Kompyuta yatabiri bingwa Kombe la Dunia
Muktasari:
- Mataifa 48 yatashiriki, mechi 104 zitachezwa, viwanja 16 vitatumika na mamilioni ya mashabiki wanatarajiwa kusafiri kutoka kila kona ya dunia kwenda Marekani, Canada na Mexico kushuhudia fainali hizo.
TEXAS, MAREKANI: TOFAUTI na fainali zilizopita za Kombe la Dunia, mwaka huu inaingia kwenye historia hata kabla ya kuanza kwa sababu ni mashindano yatakayokuwa na ukubwa ambao haujawahi kushuhudiwa.
Mataifa 48 yatashiriki, mechi 104 zitachezwa, viwanja 16 vitatumika na mamilioni ya mashabiki wanatarajiwa kusafiri kutoka kila kona ya dunia kwenda Marekani, Canada na Mexico kushuhudia fainali hizo.
Kuongezeka kwa idadi ya timu kunamaanisha kuwa mataifa mengi zaidi yana nafasi ya kuandika historia. Mataifa ambayo kwa miaka mingi yalikuwa yanatazama Kombe la Dunia kupitia televisheni sasa yamepata nafasi ya kushiriki moja kwa moja.
Cape Verde, Jordan, Uzbekistan na Curacao ni miongoni mwa mataifa yatakayocheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza. Kwao, kufuzu pekee tayari ni ushindi mkubwa lakini historia ya soka imeonyesha kuwa mara nyingi timu zinazoingia bila presha huwa na nafasi ya kufanya maajabu.
Kombe la Dunia limewahi kushuhudia maajabu mengi yaliyotikisa dunia. Mwaka 1950 Uruguay waliishtua Brazil mbele ya mashabiki zaidi ya 170,000 katika Uwanja wa Maracana. Mwaka 2002 Senegal waliinyoa Ufaransa katika mchezo wa ufunguzi. Mwaka 2022 Morocco walifika nusu fainali na kuwa taifa la kwanza kutoka Afrika kufanya hivyo.
Ndiyo maana hakuna anayethubutu kusema kuwa timu ndogo hazina nafasi.
MWAKA WA BINGWA MPYA?
Moja ya takwimu zinazovutia zaidi kutoka kwa Opta ni kwamba katika majaribio 10,000 yaliyofanywa na kompyuta yao maalumu kutabiri matokeo ya Kombe la Dunia 2026, asilimia 35.9 yalionyesha uwezekano wa taifa kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza katika historia.
Opta ni kampuni ya kimataifa inayokusanya, kuchambua na kutoa takwimu za michezo, hususan soka. Takwimu hiyo inaonyesha jinsi ushindani wa mwaka huu ulivyo mkubwa na kwamba kuna nafasi ya dunia kushuhudia bingwa mpya kabisa. Hii inaonyesha jinsi ushindani ulivyo mkubwa mwaka huu.
Katika historia ya Kombe la Dunia ni mataifa manane pekee yaliyowahi kutwaa ubingwa. Brazil, Ujerumani, Italia, Argentina, Ufaransa, Uruguay, Hispania na England ndiyo mataifa yaliyowahi kushika kombe hilo. Hata hivyo, mataifa kama Uholanzi, Ureno, Ubelgiji na Croatia yamewahi kufika fainali bila kutwaa ubingwa huo.
Uholanzi ndiyo timu iliyofika fainali mara nyingi zaidi, wamefika fainali tatu tofauti lakini kila mara waliondoka mikono mitupu.
Hali hiyo imeifanya Uholanzi kuwa moja ya timu zinazotajwa kuwa na deni kubwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia. Safari hii wanaongozwa na kizazi cha nyota wanaotaka kubadili historia hiyo.
NORWAY, KUSAPRAIZI?
Wakati wengi wakizungumza kuhusu Hispania, Ufaransa, England na Argentina, kuna taifa moja ambalo linaweza kutusapraizi ambalo ni Norway. Kwa miaka mingi taifa hilo lilikuwa halionekani katika mashindano makubwa lakini sasa lina moja ya safu kali zaidi za ushambuliaji duniani.
Erling Haaland alifunga mabao 16 katika mechi nane za kufuzu, rekodi iliyomfanya kuingia kwenye historia ya kufuzu Kombe la Dunia barani Ulaya. Martin Odegaard naye ameendelea kuwa mmoja wa viungo bora zaidi duniani. Mchanganyiko wa nyota hao wawili umeifanya Norway kupewa nafasi kubwa kuliko ilivyokuwa katika miaka mingi iliyopita.
Ikiwa watafanikiwa kuvuka hatua za awali, wanaweza kuwa miongoni mwa timu zitakazobadilisha kabisa mwelekeo wa mashindano.
