Mbappe na rekodi ya kazi bure

Muktasari:
- Mbappe amekuwa mchezaji wa kwanza wa Real Madrid kufunga hat trick (mabao matatu) katika mechi moja ya El Clasico ya La Liga, ndani ya karne ya 21.
LICHA ya Real Madrid kupoteza mabao 4-3 kwa Barcelona katika pambano la El Clasico wikiendi iliyopita, lakini mchezaji wa timu hiyo, Kylian Mbappe ameweka rekodi ya klabu ambayo bila shaka mwenyewe hatajivunia kamwe.
Mbappe amekuwa mchezaji wa kwanza wa Real Madrid kufunga hat trick (mabao matatu) katika mechi moja ya El Clasico ya La Liga, ndani ya karne ya 21.
Mchezaji wa mwisho wa Real Madrid kufanya hivyo katika mechi moja ya El Clasico ya La Liga alikuwa ni Ivan Zamorano mwaka 1995.
Karim Benzema na Vinicius Jr pia wamewahi kufunga hat trick katika El Clasico, lakini haikuwa kwenye La Liga.
Benzema alifunga mwaka 2023 katika ushindi wa 4-1 kwenye Uwanja wa Camp Nou katika mechi ya mkondo wa pili ya fainali ya Kombe la Mfalme ambalo ni sawa na Kombe la Shirikisho (FA).
Vini Jr alifunga katika ushindi wa 4-1 kwenye fainali ya Ngao ya Jamii, mwaka 2024.

Kwa jumla, Mbappe anakuwa mchezaji wa 15 wa Real Madrid kufunga hat trick kwenye El Clasico, katika historia ya mechi hii ambayo imeshuhudia jumla hat trick 25.
Lakini tofauti na Mbappe, wenzake wote waliobaki walifunga hat trick na kuzisaidia timu kushinda mchezo wakati Mbappe ameishia kupoteza.
Hii ni bahati mbaya kwake hasa ukirejea kilichotokea kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar kati ya Argentina na Ufaransa.
Mbappe alifunga hat trick na kuwa mchezaji wa kwanza kufanya hivyo ndani ya karne ya 21 na wa pili kihistoria baada ya Sir Geoff Hurst wa England.
Hurst alifunga hat trick katika Fainali ya Kombe la Dunia 1966 na kuisaidia timu yake kushinda 4-2 dhidi ya iliyokuwa Ujerumani Magharibi. Lakini Mbappe hat trick yake haikuwa na maana kwani timu yake iliishia kupoteza kwa mikwaju 4-2 ya penalti baada ya sare ya 3-3 katika dakika 120 za mchezo.
Baada ya mechi ile, yeye mwenyewe alinukuliwa akisema ni bora asingefunga hata bao moja, lakini timu yake ishinde Kombe la Dunia kuliko kufunga hat trick halafu kuishia kupoteza.

Hicho ndicho kilichomkuta safari hii - kafunga hat trick, lakini akaishia kuchezea kichapo.
Hata hivyo, Mbappe anakuwa mchezaji wa pili kufunga hat trick dhidi ya Barcelona na kuishia kupoteza mchezo.
Mchezaji wa kwanza alikuwa Milinko Pantic wa Atletico Madrid aliyefunga kwenye mkondo wa pili wa robo fainali ya Kombe la Mfalme 1997, lakini timu yake ikaishia kupoteza 5-4.
Hata hivyo, kwa Mbappe hii ni hat trick ya pili dhidi ya Barcelona. Ya kwanza alifunga 2021 katika mkondo wa kwanza wa 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakati huo akiwa PSG, Mbappe alikwenda Camp Nou na kuiangamiza Barcelona 4-1. Hat trick ya sasa ameifungia Uwanja wa Lluis Companys sio Camp Nou kwa sababu uwanja huo upo kwenye ukarabati.
Isingekuwa hivyo, bila shaka hii ingekuwa ni hat trick ya pili kwa nyota huyo kwenye Uwanja wa Camp Nou.

HAT TRICK ZA EL CLASICO
Kila mtu anajua uwanja wa nyumbani wa Real Madrid unaitwa Santiago Bernabeu, lakini ni wachache wanaojua kwa nini unaitwa hivyo.
Hilo ni jina la mtu muhimu katika historia ya klabu hiyo. Alikuwa mchezaji, akawa meneja wa timu, kocha na baadaye akawa rais wa klabu. Ndiye aliyejenga Uwanja wa Santiago Bernabeu - ule wa kwanza kabla ya huu mpya wa sasa uliojengwa na Florentino Perez.
Kwa heshima yake, uwanja ukapewa jina hilo.Hapo kabla ulikuwa unaitwa Chamartini kwa sababu upo katika eneo lenye jina hilo.
Sasa zaidi ya yote hayo, Santiago Bernabeu ndiye mchezaji wa kwanza katika historia ya El Clasico kufunga hat trick.
KAFANYA HIVYO MARA MBILI - MWAKA 1916
Ifuatayo katikati kwa ukurasa huu ni orodha ya wachezaji wote waliowahi kufunga hat trick kwenye El Clasico kutoka timu zote mbili yaani Real Madrid na Barcelona.