TOP 10: Usajili wao WPL umejibu

Muktasari:
- Katika mapambano hayo ya kumaliza ligi, zipo timu zimefanya vizuri kutokana na mchango wa nyota waliosajiliwa na vikosi hivyo dirisha dogo na wamefanya makubwa.
HADI sasa katika Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) zimesalia raundi nne kukamilisha msimu wa 2024/25 na kuna timu zimeshajua hatma zao kwenye msimamo na nyingine zinapambana kujieweka pazuri.
Katika mapambano hayo ya kumaliza ligi, zipo timu zimefanya vizuri kutokana na mchango wa nyota waliosajiliwa na vikosi hivyo dirisha dogo na wamefanya makubwa.
Timu kama Yanga Princess, iliongeza nyota watano, Simba Queens, JKT Queens mchezaji mmoja mmoja na wote wameonyesha kiwango bora ndani ya muda mfupi.
Kwa kuzingatia kile walichokionyesha wachezaji hao ndani ya siku chache, Mwanaspoti imekuchambulia baadhi yao.

JEANINNE MUKAYISENGA (YANGA)
Kwa sasa ndiye mshambuliaji tegemeo kwenye kikosi cha Yanga Princess akitokea Rayon Sports Women ya Rwanda.
Tangu asajiliwe amecheza mechi nne na kufunga mabao manne na asisti moja wastani wa kufunga bao moja kila mchezo.
Mechi ya kwanza alifunga mabao mawili dhidi ya Alliance Girls, Yanga ikiondoka na ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Bunda Queens, Mashujaa Queens na Simba Queens akifunga bao moja.
Nyota huyo alisajiliwa kuziba nafasi ya Ariet Udong ambaye alipata majeraha ya goti ambayo yangemweka nje kwa takriban mwezi mmoja.
Lakini usajili huo ni kama umewalipa Yanga ambao walikuwa na wasiwasi kumkosa mshambuliaji wao hatari, Udong aliyefunga mabao matatu hadi sasa.

TANTINE NTUMBA (CEASIAA QUEENS)
Mkongomani huyo ndiyo msimu wake wa kwanza kucheza ligi ya Tanzania akitokea DRC Congo na tayari ameonyesha kiwango bora.
Kwenye mechi nne alizocheza amefunga mabao mawili na asisti tatu jambo ambalo hapo awali mastraika wa timu hiyo hawakufunga mabao hayo.

