Majina ya kustaajabisha katika soka

Muktasari:
- Ni kweli yapo majina yenye chanzo chake katika mila na tamaduni na huwa na maana tofauti na ile ya lugha ya Kiswahili, lakini ukilisikia unashituka na unapotaka kulitumia ulimi hukataa kulitamka.
MARA nyingi tunaposikia yanatajwa baadhi ya majina ya watu hushangaa na kujiuliza kwa nini huyo mtu alipewa jina hilo ambalo tunaliona sio zuri, methali ya tusi au lenye viashiria vya udhalilishaji.
Ni kweli yapo majina yenye chanzo chake katika mila na tamaduni na huwa na maana tofauti na ile ya lugha ya Kiswahili, lakini ukilisikia unashituka na unapotaka kulitumia ulimi hukataa kulitamka.
Majina ya ajabu pia yapo kwa timu za kandanda katika nchi nyingi na leo nitayagusia machache.
Nilipokuwa Ghana mwaka 1975 na kufika katika nchi za jirani kwa kazi au matembezi nilikutana na majina ya aina hiyo na kushangaa sana. Nilipoulizia niliambiwa hakuna kanuni au sheria inayotaka majina ya timu za kandanda yawe vipi.
Ghana niligundua kuwepo klabu nyingi zenye majina ya aina hiyo. Kwa mfano katika mji wa Cape Coast ipo klabu inayoshiriki Ligi Kuu ambayo inaitwa Ebusua Dwarfs (Mbilikimo wa Ebusua).
Wengi wa watu hawa wapo Congo (karibu 90,000) na kama 200 katika milima iliyopo Brazil. Urefu wa watu hawa huwa ni wa kati ya futi 3 na inchi 10 na futi 4 na inchi 10.
Kilichonishangaza ni wengi wa wachezaji wa timu hiyo ya mji wa Cape Coast ambao wakazi wake wengi ni wa kabila la Fante walikuwa warefu zaidi kuliko wa makabila ya Ashanti, Gaa na Ewe.
Vile vile ipo timu inayoitwa Hasaacas, jina ambalo halipo katika msamiati wa watu wa nchi yote ile ya Afrika Magharibi. Nilipouliza niliamabiwa kwamba jina hilo liizuka mwaka 1931 pale kikundi cha wafanyakazi wa reli walipounda timu hiyo ya kandanda.
Watu hawa waliamua kuunganisha herufi za kwanza za majina yao kupata jina la timu. Kilichopatikana ni neno H.A.S.A.A.C.A.S. -- “ikimaanisha majina ya Hammond, Amua, Sakyi, Adotei, Allotey, Cann, Adotey na Sackey. Tumu nyengine ambayo inacheza Ligi Kuu ni Eleven Wise (Werevu 11) ya mji wa Sekondi-Takoradi uliopo magharibi ya nchi hiyo.
Timu nyingine zenye majina ya ajabu za Ghana ni pamoja na Kokomlemle Witch Doctors (Wachawi wa Kokomlele) Mankaoable Beautiful Herricane (Kimbunga Kizuri cha Makaoable) na God’s Ladies (Watoto wa kike wa Mungu).
Nchi jirani ya Nigeria ndio imetia fora kwa majina ya ajabu ya timu za kandanda. Huko zipo timu zenye majina kama Box 2 Box FC (Sanduku hadi Sanduku). Mashabiki wa timu hii hupenda wanapokwenda uwanjani kubeba masanduku.
Katika mji wa Ife-Ife ambapo watu wake wengi ni wa kabila la Yoruba ipo timu inaitwa No No No FC (Hapana Hapana Hapana).
Timu nyingine yenye jina la ajabu ni God Delivered Me Bible Church FC (Mungu Kanijaalia Kanisa la Biblia). Hii ipo katika mji wa Ogun, kusini magahribi mwa Nigeria.
Ukienda Gambia zipo timu zenye majina kama The Loyal Hooligans (Wahuni Watiifu) na Saint FC (Klabu ya Watakatifu). Gambia pia ipo timu inayoitwa We Die Here FC (Tutafia Hapa).
Botswana ipo timu inayoitwa Naughty Boys (Watoto Watundu) na ipo timu inaitwa Eleven Angels (Malaika 11).
Jina la timu ya soka ya Chuo Kikuu cha Glouccestershire, England, ni Egg Fried FC (Yai la Kukaanga) na huko Marekani timu ya chuo kimoja inaitwa How I Met Your Mother FC (Jinsi Nilivyokutana na Mama Yako) na timu nyingine iliyopo katika katika jiji la Atlanta la nchi hiyo inaitwa Sons of Pitches (Watoto wa Kiume wa Viraka vya Lami).
Katika Chuo Kikuu cha London nako ipo timu yenye jina la ajabu. Nalo ni Who Ate All the Depays (Nani Amekula Sadaka Yote).
Katika jiji la Nottingham Forest ipo timu inaitwa Chicken Tikka Masalah (Kuku wa Kuchoma).
Timu moja iliyopo Sussex, England inaitwa Earth and Wind FC (Ardhi na Upepo) na ipo inayoitwa Tea and Biscuits (Chai na Biskuti) ambayo iko Hispania.
Ukiachilia majina ya ajabu pia lipo jingine la kushangaza. Nalo ni jina la timu kuwa refu na ambalo mtu mwenye maradhi ya pumu litampa kazi kulitamka.
Kwa mfano, miaka kama 15 hivi iliyopita iliundwa timu Poland ambayo jina lake ni refu na imekuwa kazi pevu kuliandika katika tiketi ya mchezo. Timu hii ya daraja la tatu inaitwa Szczakowianka Jaworzno.
Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya majina ambayo ningependa wasomaji wafanye mazoezi au hata kushindana kuyatamka:
1. Genclerbirligi Spor Kulubu: Hii ni klabu ya Uturuki iliyoundwa 1923 na inashiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo.
2. Taumatawhatkatangihangakoauauotamateapokaiwhenuakitanatahu (hili ni neno moja). Klabu hii ambayo jina lake ndio refu kuliko la klabu ya mchezo mwingine wowote duniani ipo New Zealand. Jina hili linatokana na jina la mlima wenye urefu wa mita 305 uliopo katika nchi hiyo.
3. Clwb Pel Droed. Hiki ni kifupisho cha klabu inayoitwa: Llanfairpwllgwyngyllgogerychwyrndrobwllllantsiliogogogoch FC. Hii ni ya daraja la kwanza Wales.