Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kati ya uwekezaji wa bilioni na migogoro ya vyumba vya kubadilishia

NONDO Pict


LIGI Kuu Bara imeendelea kukua kwa kasi kubwa katika miaka ya hivi karibuni na sasa imekuwa miongoni mwa ligi zinazovutia zaidi Ukanda wa CECAFA.


Ukuaji huu umetokana na uwekezaji mkubwa wa kibiashara uliofanywa katika sekta ya soka, hususan kwenye haki za matangazo ya televisheni na redio.


Uwekezaji huo umeifanya ligi yetu ionekane zaidi Afrika na kuongeza ushindani mkubwa ndani na nje ya uwanja.

Mbali na hilo, klabu nazo zimeongeza uwekezaji kwenye usajili wa wachezaji bora, makocha wa kisasa pamoja na kuboresha mazingira ya timu.

Hali hii imewalazimu wasimamizi wa ligi kuweka kanuni na taratibu mbalimbali ili kuhakikisha mechi inasimamiwa kwa weledi unaolingana na thamani ya ligi ilipofikia sasa.

ISAMU 06

Hata hivyo, pamoja na maendeleo yote hayo, bado kuna baadhi ya mambo yanayoturudisha nyuma na kutufanya tuonekane kama tumeweka plasta kwenye jumba la matope. Mojawapo ya mambo hayo ni tabia ya baadhi ya klabu kugomea kutumia vyumba rasmi vya kubadilishia nguo.

Tatizo hili limekuwa likijirudia mara kwa mara katika ligi yetu. Timu zinaingia uwanjani bila kutumia vyumba vilivyotengwa kwa ajili ya maandalizi yao, jambo ambalo ni uvunjifu wa wazi wa kanuni za mashindano.

Mara nyingi mamlaka husika zimekuwa zikitoa faini, lakini bado tatizo linaendelea kana kwamba adhabu hizo hazina uzito wowote. Hii inaonyesha wazi kuna haja ya kuangalia upya namna ya kushughulikia suala hili ili kupata suluhisho la kudumu.

Nalitazama jambo hili katika nyanja mbili muhimu. Kwanza, mamlaka za soka zisipuuzie malalamiko yanayotolewa na klabu kuhusu sababu zinazowafanya washindwe kuamini vyumba hivyo. Kwa sasa hoja kubwa inayotolewa siyo tena ile ya imani za kishirikina kama ilivyokuwa zamani, bali ni hofu ya kupuliziwa dawa zinazoweza kuwanyong’onyesha au kuwaathiri wachezaji kiafya kabla ya mchezo.

ISAMU 07

Katika dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia, mamlaka za soka zinapaswa kuchukua hatua za kitaalamu kuhakikisha vyumba vya kubadilishia nguo vinakuwa salama kwa kila timu.

Inawezekana kabisa kuweka mifumo ya ukaguzi kabla ya timu kuingia vyumbani humo. Kwa mfano, kuwe na maafisa maalum wa ukaguzi wa mazingira ya vyumba, kamera za usalama pamoja na usimamizi wa moja kwa moja kutoka kwa waamuzi au makamishna wa mechi. Hatua hizi zitasaidia kurejesha imani ya vilabu na kuondoa hofu iliyopo.

Haitoshi tu kuendelea kuwatoza faini na kuonekana kama mamlaka zinafurahia ukusanyaji wa fedha huku tatizo lenyewe likiendelea kuwepo.

Pili, ni kuboresha kanuni ili kuondoa kabisa vitendo hivi vinavyoichafua taswira ya ligi yetu. Ukweli ni kwamba kwa klabu nyingi, pesa ya faini haina thamani kubwa mbele ya alama tatu. Timu inaweza kulipa faini lakini ikachukua ushindi wake na kuendelea mbele kwenye msimamo wa ligi. Hapo ndipo tatizo lilipo. Kama kweli tunataka nidhamu irejee, basi adhabu lazima iguse moja kwa moja malengo ya timu, nayo ni pointi.

ISAMU 05

Mimi naamini kuwa timu yoyote itakayokataa kufuata taratibu za kutumia vyumba rasmi vya kubadilishia nguo, iwe kwa sababu za imani za kishirikina au madai ya kisayansi bila uthibitisho rasmi, inapaswa kuadhibiwa kwa kupokonywa alama tatu pamoja na kufungwa mabao matatu. Adhabu hii itakuwa na maumivu makubwa kuliko faini ya fedha. Timu zitajikuta hazioni tena faida ya kuvunja kanuni kwa makusudi kwa sababu hata zikishinda, ushindi huo hautakuwa na maana yoyote.

Ikiwa timu itashinda mechi, basi alama zake ziondolewe moja kwa moja. Kama itapoteza mchezo, bado iondolewe alama tatu kutoka kwenye alama ilizokusanya katika michezo mingine. Aidha, iongezwe mabao matatu ya kufungwa kwenye rekodi zake. Mfumo huu utaifanya kila klabu kufikiria mara mbili kabla ya kukiuka taratibu za mashindano.

Hatua kama hizi zinaweza pia kusaidia kupambana na vitendo vingine vinavyoashiria ushirikina au uvunjifu wa maadili katika mchezo wetu.

  • ISAMU 04

Tukiamua kuwa wakali kwenye nidhamu, tutaisafisha ligi yetu na kuifanya iendelee kuheshimika kimataifa. Haiwezekani tuwe na ligi yenye thamani kubwa ya matangazo, viwanja vizuri na wachezaji wa kisasa, halafu bado tuendelee kushuhudia mambo yanayoonyesha ukosefu wa weledi.

Kwa kifupi, kama tunataka ligi yetu iendelee kukua na kuwa mfano bora Afrika Mashariki na Kati, basi lazima tuheshimu taratibu tulizojiwekea.

Nidhamu ndiyo msingi wa maendeleo ya soka la kisasa. Bila kufanya hivyo, tutaendelea kujenga picha nzuri kwa nje huku ndani kukiwa bado na dosari zinazoturudisha nyuma.