Kagera Sugar namba ngumu, lakini ipo

Muktasari:
- Hivi karibuni Kagera chini ya Kaseja kwenye mechi mbili za ligi imefufua matumaini ya kusalia Ligi Kuu ikishinda mechi mbili mfululizo dhidi ya Pamba Jiji 2-1 na Coastal Union 2-1.
ZIMEBAKI mechi sita za kujitetea kwa timu ambazo hazipo kwenye nafasi nzuri kuepuka kushuka daraja katika Kuu Bara msimu huu huku takwimu zikionyesha zina kazi kubwa ya kufanya.
Kagera Sugar iliyopo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kucheza mechi 24 ikikusanya pointi 22 chini ya kocha Juma Kaseja ina kibarua cha kupambana ili kuepuka kushuka daraja kutokana na mambo yalivyo kwa upande wao msimu huu licha ya mabadiliko makubwa chini ya kocha huyo.
Hivi karibuni Kagera chini ya Kaseja kwenye mechi mbili za ligi imefufua matumaini ya kusalia Ligi Kuu ikishinda mechi mbili mfululizo dhidi ya Pamba Jiji 2-1 na Coastal Union 2-1.
Matokeo hayo yamefufua matumaini kwa timu hiyo iliyobakiza mechi sita ili kumaliza msimu ikiwa imeiacha kwa pointi nne Tanzania Prisons ambayo inaifukuzia ikiwa katika nafasi ya 15 na pia imeiacha kwa pointi sita KenGold ambayo inaburuza mkiani ikiwa na pointi 16.
Kwa sasa Kagera imesaliwa na mechi sita za kuamua hatma yake ya kuendelea kuwapo Ligi Kuu kwa msimu ujao au kuwafuata ‘ndugu’ zao Mtibwa Sugar ambao walishuka msimu uliopita baada ya kudumu katika ligi hiyo tangu ilipopanda daraja mwaka 1996 na sasa wanapambana kurudi wakibakiza pointi tisa tu.
Kagera ilipanda daraja mwaka 2005, ina miaka 20 bila kushuka daraja na sasa ina kibarua cha kupata matokeo mazuri ili kuendelea kubaki katika ligi hiyo ya juu zaidi kwa ngazi ya klabu nchini.
Kagera imenolewa na makocha watatu msimu huu ikianza na Paul Nkata aliyemuachia mikoba Mmarekani Melis Medo na sasa ipo chini ya aliyekuwa kocha wao wa makipa na mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga, Kaseja.
Kagera hii msimu wa 2016-17 ilikaribia kidogo kushangaza mashabiki kwa kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo, nafasi bora zaidi kwa mabingwa hao wa zamani wa Kombe la Tusker 2006, walipoifunga Simba kwa mabao 2-1 katika fainali Agosti 20, 2006 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).

MSIMU WA 2023/24
Kagera ilimaliza katika nafasi ya 10 katika mechi 30 baada ya kushinda saba, sare 13, kupoteza 10, ikikusanya pointi 34, mabao ya kufungwa 32 ya kufunga 23.
Hivyo kutokana na matokeo waliyoyapata msimu uliopita na sasa ni wazi kuwa Kagera Sugar imeporomoka kiwango kutokana na msimu huu kujitafuta ikipambana kubaki katika Ligi Kuu msimu ujao kwani msimu huu kwenye mechi 25 walizocheza hadi sasa wamekusanya pointi 22 ambazo ni pointi nane pungufu ya ilizovuna kwenye mechi kama hizo msimu ulioisha iliokusanya pointi 30.
Kwenye mechi tano zilizobaki endapo wakapata matokeo zote watapata pointi 15 ukiongeza 22 walizonazo sasa watakuwa na pointi 37 watamaliza nafasi ya saba endapo timu zilizo juu yake zitafungwa mechi zote.
Wanachokipitia sasa ni sawa na msimu wa 2018/19 ambapo timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya 18 kati ya timu 20 zilizokuwa zinashiriki ligi huku Stand United na African Lyon zikishuka daraja.

