Prime
Uamuzi wa Yanga kujenga uwanja, hili lisisahaulike
TANZANIA kama zilivyo nchi nyingine zinazopiga hatua katika maendeleo ya soka, inapitia kipindi muhimu cha kuboresha mazingira ya mchezo huo kuanzia mifumo ya kuzalisha wachezaji, kuwajengea uwezo makocha na walimu wa soka, hadi kuboresha miundombinu ya msingi inayowezesha mchezo kufanyika kwa viwango bora.
Katika mambo hayo yote, kuna jambo moja ambalo ni la msingi sana lakini mara nyingi halipati uzito unaostahili uwepo wa viwanja bora vya kuchezea, ambavyo ndiyo msingi wa utekelezaji wa sheria namba moja ya mchezo wa soka.
Kwa kiasi kikubwa, Tanzania imebahatika kuwa na viwanja katika mikoa mingi vinavyoweza walau kupokea mashabiki 5,000 au zaidi.
Hili ni jambo la kujivunia kwa sababu linaonyesha kuwa kwa muda mrefu kulikuwepo jitihada za kuhakikisha mchezo wa soka unapata nafasi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Hata hivyo, changamoto kubwa iliyopo si uwepo wa viwanja pekee, bali ubora wake na uwezo wake wa kukidhi mahitaji ya kisasa ya mchezo.
Viwanja vingi vilivyojengwa miaka mingi iliyopita vina changamoto kwenye majukwaa ambayo mara nyingi hayakidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ajili ya kuandaa mechi za kimataifa.
Aidha, baadhi ya maeneo ya kuchezea nayo hayapo katika hali rafiki kwa mchezo wa ushindani wa kisasa.
Lakini pamoja na changamoto hizo, eneo la kuchezea linaweza kuboreshwa kwa gharama nafuu zaidi ukilinganisha na kujenga upya majukwaa au miundombinu mingine mikubwa.
Katika hali ya sasa, ni klabu chache tu nchini ambazo zinaweza kujivunia kuwa na viwanja vyao vinavyokidhi vigezo vilivyowekwa na TFF kwa ajili ya mechi za ligi kuu.
Miongoni mwa klabu hizo, Azam FC ndiyo iliyokuwa mfano wa kwanza wa kuonyesha njia baada ya kujenga uwanja wao wa kisasa uliokidhi mahitaji ya ligi na hata baadhi ya mechi za CAF.
Kwa muda mrefu, uwanja huo ulikuwa msaada mkubwa kwa timu nyingi za Dar es Salaam zilizokuwa zikikosa viwanja vya kutumia kwa mechi zao.
Baadaye, juhudi nyingine zilionekana pale Manispaa ya Kinondoni ilipojenga uwanja wake, huku JKT Tanzania na Singida Black Stars nazo zikifanya maboresho katika viwanja vyao.
Hata kabla ya hapo, Gwambina kule Misungwi walionesha mfano wa namna uwekezaji katika miundombinu ya soka unaweza kufanyika hata nje ya miji mikubwa.
Kwa upande mwingine, Kwaraa Stadium mkoani Manyara imekuwa mkombozi kwa baadhi ya klabu zinazohitaji sehemu ya kuchezea mechi zao.
Hata hivyo, ukiangalia mahitaji ya ligi yetu na ukubwa wa soka la Tanzania kwa sasa, bado idadi ya viwanja bora ni ndogo mno. Hili ni eneo ambalo linahitaji uwekezaji mkubwa zaidi kama kweli tunataka kuona maendeleo ya soka yanakuwa endelevu.
Kwa miaka ya karibuni, kumekuwa na taarifa nyingi kuhusu miamba ya Kariakoo, Simba na Yanga kuwa na mipango ya kujenga viwanja vyao.
Mara kadhaa mashabiki wameoneshwa michoro mizuri ya viwanja vya kisasa, lakini mingi imeishia kwenye makabrasha na kompyuta bila utekelezaji wa moja kwa moja.
Ukweli ni kwamba, kama nchi ingekuwa na viwanja vya kutosha vya kisasa, huenda isingekuwa hoja kubwa kwa klabu kubwa kutokuwa na viwanja vya mechi.
Lakini kinachoshangaza zaidi ni kuona hadi leo baadhi ya klabu kubwa zikikosa hata uwanja maalumu wa mazoezi.
Ndiyo maana habari za hivi karibuni kuhusu Yanga kupanga kujenga uwanja wake eneo la Jangwani zinapaswa kupokelewa kwa matumaini makubwa.
Eneo hilo ambalo awali lilikuwa likitumika kama uwanja wa mazoezi lina nafasi ya kuwa sehemu ya historia mpya ya klabu hiyo na soka la Tanzania kwa ujumla.
Furaha ya jambo hili si kwa sababu tu Yanga watakuwa na uwanja wao binafsi, bali kwa sababu taifa litapata kiwanja kingine cha kisasa kinachoweza kukidhi mahitaji ya CAF na FIFA, sambamba na uwezo wa kuandaa matukio makubwa ya michezo.
Tukisikiliza maelezo ya awali kuhusu ukubwa wa mradi huo na idadi ya watazamaji wanaotarajiwa, ni wazi kuna ndoto kubwa nyuma yake.
Kilichobaki sasa ni kuhakikisha safari hii haibaki kwenye michoro pekee.
Wadau wa soka wanatamani kuona mradi huo unatoka kwenye makaratasi na kuhamia ardhini.
Endapo hilo litafanikiwa, viongozi watakaosimamia utekelezaji wake watabaki kwenye historia kama mashujaa walioacha alama si kwa Yanga pekee, bali kwa maendeleo ya soka la Tanzania kwa ujumla.
Kila la heri Yanga katika safari hii, ikiwa kweli dhamira ni kujenga kwa maslahi ya klabu na taifa, si siasa za viongozi kutafuta ridhaa ya kuendelea kuaminiwa huku wanachama na mashabiki wakiendelea kuishi kwa matumaini yasiyo na mwisho.