Prime
Wino wa Januari unavyotishia 'falme za zamani'
UNAWEZA kusema ndani ya Ligi Kuu Bara hivi sasa shilingi imegeuka. Wale nyota waliopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri msimu huu wa 2025-2026, wameachwa mbali baadhi yao na wale walioingia dirisha dogo la Januari 2026.
Kumbuka pazia la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, linafungwa Jumanne Juni 30, 2026 baada ya kushuhudia ushindani wa hali ya juu zaidi tangu mwanzoni, huku siku hiyo ikiwa ni muhimu zaidi kwa mashabiki wa soka kwa ajili ya kutambua bingwa mpya.
Vita ya ubingwa kwa sasa imebakia kwa miamba miwili ya soka nchini, Yanga inayopambania kutetea taji hilo ililochukua kwa misimu minne mfululizo na watani zao wa jadi Simba, inayosaka ubingwa huo kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2020-2021.
Yanga iko kileleni na pointi 72 baada ya kushinda mechi 22, sare sita na kupoteza moja, ikifunga mabao 68 na kuruhusu tisa, huku Simba ikiwa ya pili na pointi 70, ikishinda 21, sare saba na kupoteza moja, ikifunga mabao 53 na kuruhusu 11.
Ukiachana na mbio za ubingwa huo, sehemu nyingine inayovuta hisia zaidi na inayotazamwa huenda ikaleta ushindani ni ya kumpata Mchezaji Bora wa Msimu (MVP), kutokana na viwango bora vinavyoendelea kuonyeshwa na nyota wa timu mbalimbali.
Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ alionekana huenda tuzo hiyo ikamuhusu moja kwa moja kutokana na kiwango chake hadi sasa, ingawa uwepo wa Allan Okello wa Yanga na Mossi Nduwumwe wa Singida Black Stars umebadili upepo. Mwanzo katika wanaotajwa kuwania tuzo hiyo, pia alikuwepo Pacome Zouzoua wa Yanga na Clatous Chama aliyeanzia Singida Black Stars kabla ya dirisha dogo kutua Simba.
Ukiangalia takwimu, Fei Toto ndiye aliyechangia mabao mengi ya Ligi Kuu Bara, baada ya kuhusika na 23, akifunga 15 na kuasisti manane, amecheza mechi 27 kati ya 29.
Nyota huyo amefanya mapinduzi msimu huu tofauti na 2024-2025, alipohusika na mabao 17, kufuatia kufunga manne na kutoa asisti 13.
Licha ya Fei Toto kuongoza kwa mabao 15 hadi sasa, lakini kiungo huyo anakabiliwa na rekodi mbili ngumu za kuzivunja katika mechi moja iliyobaki dhidi ya Dodoma Jiji, ambapo ya kwanza ni ya kuivuka ya msimu wa 2023-2024 na ya pili ni ya kuiandikia Azam historia.
Katika msimu wa 2023-2024, Fei Toto alifunga mabao 19 na sasa amebakisha mabao manne ili kuifikia rekodi yake, japo nyota huyo alikosa tuzo ya ufungaji bora, baada ya aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz KI kufunga mabao 21.
Mbali na hilo, Fei Toto anakabiliwa na rekodi nyingine ya kushinda Tuzo ya Mfungaji Bora akiwa na kikosi cha Azam, kwani mara ya mwisho mchezaji wa timu hiyo kushinda alikuwa Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast msimu wa 2012-2013.
Katika msimu huo wa 2012-2013, Kipre Tchetche aliifungia Azam mabao 17 na kushinda Tuzo ya mfungaji bora wa msimu na wa Azam pia. Kuanzia hapo hakuna nyota mwingine wa kikosi hicho aliyefanya hivyo, ikiwa ni msimu wa 13, umetimia.
Tchetche alitua Azam Januari 1, 2011, akitokea Jeunesse Club d’Abidjan ya Ivory Coast, aliondoka Julai 2016 na kujiunga na Al-Nahda na baadae Al-Suwaiq za Oman, kisha Kuching City na sasa Penang FC zote za Malaysia.
Licha ya Fei Toto kujiweka katika nafasi nzuri, miongoni mwa wachezaji wanaoweza kumwekea doa la kushinda tuzo zote mbili ni viungo washambuliaji, ambao ni Mganda Allan Okello wa Yanga na Mrundi Mossi Nduwumwe wa Singida Black Stars.