PETER LWASA
Huyu ndiye mchezaji ambaye anaibeba timu hiyo hasa eneo la ushambuliaji kwani hadi sasa ametupia kambani mara nane kati ya mabao 20 yaliyofungwa na timu hiyo yeye ndiye kinara huku kwenye msimamo wa wachezaji waliofunga mabao mengi akishika nafasi ya tano akiachwa nyuma mabao manne na kinara Charles Ahoua ambaye amefunga 12.
Mshambuliaji huyo kutoka Uganda amevuka rekodi ya mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo ambaye kwa sasa anakipiga KenGold, Obrey Chirwa aliyefunga mabao matano msimu uliopita akiwa na Kagera Sugar.

MECHI SITA ZA KUAMUA
Kagera imesaliwa na mechi sita za kuamua hatma yake ya kubaki Ligi Kuu ambazo kama itashindwa kuzitumia vyema itakula kwao ikiwamo ijayo dhidi ya Tanzania Prisons timu ambayo inachuana nayo kuhakikisha inabaki msimu ujao kabla ya kuvaana na Dodoma Jiji, Azam FC, Mashujaa, Namungo na ile ya mwisho dhidi ya Simba.
Katika mechi hizo, Kagera itacheza mbili nyumbani na zilizosalia zitakuwa za ugenini ikiwamo hiyo ya Simba ambayo inapambana kutwaa taji msimu huu mchezo utapigwa kwenye Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam.

MSIKIE KOCHA, NAHODHA
Kocha Kaseja anasema hakuna kinachoshindikana wanaamini kila kitu kinatokea kwasababu na wanapitia changamoto hiyo ya kupambania nafasi kwasababu hawakuwa na mwanzo mzuri, lakini sasa wanapambana na wanaamini mambo yatakwenda vizuri.
“Nimeaminiwa nimepewa timu, nataka kutumia nafasi hii kuhakikisha nakuwa sehemu ya kuacha alama kwa kuibakiza Kagera Sugar kucheza ligi msimu ujao. Mipango inaenda vizuri na wachezaji wameahidi kuipambania timu,” anasema na kuongeza;
“Ligi ya Tanzania ni ngumu inayohitaji mipango madhubuti kwa kila klabu hasa mzunguko wa pili ambao unakuwa wa kutimiza malengo, hatujachelewa, tuna nafasi ya kusawazisha makosa tuliyoyafanya kwenye michezo iliyopita;

“Pongezi nyingi ziende kwa wachezaji wangu nafurahishwa na kila wanachokifanya wanapambana kwa moyo kuibakisha Kagera Ligi Kuu msimu ujao, hili linawezekana kwa umoja wetu na namna ambavyo wamekuwa wakivuja jasho.
“Nimefanya kazi na Kagera Sugar nikiwa kocha wa makipa kwa muda lakini pia kuna baadhi ya wachezaji nimecheza nao ligi moja nilipokuwa mchezaji. Kitendo cha viongozi kunipa hii timu ni heshima kwangu lakini pia kwa wachezaji ambao wananifahamu hivyo tunazungumza na kukubaliana nini tufanye.”
Nahodha wa Kagera Sugar, David Ondit anasema wapo kwenye kipindi kigumu sana lakini wanapambana kuhakikisha hawaingii kwenye rekodi mbaya ya kuishusha daraja timu ambayo imehudumu miaka 20 kwenye ligi na wanaamini wanaweza.
“Hakuna asiyefahamu kuwa tunapitia magumu, sisi kama wachezaji vikao haviishi kujiuliza wapi tunakosea, tunamshukuru kocha Kaseja kwa kutuongoza kama kiongozi na sio kocha tu, amekuja kurejesha morali na kuaminisha viongozi na wana Kagera kuwa tupo tayari kuipambania timu hii,” anasema.
“Sio rahisi lakini hakuna kinachoshindikana tupo tayari kuipambania timu na tupo kwenye morali nzuri chini ya kocha ambaye ni kiongozi mzuri kwetu, tunaomba ushirikiano kutoka kwa mashabiki na viongozi ili kuweza kufikia malengo.”