibu wa habari za mwaka 2022, Emirates waliongeza mkataba wa miaka mitano kwa ajili ya jina lao kutumika katika uwanja na Arsenal wanapokea kiasi cha dola 63 milioni kwa mwaka kwa ajili ya uwanja huo kuitwa Emirates.
Pale Manchester City pia uwanja ukaitwa Etihad. Zamani uwanja wao uliitwa Maine Road, lakini Waarabu wametumbukiza noti nyingi kuhakikisha uwanja unaitwa Etihad na pia kifuani linakaa jina la kampuni hii ya ndege.
Rafiki zetu Barcelona pia uzalendo umewashinda. Kuanzia mwaka 2022 walibadilisha jina la uwanja wao na kuuita Spotify Camp Nou kwa mkataba wa Dola 310 milioni. Kwa ukata ambao unawakabili wasingeweza kuendekeza jina la Nou Camp peke yake wakati wanakufa njaa.

Marekani katika Jiji la Atlanta uwanja mkubwa wa mpira unaitwa Mercedes Benz Stadium sawa na ule wa Ujerumani unaotumiwa na klabu ya Stuttgart ambao pia unaitwa Mercedes Benz. Haya ndio maisha halisi ya wenzetu.
Katika mpira siku hizi kila kitu ni biashara. Kuna wazungu ambao hawapendezwi sana na mambo haya na wangependa sana majina ya kitamaduni yaendelezwe katika masuala ya viwanja kuliko majina ya kampuni, lakini ukweli ni kwamba kuna gharama kubwa kuendesha mpira na wamiliki wa klabu hizi wanataka fedha.
Manchester United wanataka kujenga uwanja mpya utakaochukua watu laki moja, lakini nahisi wanaweza kuondoka katika jina la Old Trafford na wakaingia ubia na kampuni fulani kwa ajili ya haki ya jina. Watapa mabilioni ya fedha.
Liverpool wangependa kuendelea na jina la Anfield kwa sababu linabeba kumbukumbu nyingi, lakini na wao wanaweza kuuza hiyo kama pesa itaongea. Ni maisha ya kawaida katika mpira kwa sasa na niliamini kwamba Simba na Yanga wangefanya hivyo mapema.

Wengine wanauza hadi haki ya viwanja vya mazoezi. Sijui mkataba uliopo kati ya Mohamed Dewji na Simba hadi kufikia hatua ya kuuita uwanja huo jina la Mo Arena, lakini ukweli ni kwamba kunapaswa kuwa na mkataba mzuri na biashara nzuri baina yao.
Angalia namna Yanga walivyoweza kulitangaza jina la Avic Town, ingawa wao ndio wanalipa kupata huduma za hapo. Kwanini wasingeingia mkataba na kampuni fulani kwa ajili ya kutengeneza viwanja vizuri vya mazoezi na kuvipa jina la biashara?
Nawatakia kila la kheri Singida na wabia wao. Labda huu ni mwanzo mzuri wa kufungua macho kwa baadhi ya viongozi wa klabu zetu ambao akili zao zimekuwa zikilala kwa muda mrefu. Katika dunia hii ya biashara kila kitu ni fursa kwa klabu zetu.
Itafute jezi ya Al Ahly uitazame vema. Ina matangazo zaidi ya matatu ya biashara. Hata klabu zetu hazipaswi kujibanza kwa mdhamini mmoja tu ambaye atakaa katika jezi. Kuna mdhamini wa kifuani, mdhamini wa begani, na mdhamini wa nyuma ya jezi. Jina la mchezaji likanaa juu halafu jina la kampuni linakaa chini.
Kila kitu ni fursa kwa timu zetu. Nashukuru wameona pia fursa katika suala la usafiri hususani wa anga ambapo mashirika ya ndege yamekuwa yakiingia mkataba na Simba na Yanga kitu ambacho kinawasaidia kwa kiasi kikubwa katika harakati zao za usafiri wa ndani.
Rafiki yangu Injinia Hersi Said amesema atawajengea Yanga uwanja. Nategemea unaweza kuitwa jina la mdhamini wa Yanga wa sasa kwa mkataba maalumu wa wazi wa pesa nyingi ambao utaeleweka kwa mashabiki na wanachama wa Yanga. Sio lazima uwanja uendelee kuitwa Kaunda.