Prime
Wachezaji, klabu mtego huu unawahusu kuepuka
LIGI Kuu Bara imeingia kwenye hatua muhimu huku zikiwa zimebaki mechi zisizozidi saba kufikia tamati ya msimu huu wa 2025-2026.
Hiki ni kipindi ambacho kila klabu inapaswa kujitazama upya na kufanya tathmini ya malengo iliyojiwekea tangu mwanzo wa msimu. Je, timu imefikia matarajio yake? Kama bado, je, mechi zilizobaki zinaweza kubadili uelekeo wa msimu wao?
Lakini si klabu pekee zinazopaswa kufanya tathmini. Wachezaji pia wanapaswa kutumia kipindi hiki kujichunguza binafsi. Kila mchezaji anatakiwa kujiuliza kama ameishi katika malengo yake, ameisaidia kwa kiwango gani timu kufikia malengo na kama hajafanikiwa, ni mambo gani yalikuwa kikwazo.
Yapo matatizo yanayoweza kutatuliwa ndani ya muda mfupi na mengine yanahitaji mipango ya muda mrefu ili yasijirudie msimu ujao.
Katika soka la kisasa, jambo la kwanza kwa mchezaji ni kuhakikisha anakitunza kibarua chake na anajenga mazingira ya kuhitajika na klabu nyingine.
Hii humsaidia kukua kisoka na kiuchumi. Ndiyo maana ni kosa kubwa kwa mchezaji anayemaliza mkataba kutokujua mustakabali wake wa msimu unaofuata.
Kwa wale ambao wanaendelea vizuri na majina yao kuwa kwenye vichwa vya habari kila wiki, hiki ndicho kipindi muhimu zaidi cha kutunza viwango vyao.
Kumalizia ligi kwa kiwango kikubwa kunaongeza thamani ya mchezaji sokoni. Unaweza kuwa na mwanzo mzuri wa msimu lakini ukamaliza vibaya na kujikuta kila ulichokifanya miezi yote kikafutwa na mechi chache za mwisho.
Huku kwetu mara nyingi usajili unaangalia kiwango cha sasa kuliko jina au historia ya zamani. Ndiyo maana mwisho wa msimu huwa na uzito mkubwa sana kwa maisha ya mchezaji. Wakati ligi inaisha, swali kubwa huwa ni uko kwenye kiwango gani?
Kwa wachezaji vijana wenye umri wa miaka 20 hadi 25, kuna jambo muhimu wanapaswa kulitazama zaidi ya kiwango cha fedha wanachopewa. Wanapaswa kujiuliza ni timu gani inaweza kuendeleza vipaji vyao.
Kwa mchezaji mwenye uzoefu mdogo wa ushindani mkubwa, si kila timu yenye jina kubwa ni sehemu sahihi kwake. Wakati mwingine timu yenye presha kubwa ya kutafuta mataji inaweza kuharibu hatua za ukuaji wa mchezaji.
Mchezaji mdogo anahitaji sehemu ambayo itampa nafasi ya kucheza, kujifunza na kufanya makosa huku akiendelea kukua. Lakini kwa wale ambao tayari wana uzoefu wa misimu kadhaa ya ushindani, inaweza kuwa wakati sahihi kwenda kwenye timu kubwa zaidi ili kupata changamoto mpya na kuendeleza uwezo wao.
Ukuaji wa mchezaji hautegemei kipaji pekee, bali pia aina ya mazoezi anayofanya, wachezaji anaocheza nao na kiwango cha mashindano anayoshiriki. Ndiyo maana timu zinazoshiriki michuano mikubwa ya kimataifa mara nyingi huchangia kukuza vipaji kwa kasi kubwa.
Hata hivyo, ushindani mkubwa pia una changamoto zake kwani umewahi kufupisha safari za baadhi ya wachezaji kutokana na presha kubwa ya matokeo.
Hivyo basi, watu wanaowasimamia wachezaji wanapaswa kuangalia zaidi hatua za maendeleo ya mchezaji kuliko kuvutiwa na fedha pekee.
Dunia ya soka ina mifano mingi inayothibitisha umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi katika hatua za maendeleo ya mchezaji.
Tunayo mifano mizuri kama wa Novatus Dismas ambaye alipitia hatua nzuri ya maendeleo kupitia Biashara United kabla ya kurejea Azam FC na baadaye kwenda Ulaya. Safari yake inaonyesha namna mpangilio mzuri wa maendeleo unavyoweza kumsaidia mchezaji kufikia mafanikio makubwa.
Pia duniani tuliona namna familia ya Erling Haaland ilivyofanya uamuzi wa busara kwa kukataa haraka ofa nyingi kubwa na kumpeleka Borussia Dortmund kabla ya kuhamia Manchester City. Hatua hizo zilimjenga taratibu mpaka kufikia kiwango cha sasa.
Kwa upande mwingine, tumeshuhudia vipaji vingi vikipotea kutokana na uamuzi usio sahihi. Hii ni mifano michache tu ya namna uchaguzi kati ya pesa na maendeleo ya kipaji unavyoweza kuamua hatima ya mchezaji.
Kitu kingine muhimu ni suala la mikataba. Hizi si zama tena za kushuhudia mchezaji akiingia kwenye migogoro ya kusaini zaidi ya timu moja.
Wasimamizi wa wachezaji wanapaswa kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa ili kumpunguzia mchezaji presha.
Jukumu la mchezaji linapaswa kuwa kutunza kiwango chake uwanjani, huku suala la mazungumzo ya mikataba na usajili likibebwa na uongozi wake.
Dirisha kubwa la usajili la msimu wa 2026-2027 linakuja na bila shaka mechi hizi chache zilizobaki zitakuwa na mchango mkubwa katika kuamua mustakabali wa wachezaji wengi pamoja na klabu zao. Hivyo basi, wakati wa kufanya tathmini ni sasa.