Kombe la Dunia la Klabu, Mamelodi Sundowns sio kinyonge

Muktasari:
- Katika mashindano ambayo timu nne kutoka Afrika ambazo ni pamoja na Wydad Casablanca yenye Mtanzania Seleman Mwalimu, Al Ahly, Esperance de Tunis na Memelodi Sundown zilizishiriki kabla ya mchezo wa mwisho wa Wydad, timu pekee iliyofanya vizuri katika hatua ya makundi ni Mamelodi ambayo imeaga ikiwa na pointi nne.
BAADA ya Mamelodi Sundown kutoka sare jana dhidi Flamengo ya Brazil, rasmi timu zote za Afrika zimeondoshwa katika mashindano ya Kombe la Dunia la klabu yanayoendelea huko Marekani.
Katika mashindano ambayo timu nne kutoka Afrika ambazo ni pamoja na Wydad Casablanca yenye Mtanzania Seleman Mwalimu, Al Ahly, Esperance de Tunis na Memelodi Sundown zilizishiriki kabla ya mchezo wa mwisho wa Wydad, timu pekee iliyofanya vizuri katika hatua ya makundi ni Mamelodi ambayo imeaga ikiwa na pointi nne.
Hata hivyo, licha ya kufanya vibaya katika michuano hii, bado timu hizi nne zimeondoka kifua mbele kutokana na kiasi kikubwa cha pesa zilizovuna.
Kwanza kabisa zimepata pesa kutokana na ushiriki wao ambao kwa mujibu wa FIFA kila timu kutoka Afrika imejikunjia dola 9.55 milioni.
Kiasi hicho cha pesa kimeizidi mara mbili zawadi ambayo inaipata timu bingwa wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ni dola 4 milioni.
Vilevile kiasi hicho cha pesa ni mara tano ya pesa ambazo bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika anazipata ambazo ni dola 2 milioni.
Hapa chini tumekuweka mchanganuo wa kiasi ambacho kila timu ya Afrika imekipata kutokana na ushiriki na matokeo yake ya uwanjani.

AL AHLY
Mabingwa hawa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Afrika, wameishia hatua ya makundi ya michuano hii wakiwa nafasi ya mwisho katika kundi lao baada ya kupata alama mbili tu.
Ahly ambayo ilikuwa kundi A ikiwa na Inter Miami, Palmeiras na FC Porto, licha ya kumaliza ya mwisho imekunja jumla ya dola 11.5 milioni kwani mbali na pesa ya ushiriki pia kwa kila sare waliyoitoa walikunja dola 1 milioni.
Wababe hawa kutoka Misri licha ya kufeli mwaka huu, ni miongoni mwa timu zenye historia nzuri na michuano hii kwani tangu ianze kushiriki mwaka 2005, imeishia nafasi ya mshindi wa tatu mara tatu ambazo ni mwaka 2006, 2020 na 2021.

ESPERANCE
Vigogo hawa wa Tunisia pia wameishia hatua ya makundi wakishika nafasi ya tatu kwa pointi tatu ambazo walizipata baada ya kuichapa Los Angeles FC bao 1-0.
Esperance pia imechukua kiasi sawa na Ahly cha dola 11.5 milioni baada ya kulipwa dola 2 milioni kutokana na ushindi wao pekee katika hatua hiyo.
Michuano ya mwaka huu ilikuwa ni mwendelezo wa Esperance kutofanya vizuri katika mashindano haya kwani mara tatu za hapo awali ilizowahi kushiriki mwaka 2011, 2018 na 2019 zote iliishia katika hatua za awali.

MAMELODI SUNDOWNS
Mamelodi ndio timu kutoka Afrika iliyovuna pesa na pointi nyingi zaidi kuliko timu yoyote. Masawandawana walihitaji ushindi katika mechi yao dhidi ya Fluminense ili kuvuka kwenda hatua inayofuata ya 16 bora lakini hawakufanikiwa.
Imemaliza kundi ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi nne wakati Fluminense ikitinga hatua ya 16 bora kwa pointi tano.
Mamelodi imekunja jumla ya dola 12.5 milioni kwa sababu ilipata sare moja ya juzi dhidi ya Fluminense ambayo ni sawa na dola 1 milioni pia ikakunja dola 2 milioni kutokana na ushindi dhidi ya Ulsan HD.
Kiasi hicho cha pesa ni mara tatu ya kile ambacho bingwa wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika anakipata pia ni mara sita ya pesa ambazo bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika anapata.
Hii ni mara ya pili kwa Mamelodi kushiriki michuano hii na imeonyesha kuwa timu iliyofanya vizuri kutoka Afrika.

WYDAD CASABLANCA
Kabla ya mchezo wake wa mwisho dhidi ya Al Ain, Wydad ndio ilikuwa timu pekee kutoka Afrika ambayo haijapata hata pointi moja katika michuano hii.
Hata hivyo, licha ya kutopata pointi, bado ina mkwanja wa kutosha katika akaunti yake kwani imezawadiwa dola 9.5 milioni kutokana na ushiriki wao.
Wydad pia iliendeleza rekodi mbaya katika michuano hii kama ilivyokuwa kwa Esperance kwani katika mechi mara mbili ilizoshiriki ambazo ni 2017 na 2023 zote iliishia hatua za awali.