Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapumziko ya FIFA mtego Ligi Kuu

NONDO Pict


LIGI Kuu Tanzania Bara imeingia kwenye mapumziko mafupi kupisha kalenda ya FIFA ambapo timu za taifa zinaendelea na majukumu yao ya kimataifa kwa takribani wiki mbili kabla ya ligi kurejea Juni 12, 2026.


Msimu huu unatarajiwa kufungwa mwishoni mwa mwezi wa sita huku kila timu ikiwa imebakiwa na mechi tano za kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu hatma zao.


Ukiuangalia msimamo wa ligi kwa sasa unaweza kuona wazi kabisa kuwa ushindani umegawanyika katika mafungu matatu au manne tofauti, kila kundi likiwa na vita yake maalumu.

Hii ndiyo hatua ambayo presha huwa kubwa zaidi kwa wachezaji, makocha, viongozi na hata waamuzi kwa sababu kila pointi inakuwa na thamani kubwa kuliko ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu.

Kundi la kwanza ni lile la kuwania ubingwa wa ligi. Hapa kuna timu tatu ambazo kwa namna moja au nyingine ndizo zilizobaki kwenye mbio za ubingwa. Yanga inaongoza kwa alama 60 ikifuatiwa na Simba yenye alama 58 huku Azam ikiwa nafasi ya tatu na alama 52. Kiuhalisia timu nyingine zilizobaki kwenye ligi haziwezi tena kufikia alama za Yanga na Simba hata kama viongozi hao wa juu watapoteza mechi zao zote zilizobaki. Hivyo basi mbio za ubingwa zimebaki kuwa za timu hizi tatu pekee.

NOND 01

Yanga na Simba bado zinaonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi kutokana na uzoefu wao wa kushindania mataji katika mazingira yenye presha kubwa. Tofauti ya alama mbili kati yao inafanya kila mchezo uliobaki kuwa sawa na fainali.

Kwa upande wa Azam, bado wana nafasi ya kinadharia lakini wanahitaji miujiza pamoja na makosa mengi kutoka kwa wapinzani wao ili waweze kurudi kwenye mbio hizo kwa nguvu.

Kundi la pili ni lile la kuwania nafasi za juu kwenye msimamo, hasa ya nne ambayo inaweza kutoa ushiriki mashindano ya kimataifa au kuongeza heshima ya timu kumaliza msimu katika nafasi nzuri. Hapa ushindani ni mkubwa kati ya Singida Black Stars yenye alama 41, JKT Tanzania (alama 38) na TRA United (alama 37). Kiuhalisia nafasi ya tatu bado inaonekana kuwa mbali kidogo lakini nafasi ya nne bado ipo wazi kwa yeyote atakayekuwa na mwisho mzuri wa msimu.

NOND 02

Katika hatua hii tofauti ya pointi ni ndogo sana kiasi kwamba matokeo ya mchezo mmoja yanaweza kubadilisha kabisa msimamo. Timu ambazo zitakuwa na utulivu wa kiufundi na kisaikolojia ndizo zitakazofanikiwa kuhimili presha ya mwisho wa msimu.

Kundi la tatu na ambalo lina presha kubwa zaidi ni lile la kupambana kubaki ligi kuu. Ukiitoa KMC yenye alama 9 ambayo tayari inaonekana kama imekubali kushuka daraja na kucheza Championship msimu ujao, timu nyingi zilizobaki bado hazina uhakika wa kubaki salama. Kuanzia Tanzania Prisons hadi Dodoma Jiji, kila timu bado ipo kwenye hatari ya kushuka daraja kutegemea matokeo ya mechi zilizobaki.

Ni kweli baadhi yao wako karibu zaidi na mstari wa njano na mwekundu, jambo linaloongeza hofu na presha kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi. Katika mazingira kama haya mara nyingi tunaona mechi zikichezwa kwa tahadhari kubwa huku kila timu ikipambana kuokoa maisha yake ndani ya ligi.

Mapumziko haya ya FIFA yanaweza kuwa na athari chanya au hasi kwa timu tofauti kulingana na hali ambayo timu ilikuwa nayo kabla ya kusimama kwa ligi. Kwa mfano, kwa timu zilizokuwa kwenye mwendelezo mzuri wa matokeo, mapumziko yanaweza kuharibu kasi yao. Fountain Gate ni mfano mzuri wa timu ambayo ilianza kupata muunganiko mzuri na kuonyesha ushindani mkubwa kabla ya mapumziko haya. Ni sawa na gari ambalo lilikuwa limeanza kuchanganya vizuri baada ya kusukumwa halafu ghafla dereva akalizima.

Lakini kwa timu ambazo zilikuwa hazifanyi vizuri, mapumziko haya ni nafasi muhimu ya kurekebisha makosa. Makocha watapata muda wa kufanya tathmini ya timu zao, kurekebisha mbinu, kuimarisha saikolojia ya wachezaji na kutafuta njia bora ya kumaliza mizunguko iliyobaki kwa mafanikio.

NOND 03

Hata hivyo, hiki si kipindi cha maandalizi mapya kama ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu. Huu ni wakati wa kutunza kile ambacho tayari kipo ndani ya timu. Wachezaji wengi wana uchovu mkubwa wa mwili kutokana na msimu mrefu wenye mechi nyingi. Hivyo jukumu kubwa la makocha litakuwa kuhakikisha timu zao zinabaki kwenye kiwango kizuri cha utimamu bila kuwaongezea mzigo mkubwa wachezaji.

Kwa namna moja au nyingine, mwalimu atakayefanikiwa kutumia vizuri siku hizi chache za mapumziko ndiye atakayekuwa na nafasi nzuri ya kumaliza msimu kwa mafanikio. Hasa kwa timu ambazo hazitakuwa zimeathirika sana kwa kutoa wachezaji wengi kwenye timu za taifa.

Kwa kuwa sasa tumeingia kwenye kipindi cha uamuzi wa ubingwa pamoja na vita ya kuepuka kushuka daraja, ni muhimu kwa Bodi ya Ligi kuongeza umakini katika usimamizi wa mashindano haya. Lazima kuwe na ufuatiliaji mkubwa ili kuondoa uwezekano wa upangaji wa matokeo, hasa kwenye mechi zinazozihusisha timu ambazo tayari zimejihakikishia usalama dhidi ya zile zinazohitaji pointi za kujiokoa au kutwaa ubingwa.

Pia waamuzi wanapaswa kuongeza umakini mkubwa katika kusimamia sheria za mchezo. Makosa madogo yanaweza kuamua hatma ya timu katika kipindi hiki kigumu cha msimu. Usawa na haki ndani ya uwanja ndiyo vitakavyosaidia kupatikana bingwa anayestahili pamoja na timu zitakazoshuka daraja kwa haki.

Mwisho wa yote, mashabiki wa soka wanachosubiri sasa ni kuona nani ataonyesha uimara wa kweli kwenye mechi zilizobaki. Je, ubingwa utaenda upande gani? Ni timu zipi zitajinasua kwenye hatari ya kushuka? Na ni nani atakayemaliza msimu akiwa shujaa au mwathirika wa presha za mwisho wa ligi? Majibu yote tutayapata mwishoni mwa Juni wakati pazia la msimu litakapofungwa rasmi.