Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbogo afunguka tuhuma za Yanga, Toto Africans

MBOGO Pict


ILIPOISHIA

“Mpira hauna uraia. Anayecheza vizuri ndiye anayestahili nafasi. Lakini ilitufike hapo vijana wetu lazima wajitume zaidi na wajiamini. Tukifanya hivyo, tutanya hivyo, tutakuwa na Watanzania wengi watakaong’ara hata nje ya nchi kama ilivyo kwa Chama na Pacome walivyokuwa mfano wa ubora katika ligi yetu.”

SASA ENDELEA...


“Baada ya kuachwa kwa mara nyingine, Ladislaus Mbogo alirudi Burundi kuendelea na maisha ya soka. Lakini aliporejea Tanzania kwa mapumziko, viongozi wa Toto Africans walimtafuta tena kwa mara nyingine.

“Waliniomba tusameheane nirudi. Kwa sababu naipenda timu yangu nikakubali.”

Anasema aliporejea alikuta mazingira ya uongozi yamebadilika kabisa.

“Kulikuwa na viongozi wapya, wengine walikuwa hawaijui historia ya timu wala watu waliokuwa wameijenga,” anasema.

Mbogo anaamini baadhi ya viongozi hao walikuwa na ajenda zao binafsi ambazo ziliathiri hata wachezaji.

“Kuna mambo mengi yalikuwa yanafanyika nyuma ya pazia. Nilikuwa mwenyeji, kwa hiyo sikukubali kuona mambo yasiyo sahihi yanaendelea.”

Anasimulia tukio moja ambalo anasema liliharibu taswira yake bila kosa wakati wakiwa na mechi dhidi ya Yanga.

“Siku moja nilimsalimia tu mchezaji mmoja ambaye tulikuwa naye Yanga akiwa timu ya vijana. Baadaye nikashangaa imegeuzwa nimekwenda kuwapa siri wapinzani,” anasema.

Kwa madai hayo, anasema viongozi walimfungia kucheza; “Waliniambia sitacheza mpaka mechi ipite. Nilishangaa sana kwa sababu sikuwa nimefanya kosa lolote.”

Anasema matukio kama hayo ndiyo yaliyokuwa yakiivuruga Toto African na hatimaye kuifanya ishuke kutoka Ligi Kuu.


CORONA ILIVYOFUNGUA MILANGO

Baada ya Toto African kushuka daraja mwaka 2018, Mbogo anasema aliamua kuweka pembeni maisha ya soka.

“Nilijiambia safari yangu ya mpira imefika mwisho. Nikabaki nacheza na timu za veterani tu.”

Lakini ndani yake bado kulikuwa na ndoto aliyokuwa ameibeba kwa miaka mingi.

Anasema mwanzo wa yote ulikuwa wa kawaida sana. Rafiki yake mmoja, Mzee Bitala, alimwomba amsaidie kumfundisha mtoto wake kucheza mpira.

“Wakati ule kulikuwa na kipindi cha Corona. Nikaanza na mtoto mmoja. Baadaye wakawa wawili, watatu, wanne, mpaka wakaanza kuongezeka,” anasema.

Ndipo akagundua kuwa alikuwa anajenga kitu kikubwa kuliko alivyokuwa akifikiria; “Nikajiambia, mbona mimi si mtu wa kuajiriwa. Nikafungua akademi yangu rasmi.”

Baada ya kukamilisha taratibu zote za usajili, ndipo ikazaliwa Mbogo Sports Akademi.

MBOG 05

MAMBO YAMEBADILIKA

Mbogo anaamini watu wengi wanaweza wasione tofauti kubwa kati ya soka la zamani na la sasa, lakini kwake kuna mambo mengi yamebadilika.

“Kiwango cha wachezaji mmoja mmoja kimeshuka kidogo, si Tanzania pekee hata sehemu nyingine. Tofauti kubwa ipo kwenye mbinu za ufundishaji. Wenzetu wamewekeza sana kwenye elimu ya makocha na maendeleo ya wachezaji.”

Anasema Tanzania ina vipaji vya kutosha, lakini changamoto ni namna ya kuviendeleza.

“Kama tunataka timu yetu ya taifa iwe bora zaidi, lazima wachezaji wetu wengi waende kucheza nje ya nchi. Huko ndiko wanakutana na ushindani mkubwa na mbinu mpya,” anasema.

Anatoa mfano wa nchi kama DR Congo, ambayo sehemu kubwa ya wachezaji wake wa timu ya taifa hucheza nje ya nchi.

“Ndiyo maana hata sisi tukipata nafasi ya kuwapeleka vijana wetu nje mapema, tutaanza kuona matokeo makubwa zaidi,” anasema.

MBOG 03

MADOGO WA SERENGETI BOYS

Mbogo anasema amefurahishwa na maendeleo ya timu za taifa za Tanzania katika miaka ya karibuni.

