Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jonas Mkude ameamua kuzisusia timu za mitaa ya kati?

HISIA Pict


KAMA tunaamini katika mtandao wa Wikipedia basi tuamine kwamba Jonas Mkude ana umri wa miaka 33 tu mpaka sasa. Sijui yuko wapi. Sijui ana mipango gani na mpira? Sijui amepata kazi nyingine? Sijui.


Ninachojua ni kwamba kuna uwezekano mkubwa akawa ameingiwa na uvivu wa kucheza. Baada ya kucheza timu mbili kubwa kwa muda mrefu labda anasikia uvivu wa kucheza mpira katika timu nyingine za kawaida.

Asikuambie mtu timu nyingine zinatia uvivu kuzichezea kama umecheza kwa wakubwa hawa kwa muda mrefu. Simba, Yanga na Azam wachezaji wake wanadekezwa. Wanatumia usafiri wa anga kwa muda mrefu kuliko timu nyingine.

Maisha yanakuwa rahisi. Simba na Yanga wakienda kucheza Ruangwa huwa wanapanda ndege mpaka Mtwara kisha wanalikuta basi lao na kwenda zao Ruangwa. Zamani maisha hayakuwa hivi kwa kina Edibily Lunyamila.

Kuna timu ilikuwa inaitwa RTC Kigoma. Ili uende kucheza na RTC Kigoma ulikuwa unalazimika kutumia usafiri wa reli ya kati kwa siku tatu. Unafika Kigoma ukiwa hoi. Unacheza mechi ukiwa hoi na unalazimika kupata matokeo. Baada ya hapo unalazimika kurudi kwa usafiri huohuo.

Wakati huo Kigoma ilikuwa haifikiki kwa lami, lakini leo inafikika kwa lami na bado wakubwa wanatumia ndege kwenda kucheza mechi zao. Uchumi wa klabu umekuwa mkubwa. Lakini sio klabu zote.

Wachezaji wa timu kubwa pia wanafikia hoteli za hadhi ya nyota tano. Wanafikia hoteli bora zaidi mikoani tofauti na kina Lunyamila ambao walikuwa wanafikia ‘guest house’ za hadhi ya chini kabisa.

Na kichekesho kinakuja pale ambapo viongozi walishindwa hata kulipa pesa ya ‘guest house’ na mwishowe kulikuwa na aibu ya mizigo ya wachezaji kushikiliwa mpaka malipo yanapofanyika. Imewahi kuwatokea sana kina Ken Mkapa.

Hali imekuwa tofauti kwa sasa. Nadhani kuna klabu ambazo zimeamua kuwekeza zaidi lakini kuna ambazo hazijawekeza vya kutosha na hizi ndizo ambazo Mkude itakuwa amezikimbia msimu huu. Klabu ambazo mpaka leo zinasafiri kwenda kucheza na Mashujaa kwa kutumia mabasi.

Mchezo wa soka ni kazi ya muda mfupi. Kuna mambo mawili unapaswa kuyafanya unapocheza soka la Tanzania. Hii ni kwa wachezaji wetu ambao hawapendi sana kucheza soka la kulipwa nje ya mipaka yetu.

Jambo la kwanza ni kuhakikisha unakusanya pesa zako nyingi na kuwekeza ili ukiachana na wakubwa uende kufanya biashara zako moja kwa moja kama hautaki kupanda basi la Namungo au JKT Tanzania na kusafiri kwenda Mbeya kucheza na Tanzania Prisons.

Jambo la pili ni kuendelea tu kukaza moyo na kuendelea kupambana kama ambavyo Thomas Ulimwengu aliyekuwa TP Mazembe ya moto, leo anacheza Coastal Union ya Tanga. Hatujui Mkude amechagua jambo gani katika haya.

Tunachojua ni kwamba mpaka alipoishia kipaji alikuwa nacho na uwezo wa kucheza timu nyingi za Ligi Kuu Bara ulikuwepo. Kuna timu nyingi tu ambazo angeweza kuzisaidia hapa na pale. Ni kama ambavyo Kevin Yondani naye umri ulikuwa umesogea lakini alikuwa ameamua kuzisaidia timu kadhaa za Ligi Kuu huku akiwa na kitambaa cha unahodha.

Hata Erasto Nyoni ambaye alionja ladha ya utamu wa Ligi Kuu kwa kucheza Azam na Simba naye aliamua kwenda kuwasaidia Namungo. Sasa hivi amekwenda kuisaidia Kagera Sugar. Wote hawa walikuwa wakubwa kwa Mkude, lakini nadhani Mkude ameamua kutususa.

Mwingine ambaye hatujui kama atatususa au vinginevyo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’. Dakika chache anazocheza Yanga zinakuonyesha kwamba kuna timu nyingine ambazo anaweza kuzisaidia kama akiachana na Yanga baada ya mechi ya leo. Tusubiri na kuona.

Inawezekana pia Mkude amepata pesa za kutosha katika mpira na sasa anafanya mambo yake. Hata hivyo ni vyema akatumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kututangazia kwamba ameachana na soka rasmi. Hatujui kwanini amepiga kimya. Hatujui yupo wapi na anafanya nini.

Umekuwa sio utamaduni kwa wachezaji wetu kutuambia hatima zao kuhusu mpira. Hata Juma Kaseja hakuwahi kututangazia rasmi kwamba amestaafu soka. Tulimuona tu ameibukia katika kazi ya ukocha - mchezaji baadaye akawa kocha rasmi. Wachezaji wasitufanyie hivi.

Kama Jonas anafanya biashara zake, basi ni jambo la heri. Wapo wachezaji wengi ambao wanaamua kustaafu mapema. Hata Ulaya kina Eric Cantona waliamua kustaafu mapema wakafanya mambo yao mengine. Ni suala la kututangazia tu.

Lakini pia ni wakati wa kuchunguza namna ambavyo tunaweza kufanya kuzisaidia klabu nyingine ziwe na uchumi mzuri ili kina Mkude wasisikie uvivu kwenda kuchezea. Kwa mfano, ni kweli kwamba Manchester United ni klabu yenye uchumi mzuri lakini kina West Ham United pia wana uchumi mzuri.

Haishangazi kuona kina Aaron Wan Bissaka wameangukia huko baada ya kuondoka Manchester United. Huku kwetu inatia uvivu kwelikweli. Kama haujajipanga kimaisha inaweza kukuachia kisirani kikubwa na ukasusa kwenda kucheza timu hizo.

Kuna wachezaji wengine wa timu kubwa wakienda katika klabu hizo wanajikuta wanaleta vurugu na kile kinachoitwa utovu wa nidhamu kwa sababu hawakubaliani moja kwa moja na mazingira ya timu.

Saido Ntibanzokiza alipokwenda Geita Gold aliamua awe anajikatia tiketi zake za ndege pindi timu ilipokuwa inakwenda kucheza mbali na Geita. Katika hali ya kawaida inaweza kuleta mgawanyiko katika timu.