Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kulikuwa na Charles Hilary mmoja tu, mmoja tu...

HISIA Pict

Muktasari:

  • Sijui ugonjwa gani ulisababisha mauti yamkute katika kitanda kimoja cha Hospitali ya Mloganzila juzi Jumapili alfajiri, lakini ni wazi haikutokana na tabia zake binafsi za moyo na sura.

WALIODAI tusiwe na makasiriko katika maisha ili itusaidie kuondoa magonjwa yasiyo na ulazima inawezekana walikuwa sahihi. Na kama kweli walikuwa sahihi, basi mkongwe na nguli wa habari, Charles Hilary angeweza kuishi zaidi ya miaka 120 kwa namna ambavyo nafsi yake ilikuwa huru.

Sijui ugonjwa gani ulisababisha mauti yamkute katika kitanda kimoja cha Hospitali ya Mloganzila juzi Jumapili alfajiri, lakini ni wazi haikutokana na tabia zake binafsi za moyo na sura.

Charles alikuwa mtu wa aina yake. Mtu mwenye furaha, raha, utani na aliyekunjua moyo.

Ungeweza kuhisi hivyo kupitia sauti yake kabla hujakutana naye. Wakati ule akitangaza Redio Tanzania huku wengi wakiwa hawamfahamu kwa sura watu walijua na Charles alikuwa mtu mcheshi na anayemwaga burudani kwa kutangaza mpira. Alikuwa na ladha katika sauti yake ukizingatia alikuwa amekulia pia Zanzibar.

Alikuwa na sauti kali ambayo kwa lugha ya watangazaji wa sasa huwa inajulikana kama ‘punching’. Kuanzia katika kusoma taarifa ya habari hadi kutangaza mpira Charles alikuwa na sauti kali ya juu na yenye ladha, huku akibeba mizaha mingi yenye heshima ndani yake. Kulikuwa na Charles Hilary mmoja tu nchini.

Katika mpira ni yeye ndiye ambaye aliwapa wachezaji wengi majina ya utani. Ni yeye ambaye aligeuzwa kuwa ‘Azam TV’ kabla hata televisheni hazijaingia nchini. Angeweza kumuelezea Hamis Gaga kwa ufasaha na ukadhani unamtazama. “Hamis Gaga kama kawaida nywele zake hajachana, jezi yake hajachomekea na namuona anatembea kwa mikogo mbele ya mwamuzi Msafiri Mkeremi kutoka Tabora”. Huyo ndiye Charles halisi.

HILA 01

Angeweza kuelezea mandhari ya mechi kiasi ukajiona upo uwanjani. Angeelezea jezi za Simba, michirizi yake, rangi ya soksi na namna upepo unavyovuma kutoka Kaskazini kwenda Kusini. Ni yeye ndiye ambaye alikuwa anaingiza mbwembwe nyingi katika utangazaji. Mchezaji kuwa katika nafasi ya kuotea angesema: “Justine Mtekere amejenga kibanda bila ya idhini ya meneja wa Uwanja wa Taifa, Frank Macha.”

Charles Hilary alikuwa anakitendea haki kipaza sauti chake. Rafiki yangu, staa wa zamani wa Bandari Mtwara, Yanga na timu ya taifa, Ildephonce Amlima aliwahi kuniambia asingechaguliwa timu ya taifa kama Charles asingekipamba kipaji chake kupitia kipaza sauti wakati akitangaza mechi za Bandari Mtwara.

Utamu wa mechi ungeupata zaidi kama Charles angepangwa na Ahmed Jongo katika mechi za Ligi Kuu Bara wakati huo. Tatizo Jongo, ambaye naye ametangulia mbele ya haki alikuwa Yanga wa kutupwa, lakini Charles hakuwahi kujulikana alikuwa anashabikia timu gani kati ya Yanga na Simba. Hakuwa na mihemko.

