Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ulipo mtego wa wagombea uchaguzi mkuu TFF

Muktasari:

  • Zoezi hilo la kuweka na kupokea pingamizi linawahusu wagombea 25 na sita upande wa Urais na 19 Ujumbe Kamati ya Utendaji.

KALENDA ya Uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inaonyesha sasa tupo kwenye kipindi cha kuweka na kupokea pingamizi kwa wagombea, zoezi hilo limeanza Juni 26 na tamati yake Juni 28, 2025 saa 10:00 jioni.

Zoezi hilo la kuweka na kupokea pingamizi linawahusu wagombea 25 na sita upande wa Urais na 19 Ujumbe Kamati ya Utendaji.

Taarifa iliyotolewa Juni 24, 2025 na Makamu Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi TFF, Wakili Benjamin Kalume, iliwataja wagombea wote 25 wanaowania nafasi ya uongozi kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Agosti 16, mwaka huu jijini Tanga.

Nafasi ya Urais kuna wagombea sita ambao ni Ally Mayay Tembele, Ally Thabit Mbingo, Mbette Mshindo Msolla, Mustapha Salumu Himba, Shija Richard Shija na Wallace John Karia ambaye anatetea nafasi yake.

Upande wa wajumbe kamati ya utendaji, kuna wagombea 19 kutoka kanda tofauti ambao ni CPA Hosseah Hopaje Lugano (Kanda Namba Moja), Cyprian Charles Kuyava (Kanda Namba Tatu), Evance Gerald Mgeusa (Kanda Namba Tatu), Issa Mrisho Bukuku (Kanda Namba Sita), James Patrick Mhagama (Kanda Namba Tatu), Khalid Abdallah Mohamed (Kanda Namba Mbili), Lameck Nyambaya (Kanda Namba Moja), Martin Kibua Sekisasa (Kanda Namba Mbili) na Mohamed Omar Aden (Kanda Namba Nne).

Wengine ni Ally Omary Msigwa, DR David Cleopa Msuya, DR Yono Stanley Kevela, Juvenalius Pius Rugambwa, Maanya Juma Maanya, Robert Bundala Kajuba, Rocky Raymund Mgeju, Saleh Alawi Abdulllah, Salum Alli Kulunge na Vedastus Kalwizira Lufano.

Katika uchaguzi huo, wapigakura watatoka kwenye kanda sita kisoka ambazo ni Kanda Namba Moja inayohusisha mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Morogoro na Pwani, huku Kanda Namba Mbili ni mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga, wakati Kanda Namba Tatu ikiwa na mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songwe.

Kwa upande wa Kanda Namba Nne ni mikoa ya Dodoma, Simiyu na Singida ilhali Kanda Namba Tano ina mikoa ya Geita, Mara, Mwanza na Kagera.

Pia Kanda Namba Sita ina mikoa ya Katavi, Kigoma, Rukwa na Tabora.

Kwenye uchaguzi huo kuna nafasi saba zinazowaniwa ikiwamo moja ya urais na sita za wajumbe wa Kamati ya Utendaji na zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu lilianza Juni 16, 2025 na kuhitimishwa Juni 20, 2025.


Mtego upo hapa

Kanuni ya Uchaguzi ya Mwaka 2021 Ibara ya 10 (3-4) inaeleza kuwa mgombea wa urais wa TFF lazima awe na barua tano za udhamini kutoka kwa wanachama wa TFF, huku kwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka kanda lazima awe na barua ya udhamini kutoka chama cha soka cha mkoa husika.

Inaongeza, mwanachama hapaswi kumdhamini mgombea zaidi ya mmoja kwa nafasi moja vinginevyo udhamini wote utakuwa batili.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo wanaotoa uidhinishaji kwa wagombea ni 47 ambao mchanganuo wake upo hivi; vyama vya soka vya mikoa (FA) vyenye wajumbe 26, klabu za Ligi Kuu Bara (16), huku Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA), Chama cha Madaktari wa Michezo (TSMA), Chama cha Wachezaji (SPUTANZA) na Chama cha Soka la Wanawake (TWFA) kila kimoja kikiwa na mjumbe mmoja.

Pia Kifungu cha 9 inayoainisha Vigezo vya mgombea, inafafanua mambo tisa ambayo kama hujatimiza hivyo, basi umenasa kwenye mtego wa kuenguliwa kikifika kipindi cha usaili ambacho kitafanyika kwa siku tatu kuanzia Julai 1 hadi 3.

Kifungu hicho kinasema mtu yeyote anayetaka kugombea nafasi yoyote katika Shirikisho lazima atimize masharti yafuatayo:

1. Awe raia wa Tanzania;

2. Awe na sifa za kielimu angalau Kidato cha Nne na mwenye cheti cha kuhitimu elimu ya sekondari;

3. Awe na uzoefu wa angalau miaka mitano (5) unaothibitishwa katika uongozi wa soka;

4. Awe hajawahi kupatikana na hatia ya kosa la jinai na kuhukumiwa kifungo jela bila fursa ya kulipa faini;

5. Awe na umri wa angalau miaka 25;

6. Awe amewahi kucheza mpira, kuwa kocha, mwamuzi au kushiriki katika uongozi wa mpira wa miguu angalau katika ngazi ya Mkoa, Ligi Daraja la Kwanza au Ligi Daraja la Pili kwa kipindi kisichopungua miaka mitano;

7. Awe na uadilifu, kiwango cha juu cha uaminifu na uwezo wa kutekeleza majukumu na malengo ya TFF;

8. Mgombea wa nafasi ya Rais wa TFF lazima awe na sifa za chini za kielimu za Shahada ya Chuo Kikuu na awe na uwezo na haiba ya kuiwakilisha TFF ndani na nje ya nchi.

Ukipenya hapo, kuna kipengele cha MASHARTI YA MWISHO, Kifungu cha 26 kinazungumzia Ukiukwaji, Haki za FIFA, Uhifadhi wa Nyaraka, Mapungufu, ambapo chini kabisa inasema:

“Wakati wa mchakato wa uchaguzi, mtu yeyote au mwanachama atakayekiuka kanuni hii au kutoa taarifa za uongo kuhusu sifa au vielelezo vyake atapelekwa kwenye chombo husika cha TFF kwa hatua zaidi.”