Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JICHO LA MWEWE: Wamorocco wametupeleka ‘Kigoma’ yao, hatuna wasiwasi

JICHO Pict

Muktasari:

  • Hakukuwa na mpira ulioingia katika nyavu zozote za timu hizo mbili huku Algeria wakiwa wameshafuzu katika kundi hilo. Taifa Stars ikafanikiwa kufuzu kupitia suluhu hiyo ambayo ilipatikana katika mkoa wa ‘Iringa’ ya huko. Tulirudi na shangwe kubwa. Ngamia alikuwa amepenya katika tundu la sindano.

SEPTEMBA 7, 2023, Waalgeria waliipeleka Taifa Stars katika jiji la Annaba lilipo kaskazini Mashariki mwa Algeria, kilomita takribani 600 kutoka katika mji mkuu wa Algeria, Algers kwa ajili ya pambano ambalo kwao halikuwa na umuhimu kufuzu kwao michuano ya Afcon ya mwaka 2024.

Hakukuwa na mpira ulioingia katika nyavu zozote za timu hizo mbili huku Algeria wakiwa wameshafuzu katika kundi hilo. Taifa Stars ikafanikiwa kufuzu kupitia suluhu hiyo ambayo ilipatikana katika mkoa wa ‘Iringa’ ya huko. Tulirudi na shangwe kubwa. Ngamia alikuwa amepenya katika tundu la sindano.

Juzi Wamorocco tena wamefanya tabia hii. Kwa kiasi fulani ni tabia njema. Nitakwambia kwanini. Lakini kwanza Taifa Stars wamelazimika kusafiri mwendo wa saa moja na dakika 45 kwa ndege kutoka Casablanca kwenda katika jiji la Oujda kucheza pambano la kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya wenyeji hawa.

Nilikosa tiketi ya ndege kutoka Casablanca kwenda Oujda na nililazimika kusafiri mwendo wa saa tisa za treni kutoka Casablanca kwenda Oujda mji ulio kaskazini Mashariki mwa Morocco karibu na mpaka na mahasimu wao Algeria. Ilikuwa safari ndefu. Mwendo wa saa moja na dakika 45 kwa ndege ina maana Wamorocco wameipeleka Taifa Stars ‘Kigoma’ yao.

JICH 02

Kwanini wanafanya hivi? Kwanza kabisa wanautawanya mpira wao. Sio tu kwamba wanautawanya mpira wao kwa bahati mbaya, hapana, wana kila sababu. Wana vitendea kazi vingi. Kila uwanja wao unakidhi vigezo vya CAF na FIFA. Je, uwanja wa Lake Tanganyika pale Kigoma unakidhi vigezo vya FIFA na CAF? Ni jambo la kujiuliza.

Rafiki zetu Misri wanaweza kupeleka mechi Ismailia, Alexandria, Cairo na kwingineko. Sisi ukifungiwa Uwanja wa Taifa tu habari yetu imekwisha. Ni kama ilivyo kwa hapa Morocco,  Tunisia, Algeria, Afrika Kusini na nchi nyingine chache zilizoendelea barani Afrika. Sisi kazi tunayo. Sio kazi ndogo.

Lakini hapo hapo kumbuka kwamba ‘Kigoma’ zao zina hoteli za kutosha kukidhi mahitaji ya timu mbili, maofisa wa CAF, waamuzi, na wageni mbalimbali wanaotarajiwa kuhudhuria mechi husika. Haishangazi kuona nchi kama Morocco inaandaa michuano ya Afcon kwa wakubwa, watoto under 15 na under 17, pamoja na ile ya wanawake ndani ya mwaka huu tu.

JICH 03

Tuachane na hilo. Mechi kama hii kuchezwa Oujda ina maana gani? Ni mechi ambayo itaacha simulizi kwa wakazi wa hapa. Hawachezi mechi hizi mara nyingi lakini kwa kuletewa mechi hizi wanapata fursa ya kuwaona mastaa wao wakubwa wanaotamba Ulaya. Kina Hakim Ziyech, Achraf Hakimi, Sofiane Amrabat, Sofiane Bafoul na wengineo kibao.

Wakati wa Oujda kwa kuletewa mechi hii wanamaanisha wameletewa deni kubwa la kuishangilia timu kama inavyocheza Rabat, Casablanca, Marreikh na miji mingine mikubwa ya Morocco. Kazi kwao kuhakikisha Morocco wanapata pointi tatu ambazo zitawasogeza kwenda katika Kombe la Dunia mwakani.

Inanikumbusha namna ambavyo mastaa wa Algeria waliwaangusha mashabiki wa Annaba katika pambano lile ambalo Taifa Stars walitoka suluhu na Algeria na kufanikiwa kupata tiketi ya kushiriki michuano ya Afcon mwaka jana pale Ivory Coast. Sio kwamba Algeria walikuwa wanahitaji chochote katika mechi ile, basi tu, mashabiki wa Algeria walitaka timu yao ishinde.