Baadaye Charles alikuwa katika kundi la wakongwe wa RTD waliokwenda kuanzisha Radio One. Pale matangazo ya mpira yalikoma kidogo na Charles akajikita katika vipindi vingine. Na kwa sababu Radio One ilikwenda sambamba na kuanzishwa kwa Televisheni ya ITV, kwa mara ya kwanza watu wengi walipata kumjua Charles kwa sura.

HILA 02

Akaendesha vipindi mbalimbali kama Charanga Time. Akaendesha kipindi cha asubuhi huku akipokea simu. Hapa katika kupokea simu Charles alituburudisha zaidi kwanza kwa kutaka watu watamke jina lake kama Chaz Hilary na sio Charles Hilary. Angeweza kutumia sekunde 30 akibishana na msikilizaji namna ya kulitamka kwa usahihi jina lake huku akilazimisha aitwe Chaz.

Ilichekesha kidogo wakati alipokuwa analazimisha eneo aliloishi la Sinza lijulikane kama ‘Sinza kwa Chaz’ akijaribu kujenga heshima yake binafsi kama ambavyo ilitokea kwa Dk Remmy Ongala ambaye jina lake lilitengeneza eneo la Sinza kwa Remmy.

Baadaye Chaz alipata alichostahili kwenda kutangaza Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani kisha BBC London. Aliporudi nchini alijulikana zaidi kwa kutangaza taarifa ya habari ya Azam akiwa pembeni ya mrembo, Ivona Kamuntu. Hakuwahi kuacha masikhara na aliweka vibwagizo vyake kila alipopata nafasi mara baada ya taarifa ya habari kufika tamati. Mara ya mwisho kuonana na Chaz ilikuwa mwishoni mwa mwaka jana wakati aliponiita maeneo ya Hoteli ya Wanyama pale Sinza tulikuwa na maongezi binafsi akiwa tayari ni mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar.

Hata hivyo tulitumia dakika chache kuongea vitu vya msingi na baada ya hapo kilichofuata yalikuwa masikhara ya muda mrefu, huku tukipata kinywaji. Ndivyo alivyokuwa. Kuanzia hapo tuliongea zaidi kwa simu kwa sababu Chaz alikuwa anakerwa na namna watangazaji wa sasa na waandishi wanavyoikosea taaluma ya uandishi wa habari katika mambo kadha wa kadha. Alikerwa na matamashi ya watangazaji. Alikerwa na maandishi ya waandishi. Mimi ni miongoni mwa watu wake wachache wa kizazi kipya ambao aliwaamini katika kufikisha ujumbe.

HILA 03

Mara ya mwisho kuongea naye ilikuwa wakati wa mkutano mkuu wa CCM pale Dodoma. Tuliongea kwa simu akiwa Zanzibar kwa sababu nilishangazwa kutomwona Dodoma huku Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akiwa hapo. Alileta masikhara mengi na tukacheka. Hata hivyo aliniambia alikuwa hajisikii vizuri.

Asubuhi ya juzi nikiwa hapa Barcelona nilipokea habari ya msiba wa kaka Chaz na ilikuwa habari nzito kwa Watanzania wanaoshi nchini hapa. Mazungumzo ya siku nzima yalihusu msiba wa Chaz. Kila mtu alimwelezea alivyojisikia, lakini kilichotawala kuhusu yeye ni kipaji cha kutangaza na ucheshi alivyozaliwa navyo. Sasa nguli amelala usingizi wa milele. Chaz ni miongoni mwa Watanzania wachache katika fani zao ambao neno nguli au kwa Kiingereza legend linamstahili. Alikuwa nguli hasa. Kwa kile alichofanya hakuna mtangazaji ambaye unaweza kusema alirithi mikoba yake. Kulikuwa na Chaz Hilary mmoja tu. Hakukuwa na mwingine.

Mshairi mmoja wa Kiingereza aliwahi kusema ‘immortality lies not in the things you leave behind, but in the people your life has touched’.

Uzuri au urefu wa maisha yako haupimwi na vitu ulivyoacha, bali ni namna maisha yako yalivyowagusa watu. Chaz aligusa wengi. Mimi ni mmojawao.