Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar iliyoacha maswali, Dar es Salaam inasubiri majibu

NONDO Pict


SHEREHE kubwa ya soka imefanyika visiwani Zanzibar katika fainali za michuano ya kumbukumbu ya Muungano, ikiwa ni pambano lililowakutanisha wapinzani wa jadi kutoka Kariakoo, Simba SC na Yanga SC.


Tukio hili halikuwa tu mechi ya kawaida, bali liligeuka sikukuu halisi ya soka, likikusanya mashabiki wengi na kuonyesha ushindani wa hali ya juu uliodumu kwa dakika zote 120 za mechi.


Uwanjani, mashabiki walishuhudia aina ya soka la kisasa lililojaa mbinu, nidhamu na akili ya juu ya mchezo. Ingawa kwa macho ya watazamaji wa kawaida huenda haukuwa wa kuvutia sana kutokana na ukosefu wa mabao mengi au mashambulizi ya moja kwa moja, kwa wachambuzi na wataalamu wa soka ulikuwa ni wa kiwango cha juu sana.

PUM 06

Hapa ndipo unapoona namna soka la Tanzania linavyoendelea kukua kimkakati na kila hatua uwanjani inaendeshwa kwa tafiti na mipango kutoka kwenye mabenchi ya ufundi.

Kwa upande wa Simba, walionekana kuingia uwanjani wakiwa na tahadhari kubwa, hasa katika kuzuia mashambulizi ya kushtukiza kutoka kwa wapinzani wao.

Walikuwa na kumbukumbu ya namna Yanga wamekuwa hatari kwenye mipira ya kujibu, chini ya mwongozo wa kocha wao Pedro Goncalves, ambaye ameziumiza timu nyingi kwa mfumo huo.

PUM 05

Mfano mzuri ni ushindi wao dhidi ya Azam katika nusu fainali na walitumia mbinu ya kupokonya mpira na kushambulia kwa kasi. Hivyo basi, benchi la ufundi la Simba lilijikita zaidi katika kuhakikisha mbinu hiyo haifanikiwi.

Kwa upande wa Yanga, walikuja na mkakati tofauti lakini wenye ufanisi mkubwa. Walilenga kuwanyima Simba muda na nafasi ya kufanya maamuzi, hasa katikati ya uwanja.

Wachezaji wao wa kiungo kama Mudathir Yahaya, Mohamed Damaro na Maxi Nzengeli walifanya kazi kubwa ya kuwasumbua wapinzani wao, wakilazimisha Simba kucheza pasi nyingi za nyuma (back passes) na pembeni (square passes).

PUM 04

Hii ilipunguza ubunifu wa Simba na kufanya mchezo ubaki zaidi katikati ya uwanja, hali iliyosababisha hata makipa kupata muda mwingi wa kucheza mpira kwa miguu kuliko kufanya kazi ya kuokoa hatari.

Katika mchezo huo pia kulikuwa na kipengele cha uamuzi wa mwamuzi ambacho kilichangia kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa matokeo.

Ingawa ni kweli hakuna binadamu aliyekamilika kwa asilimia mia moja katika uamuzi, mwamuzi alionyesha ujasiri na kujiamini katika kusimamia mchezo.

PUM 03

Tukio la penalti lililoamua matokeo lilihitaji mtu jasiri sana kulitoa, hasa dakika za mwisho za mchezo. Licha ya presha kubwa, alifanya uamuzi sahihi ambao umeacha mjadala, pia fundisho muhimu kuhusu ujasiri katika uamuzi.

Baada ya fainali hiyo, sasa macho yote yanarejea kwenye ligi kuu na mbio za ubingwa zimepamba moto zaidi.

Yanga inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na alama 47 baada ya mechi 19, huku Simba ikifuatia nafasi ya pili ikiwa na alama 42 ikiwa pia wamecheza idadi hiyo hiyo ya michezo.

PUM 02

Tofauti ya alama tano inaifanya ligi kuwa ya kusisimua zaidi, hasa kuelekea mchezo muhimu wa tarehe tatu ambao unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuamua hatima ya ubingwa.

Ni wazi hatutarajii kuona mchezo tofauti sana na ule wa fainali ya Kombe la Muungano, lakini bado kuna uwezekano wa mabadiliko ya kimkakati kutoka kwa makocha. Pia ubora wa wachezaji mmoja mmoja unaweza kuleta tofauti kubwa, bila kusahau athari za uchovu na majeraha ambazo zinaweza kubadilisha kabisa mwenendo wa mchezo.

Kwa jumla, ushindani kati ya Simba na Yanga unaendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya soka la Tanzania na kila pambano lao linaacha alama ya kipekee kwa mashabiki na wadau wa soka.