MOROCCO NA NDOTO YA AFRIKA
Mwaka 2022 Morocco walifanya jambo ambalo kwa muda mrefu lilionekana haliwezekani. Walifika nusu fainali ya Kombe la Dunia. Walizifunga Ubelgiji, Hispania na Ureno kabla ya kusimamishwa na Ufaransa katika hatua ya nne bora. Safari hiyo ilibadilisha namna dunia inavyoitazama Afrika.
Kwa mara ya kwanza, watu wengi walianza kuamini taifa la Afrika linaweza kufika fainali na hata kutwaa Kombe la Dunia.
Morocco sasa hawana tena hadhi ya timu ya kushtukiza. Wanaingia kwenye mashindano haya kama moja ya timu zinazoheshimiwa zaidi duniani.
Achraf Hakimi anaendelea kuwa mmoja wa mabeki bora wa kulia duniani huku safu yao ya ulinzi ikisalia kuwa moja timu ngumu kufungika. Ikiwa kuna timu ya Afrika yenye nafasi ya kufanya jambo kubwa zaidi mwaka huu, basi Morocco ndiyo jina linalotajwa kwanza.
HUKU MESSI KULE CR7
Kwa zaidi ya miaka 20, soka la dunia limeongozwa na majina mawili. Lionel Messi na Cristiano Ronaldo (CR 7).
Wawili hao wamegawana Ballon d’Or nyingi, rekodi nyingi za mabao na mafanikio makubwa ya klabu kuliko wachezaji wengi waliowahi kutokea.
Kombe la Dunia 2026 linaweza kuwa mara ya mwisho kwa dunia kuwaona katika michuano hiyo mikubwa zaidi duniani.
Messi tayari ameshinda kila kitu kinachowezekana kushinda katika soka. Ronaldo bado anatafuta Kombe la Dunia ambalo ndilo taji kubwa pekee linalokosekana katika mkusanyiko wake. Iwapo Ureno watafika mbali, dunia inaweza kushuhudia moja ya hadithi kubwa zaidi katika historia ya michezo.
Lakini hata kama hawatafika mbali, ukweli kwamba Messi na Ronaldo watakuwa katika Kombe la Dunia lao la sita tayari ni historia ambayo inaweza kuchukua miaka mingi kuvunjwa.
KOMPYUTA SAHIHI?
Hili ndilo swali ambalo mashabiki wengi wa soka duniani wanaendelea kujiuliza kuelekea Kombe la Dunia 2026.
Kampuni ya takwimu za michezo ya Opta imeitaja Hispania kuwa timu yenye nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa kupitia mfumo wake wa kisasa wa uchambuzi unaojulikana kama Opta Supercomputer.
Mfumo huo ulifanya mahesabu ya maelfu ya matokeo yanayoweza kutokea katika mashindano hayo kwa kutumia takwimu za timu, viwango vya wachezaji, matokeo ya mechi zilizopita na mwenendo wa kila taifa katika miaka ya karibuni. Hata hivyo, pamoja na uwezo mkubwa wa teknolojia na takwimu hizo, historia ya soka imeonyesha mara nyingi kuwa mchezo huo hauchezwi kwenye kompyuta bali uwanjani. Takwimu zinaweza kutoa picha ya nani ana nafasi kubwa ya kushinda, lakini haziwezi kutabiri kila kitu kinachoweza kutokea ndani ya dakika 90 za mchezo. Presha ya mashindano, makosa ya kibinadamu, maamuzi ya waamuzi, majeraha ya ghafla na hata bahati vinaweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa mechi au mashindano yote.
MAAJABU YA SOKA
Kombe la Dunia limekuwa likitoa matokeo ambayo hayakutarajiwa mara kwa mara. Mwaka 2006, Italia waliingia kwenye mashindano bila kupewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa lakini waliibuka mabingwa baada ya kuifunga Ufaransa katika fainali.
Mwaka 2014, dunia ilishuhudia moja ya matokeo ya kushangaza zaidi katika historia ya soka wakati Ujerumani ilipoichapa Brazil mabao 7-1 katika nusu fainali mbele ya mashabiki wa Brazil, matokeo ambayo wachambuzi wengi hawakuyategemea.
Miaka minane baadaye, katika Kombe la Dunia la Qatar 2022, Saudi Arabia waliandika historia kwa kuifunga Argentina mabingwa watarajiwa kwa mabao 2-1 katika hatua ya makundi. Kabla ya mchezo huo, karibu kila utabiri uliipa Argentina ushindi lakini uhalisia wa uwanjani ulikuwa tofauti kabisa. Cha kushangaza zaidi ni kwamba Argentina walipona kutoka katika kipigo hicho na baadaye kutwaa ubingwa wa dunia, jambo lililoonyesha jinsi soka linavyoweza kubadilika ndani ya muda mfupi.