Anaamini taifa limeanza kuonyesha dalili za kupiga hatua baada ya kurejea mara kwa mara kwenye michuano mikubwa ya Afrika.

“Ukicheza na timu kama Morocco leo unaona tofauti ilivyopungua. Zamani ilikuwa ngumu hata kuwapa presha lakini sasa wanafanya kazi kweli kutushinda,” anasema.

Anasema mafanikio ya timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 yanapaswa kuwa mwanzo wa mpango mkubwa wa maendeleo.

“Wale vijana wasipelekwe haraka Simba au Yanga. Wapewe nafasi ya kwenda kucheza nje ya nchi. Wakikulia kwenye ushindani wa kimataifa, baada ya miaka michache watakuwa uti wa mgongo wa Taifa Stars,” anasema.

Kwa mtazamo wake, idadi kubwa ya Watanzania wanaocheza nje ndiyo itakayoifanya Tanzania kuwa taifa kubwa kisoka.

MBOG 06

MPIRA NI BIASHARA

Mbogo anasema tofauti kubwa kati ya enzi zao na sasa ni namna klabu zilivyoanza kuutazama mpira kama biashara.

“Leo kila mtu ameelewa kwamba mpira ni pesa, ndiyo maana unaona klabu zinawekeza sana.”

Anasema si ajabu kuona Simba na Yanga zikitoa fedha nyingi kwa wachezaji wa kigeni.

“Unalipa mchezaji wa kigeni mshahara mkubwa kwa sababu unaamini atakusaidia kupata mafanikio, huo ndiyo uwekezaji,” anasema.

Anaongeza kuwa mafanikio ambayo klabu hizo zimekuwa zikiyapata kimataifa hayajatokea kwa bahati mbaya.

“Wanawekeza, ndiyo maana wanafika mbali, mimi naamini ipo siku timu ya Tanzania itachukua ubingwa mkubwa Afrika, “ anasema.

MBOG 04

HAWA WALIKUWA TISHIO

Akiulizwa ni washambuliaji gani waliomtesa zaidi akiwa beki, Mbogo anacheka kabla ya kukiri kuwa kulikuwa na baadhi ya majina ambayo beki yeyote hakutamani kuyakabili.

“Kama unasikia leo unacheza dhidi ya Okwi, lazima uanze kufikiria mara mbili. Alikuwa msumbufu sana,” anasema.

Anawataja pia Jerry Tegete, Mrisho Ngassa, Shamte Ally, Felix Sunzu, Boniface Ambani pamoja na mshambuliaji Mganda Mike Katende kuwa ni miongoni mwa washambuliaji waliokuwa na uwezo mkubwa.

“Wale walikuwa na ubora wa kweli, beki ukikutana nao lazima ujipange,” anasema.


MPIRA UMEMLIPA

Licha ya kutokufikia ndoto yake ya kucheza Ulaya au ligi kubwa nje ya Afrika, Mbogo anasema hana sababu ya kujutia maisha yake ya soka.

“Mpira umenipa marafiki, umenizungusha sehemu nyingi na umenitengenezea jina,” anasema huku akitabasamu.

Anasema wakati mwingine watu hupima mafanikio kwa fedha pekee, lakini yeye anaamini kuna mambo mengi aliyoyapata kupitia soka.

“Kama nisingekuwa mchezaji, pengine hata wewe usingekuja kufanya mahojiano haya. Hiyo nayo ni sehemu ya mafanikio,” anasema.

Anakiri kuwa ndoto yake ilikuwa kucheza nje ya Tanzania kwa kiwango kikubwa zaidi, lakini anaamini Mungu alimpa kile kilichokuwa sehemu yake.

“Sikufika kwenye kila ndoto niliyokuwa nayo, lakini nilifika sehemu ambayo watu wengi wamekuwa wakiiota bila kuifikia,” anasema.

MBOG 01

NAFASI YA VIJANA

Akimalizia mazungumzo, Mbogo anasema kizazi cha sasa kina bahati kubwa kuliko kile walichokulia wao.

“Sasa hivi mpira unalipa kweli. Kuna wachezaji wanalipwa mamia ya mamilioni ya shilingi,” anasema.

Anawataja wachezaji kama Mbwana Samatta na Simon Msuva kuwa mifano ya namna soka lilivyobadilisha maisha ya Watanzania.

“Zamani hata ukisajiliwa watu walikuwa hawajui umepata kiasi gani. Leo kila kitu kiko wazi.”

Lakini pamoja na fursa hizo zote, anawataka vijana wasiishi kwa mazoea.

Anatabasamu kidogo kabla ya kumalizia mazungumzo yetu kwa sentensi ambayo inaonekana ndiyo falsafa yake ya maisha.

“Mpira umenilipa kwa kiwango chake. Leo na mimi nataka nirejeshe kwa kuwalea watoto. Nikiona mmoja wao anafika mbali kuliko nilipofika mimi, nitajiona nimefanikiwa zaidi.”