Prime
JICHO LA MWEWE: Jean Charles Ahoua, Simba kupanga ni kuchagua

Muktasari:
- Unapohitaji mchezaji kama Ahoua, licha ya kuwa alikuwa mchezaji bora wa msimu katika Ligi Kuu ya Ivory Coast lazima utambue ni mchezaji wa aina gani. Tatizo letu wakati mwingine ni kumchukua kiungo bora na mchezaji bora katika ligi fulani bila ya kujali aina yake ya uchezaji.
PACOME Zouzoua hakufunga bao katika jioni ambayo Yanga walitamba ugenini dhidi ya Tabora United pale katika ardhi ya Mtemi Mirambo. Hata hivyo aliondoka na tuzo yake kama mchezaji bora wa mechi hiyo.
Bao la kwanza lilifungwa na Israel Mwenda, la pili likafungwa na Clement Mzize akimalizia pasi ya Pacome, la tatu likafungwa na Prince Dube akimalizia pasi ya Pacome.
Simba bado wanaguna kuhusu kiungo wao, Jean Charles Ahoua. Kuna kitu wanatamani kukiona kutoka kwake lakini huwa wanakiona kwa Feisal Salum pale Azam. Fei Toto. Huwa wanatamani kukiona kutoka kwa Ahoua lakini huwa wanakiona kutoka kwa Pacome pale Yanga.
Zamani kitu hiki walikuwa wamezoea kukiona kila wikiendi kutoka kwa Clatous Chotta Chama. kila wikiendi kiungo wao mshambuliaji alikuwa anaondoka uwanjani huku wachezaji wa timu pinzani wakiwa wamechoka kuikaba akili yake kama sio kuukaba mwili wake.
Nimemtazama Jean Charles Ahoua vizuri tu. Ni kiungo mzuri wa matukio. Anafunga, anapiga penalti vizuri. Anapiga mipira ya adhabu vyema. Lakini hajaumbwa kiungo mtawala dimbani. Wazungu kwa kile kiingereza chao huwa wanaita dominant midfielder.

Dominant midfielder ni kiungo anayegeuka, anaondoka na mpira, anaweza kugeuka tena na tena, kisha akaachia nafasi na hapo hapo akapokea tena mpira na kupiga pasi rula kwenda eneo la adui. Kiungo mtawala huku uswahilini kwetu lazima awe na udambwiudambwi. Licha ya kugeuka na kupita katikati ya watu inabidi awe na chenga za madaha, tobo kidogo na kanzu ikibidi.
Ahoua sio kiungo wa namna hii. Ni kiungo anayecheza kwa msingi wa matukio. Nimepata habari za ndani namna ambavyo kuna mabosi wa Simba hawaridhiki naye. Wangefurahi kuwa na Fei Toto kuliko Ahoua. Wanadai amefunga mabao rahisi, pia ‘asisti’ zake ni zile za kupiga faulo zinazotumiwa vyema na washambuliaji wake.
Kwa mpira wetu inakuwa ngumu kumkubali kiungo kama Ahoua. Hachezi kama namba 10 inavyotakiwa kuchezwa kwa mujibu wa viwango vyetu vya mpira. Kwamba namba 10 lazima ndio awe staa wa timu. Kiongozi wa akili za wachezaji wote waliopo uwanjani.

Ninavyojua kwa namna watu wa Simba wasivyoridhika sana na Ahoua licha ya namba zake kuwa vyema, ni kwamba kwa sasa lazima wawe sokoni kuendelea kumsaka namba 10 aina ya Pacome. Labda ndiyo maana licha ya Ahoua kuwa na namba nzuri lakini bado Simba hawajaacha kumuota Fei.
Ulaya kuna viungo ambao waliwahi kutokea wakiwa na aina ya mpira ya Ahoua lakini wakajizolea umaarufu mkubwa. Mfano ni Frank Lampard wa Chelsea. Uwanjani hakuwa na mambo mengi. Lampard alikuwa mtu wa kucheza mpira wa msingi.
Lampard anapiga pasi ndefu kando kisha anakimbilia katika boksi kwa ajili ya kufunga. Ni aina tofauti kabisa na kina Zinedine Zidane ambao walikuwa watawala wa dimba kwa staili ya chenga, pasi, tobo na mengineyo.

Ukiwauliza mashabiki wengi wa Tanzania wangekwenda na nani kati ya Lampard au Zidane ni wazi watakwenda na Zidane. Hata hivyo, Lampard atabakia kuwa mmoja kati ya viungo bora zaidi wafungaji kuwahi kucheza soka. anawazidi Zidane na Ronaldinho katika jambo hilo. Pale Chelsea Lampard ndiye mfungaji wao bora wa muda wote katika historia.
Kwa Ahoua nadhani Simba wanapaswa kurudi katika ule msemo wa Kiswahili unaosema ‘kupanga ni kuchagua’. Wanaweza kupanga kuwa na mchezaji wa aina yake au wa aina ya Pacome ambaye hafungi zaidi lakini anatawala dimba.
Lakini hapo hapo narudi nyuma kidogo. Baada ya kukosea sana katika masuala ya usajili hapo katikati msimu huu ulioisha Simba walikuwa wamepania kufanya vema katika soko la uhamisho la wachezaji. walipoenda kwa Jean Charles Ahoua hawakujua ni mchezaji wa namna gani?

Hapa tunarudi nyuma katika suala la kuskauti wachezaji. Nadhani bado tupo nyuma bila ya sababu za msingi. Tunapohitaji mchezaji wa kuziba nafasi ya Chama na mwenye sifa kama za Chama nadhani tunahitaji kuwa na utulivu wa kusaka mchezaji wa aina yake.
Unapohitaji mchezaji kama Ahoua, licha ya kuwa alikuwa mchezaji bora wa msimu katika Ligi Kuu ya Ivory Coast lazima utambue ni mchezaji wa aina gani. Tatizo letu wakati mwingine ni kumchukua kiungo bora na mchezaji bora katika ligi fulani bila ya kujali aina yake ya uchezaji.
Viungo wamegawanyika katika sifa mbalimbali na ni bora mabosi wetu wajue aina ya wachezaji wanaowataka kwa wakati huo. Sio kila kiungo wa mbele ni kiungo mchezeshaji. Sio kila kiungo wa mbele ni mfungaji. Wachezaji wagawanyika katika aina tofauti za uchezaji wao. Steven Gerrard sio Ronaldinho.

Labda tu kwa kiherehere changu cha kuhisi mambo, nadhani mwishoni mwa msimu tutasikia wengi. Nadhani kuna kundi la mabosi ambao watataka Chama arudi kwa ajili ya kutawala dimba kama Pacome anavyofanya Yanga au Feisal anavyofanya Azam.
Wengine nasikia wamekunja moyo na hawataki kusikia jina la Chama. Hata huku kwa wanachama na mashabiki hali ni hii hii. Aliwasumbua sana na kitendo cha kwenda kucheza Yanga kilihitimisha hisia zao, mchezaji huyo alikuwa na mapenzi makubwa na Yanga angali akiwa anavaa jezi zao za nyekundu na nyeupe kitu ambacho kilikuwa kinaleta usumbufu mkubwa kwao.