JICH 01

Kwa Kiswahili cha mtaani mashabiki wa Algeria walikuwa wanataka timu yao iifanyie roho mbaya Taifa Stars bila ya kujali athari ambazo zingeweza kutokea kwa Watanzania. Ndivyo mpira ulivyo. Ndicho ambacho walikihitaji kuliko kitu chochote kile kwa wakati huo. Ndivyo nidhamu ya mpira ilivyo.

Vipi kuhusu hawa Wamorocco wa Oujda waliopewa fursa ya kuisogeza Morocco katika michuano ya Kombe la Dunia mwakani kule Marekani, Canada na Mexico? Itakuwa kazi ngumu kwa wachezaji wa Taifa Stars, benchi la ufundi na Watanzania wanaoiombea mema Taifa Stars pale Oujda.

Vipi kwa wachezaji wa Taifa Stars wenyewe? Wachezaji ni watu wa ajabu. Wala hawana presha. Kwanza kabisa nitakusimulia presha za namna mbili. Kwanza ni kwa wachezaji wa Simba na Yanga waliopo hapa Oujda. Hawana habari na jambo kubwa linaloendelea kwa sasa katika mitandao ya Tanzania pamoja na mitaani. Kuhusu kuahirishwa kwa pambano lao wiki iliyopita.

JICH 03

Wanakaa pamoja, wanapiga stori pamoja, wanakula pamoja, wanatembea pamoja. Wengine wana urafiki mkubwa baina yao kama Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Mudathir Yahaya. Hawana habari na mambo ya Simba na Yanga. Wanaongea mambo yao. Mashabiki mitaani ndio wana maneno zaidi. Wao siasa za kwanini mechi haikuchezwa haziwahusu.

Na pia kuna urafiki mkubwa baina ya Feisal Salum na wachezaji wa Yanga. Kilichotokea kati ya Fei na Yanga hakiwahusu wachezaji na urafiki wao. Haya ndio maisha ya kila siku ya wachezaji. Inakuwa tofauti na hisia za mashabiki wanaotokwa na mapovu mitaani na mitandaoni. Wengine wanatukanana kabisa.

Presha nyingine ambayo haipo kwa wachezaji wenyewe ni kuhusu mechi yenyewe. Ni ngumu kama ilivyo lakini wachezaji wetu huwa hawakosi usingizi kuwaza mechi. Wanaishi maisha yao kama kawaida na haukuti wanazungumzia mechi. Wanachosubiri ni kucheza tu basi. Ni tofauti na mawazo ya mashabiki wengi kwamba wachezaji huwa wanawaza sana kuhusu mechi. Ni kama ambavyo sisi huwa hatuziwazi sana kazi zetu lakini tunazifanya.

JICH 05

Nini kitaenda kitokea uwanjani? Binafsi nimeanza kuambukizwa kutokuwa na wasiwasi kama ambavyo wachezaji wasivyo na wasiwasi. Tofauti yetu ni moja tu. Mimi sina wasiwasi kwa sababu na wao siku hizi wanacheza vizuri bila ya wasiwasi. Wanakaa na ‘mali’ mguuni na wanacheza bila ya hofu. Kwanini niwe na hofu? Ni tofauti na zamani ambapo usingeweza hata kuona pasi saba mfululizo kutoka kwa wachezaji wa Taifa Stars. Siku hizi unaona pasi nyingi.

Hii imesababishwa na wachezaji wetu kuwa na ‘exposure’ na mechi hizi. Inaanzia katika vilabu vyao. Wachezaji wa Simba na Yanga wanacheza mechi ya CAF na klabu kubwa za Afrika na wanafika mbali. Wachezaji wa Azam akina Lusako Mwaikenda pia wanacheza mechi hizi. Halafu kuna akina Novatus Dismas nao wanacheza Ligi zinazoeleweka Ulaya.

Kunakuwa na kiburi chanya kutoka kwa wachezaji wetu na huwa inatusaidia. Sawa, Morocco wapo juu yetu na huenda wapo tayari zaidi kuiwakilisha Afrika katika kombe la dunia kuliko sisi. Hata hivyo acha kwanza mpira uchezwe uwanjani halafu aliye juu aonyeshe kama anastahili kuwa juu na kuiwakilisha Afrika katika kombe la dunia. Hatuwezi kugawa pointi tatu kwa mdomo tu.

JICH 04

Hali ya hewa ni baridi. Hawa jamaa wamepakana na Ulaya. Wakati msimu wa baridi ukiwa unataka kutoweka Ulaya na wao msimu wa baridi pia unakuwa unataka kutoweka kwao. Hata hivyo kwa kiwango cha ngozi zetu bado tunaona baridi hasa. Acha twende uwanjani Jumatano baada ya futari tukapashane joto hasa. Kila la kheri Taifa Stars.