ALLAN OKELLO
Kiungo wa Yanga, Mganda, Allan Okello ‘Star Boy’ aliyejiunga na kikosi hicho Januari 12, 2026, akitokea Vipers SC ya kwao Uganda, baada ya mwanzo mgumu, hivi sasa amekuwa lulu na miongoni mwa wachezaji pendwa wa mashabiki hasa wa timu hiyo kutokana na kiwango chake.
Okello anashika nafasi ya pili kwa nyota waliochangia mabao mengi, akihusika na 21, akifunga 14 na kuasisti saba, akiendeleza kiwango bora kinachoashiria huenda akaingia katika vita ya MVP mwishoni mwa msimu.
Mbali na kuwania Tuzo ya MVP, Okello ana nafasi ya kuibuka mfungaji bora kutokana na idadi ya mabao 14 aliyofunga ambayo ni sawa na ya Mossi Nduwumwe wakizidiwa moja tu na Fei Toto aliyefunga 15.
Nyota huyo katika kipindi kifupi alichopo Yanga, amekuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho akicheza mechi 23. Mbali na kupiga hat trick, pia ana rekodi ya kutoa asisti tatu katika mechi moja dhidi ya Pamba Jiji, Yanga ikishinda 3-0.
MOSI NDUWUMWE
Amekuwa miongoni mwa nyota wa kutazamwa kutokana na kiwango chake anachoendelea kukionyesha, ambapo licha ya kutokuwa na asisti yoyote hadi sasa, ila ugeni wake sio tatizo la kuendelea kucheka na nyavu za wapinzani kwa msimu huu.
Nyota huyo aliyezaliwa Januari 1, 2002, alijiunga na Flambeau du Centre FC Julai 1, 2023, baada ya kuachana na Musongati FC ya kwao pia Burundi, ambapo aliwavutia zaidi mabosi wa Singida walipokutana katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Singida ilikutana na Flambeau katika hatua ya pili kusaka tiketi ya kufuzu makundi, ambapo ilifuzu kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare ya bao 1-1, Burundi, Oktoba 19, 2025, kisha kushinda jijini Dar es Salaam, mabao 3-1, Oktoba 25, 2025.
Kiwango bora alichokionyesha katika mechi hizo mbili, kikawavutia mabosi wa Singida ambao dirisha dogo la Januari 2026, wakamsajili wakiamini atakuwa ni nguzo muhimu kwa kikosi hicho na sasa matunda yake wameanza kuyafaidi kwa muda mfupi.
Nduwumwe ndiye mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga Hat-Trick, katika ushindi wa Singida wa mabao 5-0 dhidi ya Dodoma Jiji, Juni 17, 2026, akifuatiwa na Mathew Momanyi wa Pamba Jiji, Fabrice Ngoy (Namungo FC) na Allan Okello (Yanga).
Nyota huyo mabao 14 aliyofunga katika ligi, yametokana na mechi 21, akizidiwa mbili na Okello, pia akipitwa sita na Fei Toto.
MTIHANI ULIPO
Katika mechi za mwisho zitakazoamua, Azam FC itakuwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kuikaribisha Dodoma Jiji, huku Yanga ikicheza ugenini kupambana na JKT Tanzania, wakati Singida Black Stars itaifuata Fountain Gate.
Mechi hizo tatu, ndizo zinaweza kuamua hatima ya mfungaji bora na mchezaji bora wa msimu yaani MVP, kwa wachezaji watatu, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Allan Okello na Mossi Nduwumwe ambao wanaoonekana na kupewa nafasi zaidi ya kushindania.
Kati ya nyota hao watatu, Fei Toto anadaiwa na wenzake kufunga hat trick kwani wao wameshafunga, hivyo dhidi ya Dodoma Jiji, huenda kiungo huyo naye akaingia kwenye orodha ya wachezaji wenye hat trick Ligi Kuu Bara ambapo hadi sasa hakuna mzawa aliyefunga.
Simba SC attacking midfielder Elie Mpanzu celebrates after scoring against Pamba Jiji FC at the KMC Complex yesterday. Simba secured a 2-1 victory in the match. PHOTO | COURTESY
MPANZU ASAKA REKODI
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Elie Mpanzu ndiye anayeongoza kwa wachezaji wenye asisti nyingi msimu huu hadi sasa, ambapo nyota huyo anazo 10, akibakisha tatu kuifikia rekodi ya Fei Toto aliyoiweka msimu wa 2024-2025, alipokuwa na 13.