LYDIA AKOTH (YANGA)
Ni miongoni mwa wachezaji ambao wameingia diridsha dogo lakini ameonyesha kiwango kikubwa kiasi cha kuaminiwa na kocha wa timu hiyo, Edna Lema na amekuwa akimpa nafasi mara kwa mara.
Akoth ana uwezo wa kucheza nafasi zote za kiungo na hapo awali Yanga ilikuwa inapitia changamoto ya kukosa huduma ya kiungo mshambuliaji lakini tangu ametua jangwani ni kama amerahisisha mambo.
Mkenya huyo alisajiliwa na Yanga Princess kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Kenya Police Bullets ya nchini kwao.
Alikuwa kiungo muhimu kwenye timu hiyo ambayo msimu wake wa kwanza aliisadia kuchukua ubingwa likiwa taji la kwanza kwa timu hiyo akifunga mabao nane na asisti 10 kwenye mechi 18.
Kiwango alichoonyesha kilimfanya anyakue tuzo ya mchezaji bora wa mwaka (MVP) mbele ya Maximilla Robie wa Kibera Queens na Rebecca Okwaro anayekipiga timu moja.
ELIZABETH CHENGE (JKT QUEENS)
Hakucheza muda mrefu Ligi Kuu ya Wanawake, msimu wake wa kwanza ilikuwa 2022/23 akipata muda mchache wa kucheza kwenye kikosi ncha Alliance Girls wakati huo chini ya kocha Ezekiel Chobanka.
Msimu uliofuata akapandishwa kutoka kwenye kikosi cha vijana hadi kikosi cha kwanza akakabidhiwa unahodha msaidizi kusaidia na Anita Adongo.
Msimu uliopita alicheza mechi 18 akiwa miongoni mwa wachezaji wachanga wakutegemewa katika kikosi hicho kilichomaliza nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi.
Mwanzoni mwa msimu huu kiungo huyo aliendelea kuonyesa kiwango chake na dirisha dogo, JKT ilimsajili kwa makubaliano na Alliance ambayo hayakuwekwa wazi.
Pamoja na ubora wa viungo wa timu hiyo lakini kinda huyo (17) aliingia moja kwa moja kwenye kikosi cha JKT na kuonyesha kiwango bora.
Ubora alioendelea kuuonyesha kwenye mechi mbili tu alizocheza kilimshawishi kocha wa kikosi cha taifa ‘Twiga Stars’, Bakari Shime kumjumuisha kwenye mashindano ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake.
Hakuishia kuitwa tu lakini nyota huyo alianza kwenye kikosi hicho kilichokuwa kinatafuta matokeo ya kufuzu dhidi ya Ikweta ya Guinea.
WILFRIDA CEDAR (SIMBA)
Kipa huyo raia wa Kenya alisajiliwa na Simba dirisha dogo akitokea Gets Program ambako alivunja mkataba wake kutokana na changamoto ilizokuwa inapitia timu hiyo.
Simba alisajiliwa kama mbadala wa Mkenya mwenzake, Carolyne Rufaa aliyepata jeraha la goti ambalo litamuweka nje ya uwanja kwa msimu mzima.
Rufaa alikuwa kipa tegemeo wa Simba msimu uliopita aliisaidia timu hiyo kuchukua ubingwa wa ligi, ngao ya jamii akinyakua tuzo ya kipa bora wa mwaka.
Mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Yanga Princess akiruhusu bao 1-0 lakini alionyesha kiwango bora akichomoa mashuti makali matano yaliyolenga lango lake.
Hata hivyo, eneo analocheza anakumbana na changamoto ya namba kikosini kwani kuna Janet Shija ambaye amecheza mechi 12 na Gelwa Yona muda mwingi anasalia benchi.
AREGASH KALSA (YANGA)
Kwa sasa ndiye supastaa wa Yanga baada ya Precious Christopher kutimkia Simba msimu huu.
Aregash alitambulishwa kikosini hapo dirisha dogo akitokea C.B.E ya nchini kwao Ethiopia ambako aliisaidia timu hiyo kuchukua ubingwa wa CECAFA.
Alitazamwa kuja kurithi nafasi ya Precious ambaye alikuwa na misimu bora jangwani na kweli ameziba pengo hilo kwani ndani ya mechi tatu tu amethibitisha ubora.
Kiungo huyo mshambuliaji ambaye pia anamudu kucheza nafasi ya winga zote mbili hadi sasa amecheza mechi tatu akifunga bao moja na asisti mbili.
Faida kubwa aliyokuwa nayo mrembo huyo anatumia mguu wa kushoto kama ilivyo kwa staa wa Yanga, Aziz KI ambaye amekuwa akivutiwa na uwezo na uchezaji wa mwanadada huyo.

PROTASIA MBUNDA (YANGA)
Ndiyo chaguo la kwanza la Kocha Edna kwenye eneo la ulinzi wa pembeni lakini anamudu pia kucheza kama kiungo na beki wa kati.
Alipita klabu kama Panama, Evergreen, Ruvuma Queens, Fountain Gate Princess na Get Program ambako kote alionesha kiwango bora.
Ubora alionyesha umemfanya aingie kwenye kikosi cha timu hiyo moja kwa moja na kuwaweka benchi wazawa wanaocheza eneo hilo, Wema Maile na Silvia Mwacha.
DIANA MNALLY (YANGA)
Aliwahi kupita Simba kabla ya kujiunga na Yanga dirisha dogo akitokea Gets Program iliyopo nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi.
Aliondoka Simba baada ya kukutana na ushindani wa namba kwenye kikosi hicho eneo ambalo anacheza Fatuma Issa ‘Fetty Densa’.