Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo 6 Singida, Yanga zikicheza Dak 57

SINGIDA Pict

Muktasari:

  • Uwanja huu si tu utafaidisha Singida BS, bali pia utafungua milango kwa mashindano mengine kufanyika katika mkoa huo kama vile kuchezwa kwa Fainali ya Kombe la FA miaka michache ijayo.

UZINDUZI wa uwanja wa Singida BS ni tukio la kihistoria katika soka la Tanzania. Uwekezaji huu unaashiria maendeleo katika miundombinu ya michezo na ni hatua inayoweza kuwa chachu kwa klabu nyingine kufanya jambo kama hili.

Uwanja huu si tu utafaidisha Singida BS, bali pia utafungua milango kwa mashindano mengine kufanyika katika mkoa huo kama vile kuchezwa kwa Fainali ya Kombe la FA miaka michache ijayo.

Hapa kuna mambo muhimu yaliyojitokeza katika uzinduzi wa uwanja huo.


VIJEMBE KWA SIMBA, YANGA

Katika hafla hiyo, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Singida BS, Festo Sanga alitupa kijembe kwa klabu kongwe za Simba na Yanga.

Alisisitiza licha ya kuwa na zaidi ya miaka 70 katika soka la Tanzania, bado hawajajenga viwanja vyao vya mechi, huku Singida BS ikiwa na uwanja wake ndani ya muda mfupi.

Hii ni changamoto kwa klabu za Tanzania kuanza kuwekeza katika miundombinu yao badala ya kutegemea viwanja vya serikali au klabu nyingine kwa ajili ya michezo yao.

Kwa miaka mingi, Simba na Yanga wamekuwa wakitumia Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kama uwanja wao wa nyumbani. Ingawa uwanja huo una hadhi ya kimataifa, bado ni uwanja wa Serikali na hii inaonyesha miamba hiyo haijafanikiwa kuwekeza vya kutosha katika miundombinu yao wenyewe.

Uwekezaji wa Singida BS unaweza kuwa somo kwao na iwapo watachukua hatua, soka la Tanzania litazidi kukua.

SING 03

NAIBU WAZIRI

Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni, na Michezo, Hamisi Mwinjuma 'Mwana FA', aliwapongeza viongozi wa Singida BS kwa uamuzi wa kujenga uwanja wao na kuonyesha mfano kwa klabu nyingine. "Uwekezaji katika michezo haupaswi kuwa jukumu la Serikali pekee licha ya kufanya makubwa ndani ya miaka minne bali pia mashirika binafsi na wadau wa michezo kwa ujumla."

Mwana FA alisisitiza maendeleo ya soka nchini hayawezi kupatikana bila kuwa na miundombinu bora. Hii ni fursa kwa mikoa mingine kufuata nyayo za Singida BS na kuwekeza katika viwanja bora vya michezo. Kwa muda mrefu, Tanzania imekuwa ikitegemea viwanja vichache vyenye hadhi ya kimataifa, lakini juhudi kama hizi zinaweza kusaidia kupanua wigo wa maendeleo ya soka nchini.

SING 02

ENEO LA KUCHEZEA 

Moja ya vivutio vikubwa vya uwanja huu ni eneo lake la kuchezea, ambalo limewekewa mifereji maalum inayosaidia kuondoa maji na kuzuia maji kutuama. Katika siku ya uzinduzi, mvua kubwa ilinyesha lakini haikuathiri mchezo, jambo linalothibitisha ubora wa miundombinu ya uwanja huo.

Viwanja vingi vya Tanzania vimekuwa vikikumbwa na changamoto za mifereji mibovu, hali inayopelekea maji kutuama na kuharibu ubora wa michezo. Hali hii inasababisha mechi kuahirishwa au kuchezwa katika mazingira magumu. Uwanja wa Singida BS umeonyesha kuwa kwa uwekezaji mzuri, changamoto hizi zinaweza kuzuilika na hii ni hatua kubwa kwa soka la Tanzania.

SING 04

KINGO ZA UWANJA

Tofauti na viwanja vingi nchini, uwanja mpya wa Singida BS umewekewa kingo maalum zilizo na nyavu zinazozuia mashabiki kuingia eneo la kuchezea. Hili ni jambo la kipekee linaloongeza usalama na utulivu wakati wa mechi.

Katika viwanja vingine, mashabiki mara nyingi huingia uwanjani kwa hasira au furaha, jambo linaloweza kusababisha vurugu au kusimamisha mechi.

Usalama wa mashabiki na wachezaji ni jambo la msingi katika soka la kisasa, na uwanja wa Singida BS umeonyesha mfano mzuri wa jinsi ambavyo klabu zinaweza kuwekeza katika kuhakikisha michezo inachezwa kwa utulivu. Hili ni jambo ambalo viwanja vingine vya Tanzania vinapaswa kuiga ili kuhakikisha soka linaendelea kuchezwa katika mazingira salama.

SING 05

MECHI ILIVYOVUNJIKA

Mchezo wa ufunguzi kati ya Singida BS na Yanga SC haukuweza kumalizika kutokana na hali mbaya ya hewa. Upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa ulisababisha mchezo kuvunjika katika dakika ya 57, huku timu hizo zikiwa sare ya bao 1-1.

Hii ilionyesha changamoto za hali ya hewa ambazo zinaweza kuathiri michezo, hasa kwa viwanja ambavyo havina sehemu za kujikinga na mvua.

Licha ya changamoto hiyo, mechi hiyo ilithibitisha kuwa uwanja wa Singida BS una miundombinu imara, kwani mvua haikuathiri eneo la kuchezea. Hili ni jambo la kutia moyo na linaonyesha uwanja huu unaweza kutumika kwa hekaheka za Ligi Kuu Tanzania Bara.


CHANGAMOTO YA MAJUKWAA

Kuna changamoto ya kukamilisha majukwaa ya uwanja huo. Viongozi wa Singida BS wana jukumu kubwa la kuhakikisha uwanja huo unakamilika kwa asilimia 100 ili kuwapa mashabiki wao burudani bora zaidi. Kwa sasa, mashabiki wanaweza kuangalia mechi lakini uwanja unahitaji majukwaa ili kutoa huduma bora.

Ikiwa viongozi wa Singida BS watakamilisha majukwaa haya kwa wakati, uwanja huu unaweza kuwa moja ya viwanja bora nchini. Hii itaongeza hamasa kwa mashabiki, pia kufanya uwanja huu kuwa kivutio kwa timu zingine za ligi kutumia kwa mechi zao.