Msimu uliopita wa 2024-2025, Mpanzu alitoa asisti sita kwa maana hivi sasa ameivunja rekodi yake na sasa anaifukuzia ya Fei Toto huku ikibakia mechi moja tu kwa timu hiyo dhidi ya KMC iliyoshuka daraja.
Asisti zake 10 zimetokana na mechi 24 alizocheza kati ya 29. Mechi saba za hivi karibuni, Mpanzu amehusika kwenye jumla ya mabao saba, takwimu zinazomfanya kuwa kama ameibuka upya kufuatia hapo awali kuonekana kushuka kiwango.
DIARRA MFALME MPYA
Ushindi wa Yanga wa mabao 3-0 dhidi ya TRA United, Juni 27, 2026, umemfanya nyota wa timu hiyo, Djigui Diarra kuwa mfalme mpya kwa msimu huu wa 2025-2026 baada ya kufikisha Clean Sheets 17, ambazo haziwezi kufikiwa na makipa wengine ndani ya ligi hiyo msimu huu.
Clean Sheets hizo 17 za Diarra ni sawa na alizokuwa nazo pia msimu wa 2024-2025, alipozidiwa mbili na kipa wa Simba, Moussa Camara aliyeibuka kidedea baada ya kufikisha 19, ikiwa ni msimu wake wa kwanza tu tangu ajiunge na kikosi hicho.
Camara aliyejiunga na Simba Agosti 1, 2024, akitokea Horoya AC ya kwao Guinea, alifikisha Clean Sheets hizo 19 na kuifikia rekodi iliyokuwa inashikiliwa na aliyekuwa kipa wa kikosi hicho, Aishi Manula aliyoiweka msimu wa 2017-2018.
Manula ambaye kwa sasa anaichezea Azam FC aliyowahi kuitumikia awali, alikuwa ni kipa wa mwisho wa Simba kufikisha Clean Sheets 19, hata hivyo, rekodi hiyo ilifikiwa na Camara ambaye tangu msimu umeanza ameandamwa na majeraha yaliyofanya kuondolewa kikosini. Kipa aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kushindana na Diarra msimu huu ni Mahamadou Tanja Kassali wa Simba, aliyejiunga na kikosi hicho dirisha dogo la Januari 2026, akitokea AS FAN Niamey ya kwao Niger ambaye hata hivyo hawezi pia kuzifikia.
Kassali ana Clean Sheets 15 hadi sasa katika mechi 21 na hata asiporuhusu bao lolote katika mechi ya mwisho dhidi ya KMC, maana yake ataishia na 16, ambazo haziwezi kufikia za Diarra. Kuumia kwa Camara mwanzoni mwa msimu na kuondolewa katika mfumo dirisha dogo ili nafasi yake kuchukuliwa na Kassali, kumechangia zaidi kwa Diarra kumaliza kinara wa Clean Sheets baada ya msimu wa 2024-2025 kuzidiwa.
Kwa namna ambavyo Simba imebadilisha makipa kumetoa nafasi kwa Diarra ambaye ameanza katika mechi 23, akikosa sita pekee ambazo Aboutwalib Mshery, Hussein Masalanga na Khomein Abubakar kabla ya kuumia, ndiyo walipata nao nafasi ya kuanza.
Ukija kwa Azam, Manula alikaa nje kwa muda mrefu, lakini alipoanza kucheza Oktoba 2025, hadi sasa amefanikiwa kukusanya clean sheet 13 akianza katika mechi 15, hivyo ameruhusu bao katika mechi mbili pekee.
Uamuzi wa Kocha wa Azam, Florent Ibenge kufanya mabadiliko ya mara kwa mara katika eneo hilo la makipa akimtumia Manula, Zuberi Foba mwenye clean sheet tisa akicheza mechi 11, huku Issa Fofana naye akidaka mechi tatu akiambulia clean sheet moja, yamechangia kumpa nafasi Diarra kuweka utawala wake.
Kwa wastani ukiangalia mechi alizodaka Manula au Foba, endapo mmojawapo angeongeza idadi ya mechi angetoa ushindani mkubwa kwa Diarra. Kumbuka Manula na Foba wameruhusu bao katika mechi mbili pekee kila mmoja, wakati Diarra akiruhusu mechi tano.