Meja Jen. Isamuhyo; CAF haina shaka kwa AFCON 2027
Muktasari:
- Uwanja huo ulipata heshima hiyo baada ya Simba kuamua kuutumia kwa mechi zake za nyumbani kutokana na kufungwa kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya maboresho na utatumika kuandaa Fainali za Afcon 2027.
UWANJA wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni Dar es Salaam, uliandika historia baada ya kuchezwa moja ya mechi kubwa za Ligi Kuu Bara, Kariakoo Dabi, iliyohusisha watani wa jadi, Simba na Yanga.
Uwanja huo ulipata heshima hiyo baada ya Simba kuamua kuutumia kwa mechi zake za nyumbani kutokana na kufungwa kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya maboresho na utatumika kuandaa Fainali za Afcon 2027.
Isamuhyo unaingiza mashabiki 12,000 na ulitumika katika mechi hiyo ya watani licha ya uwepo wa viwanja vingine vilivyodhaniwa huenda vingetumika badala ya huo.
Hata hivyo, mashabiki waliokuwapo katika mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2 ilifana na mashabiki walifurahia mandhari nzuri na ya kuvutia.
Kutokana na udogo wake hasa kwenye idadi ya mashabiki, wengine walidhani Dabi ingefanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha au New Amaan Complex Zanzibar, kwani timu hizo zote zilikuwa visiwani humo kwa ajili ya fainali ya Kombe la Muungano.
Hata hivyo, Simba, ikiwa kama timu mwenyeji yenye haki ya kuchagua uwanja wa nyumbani kama kanuni za Ligi zinavyoelekeza, ilitangaza kuutumia Isamuhyo. Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilibariki uamuzi huo na mechi ikapigwa.
Aprili 24, Bodi ya Ligi ilitangaza rasmi Dabi kupigwa Isamuhyo, na maandalizi ya uwanja na miundombinu mingine yalianza mara moja, ikiwemo kuongeza viti 2,000, kufikia jumla ya viti 12,000.
Kuelekea mchezo huo, kulizuka vimbwanga vingi. Video zikisambaa zikionyesha uwanja ulivyo na matope kutokana na mvua zilizokuwa zinaendelea kunyesha Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi, lakini hilo halikubadilisha maamuzi.
Mwanaspoti limepiga stori na meneja wa uwanja huo, Said Mpuche, ambaye ameeleza mengi, ikiwemo mpango mkakati wa uwanja huo kwa miaka ya baadaye na sasa.
Wala hakuwa na presha
Mpuche anasema hakuhisi presha katika kuandaa uwanja kwa ajili ya Dabi kwani ‘pitch’, ambayo ndio kigezo cha kwanza katika sheria za mpira wa miguu, ilikuwa katika hali nzuri.
“Nilipewa taarifa siku tano kabla ya mechi. Sikuwa na presha kwani kazi yangu ilikuwa ni kufanya maandalizi. Pitch ilikuwa nzuri na maboresho yalihitajika kwenye miundombinu mingine, tofauti na pitch, ambayo haikuwa kikwazo kutokana na utayari wa viongozi wangu. Tulikaa tukaona nini cha kuongeza na tulifanikiwa kufanya kwa wakati. Shauku yangu ilikuwa kuona mashabiki wanafurahi. Tukaona kuongeza viti ni jambo muhimu, tulifanikiwa kuongeza viti 2,000,” anasema Mpuche.
Anaongeza: “Ningelala mimi, shughuli nyingine zote zingelala.”
Zile video ni kutoana mchezoni
Mpuche anasema video zilizokuwa zikienea zilikuwa ni ‘mind game’, kwani eneo la kuchezea lilikuwa vizuri. Video hizo zilionyesha tu sehemu za nje ya pitch, si eneo la mchezo.
“Zile video zilikuwa za kutoana tu mchezoni. Eneo la kuchezea lilikuwa vizuri. Video hizo zilitengenezwa nje ya eneo la kuchezea, na Yanga walikuja kufanya mazoezi kwa nusu saa tu mvua ilikuwa imekata. Uwanja huu kila mita mbili una mifereji ya kutoa maji ‘(drainage system)’ vizuri. Kwa ubora wa Uwanja wa Isamuhyo, sio Dabi tu; hata mechi za timu ya Taifa Stars zinaweza kupigwa hapa,” anasema, huku akisisitiza kuandaa Dabi kumempa funzo na kuongeza uzoefu.
CAF haina shaka
Uwanja wa Isamuhyo ni mojawapo ya viwanja vya mazoezi vitakavyotumika katika mashindano ya AFCON 2027, yatakayofanyika katika nchi za Tanzania, Kenya, na Uganda.
Meneja huyo anasema CAF imekuwa ikivikagua mara kwa mara na kutoa maoni chanya kuhusu uwanja huo.
“Maandalizi kuelekea AFCON 2027 yanaendelea vizuri. CAF wanakuja kukagua uwanja kila siku na hawana shaka. Uwanja wetu upo tayari tofauti na viwanja vingine vya mazoezi,” anasema, huku akiongeza ndoto yake kama meneja ni kusimamia mechi kubwa ikiwemo Dabi ya Kariakoo.
Malengo ni mashabiki 20,000
Licha ya kuongeza majukwaa na uwezo wa mashabiki 12,000, malengo ni uwanja kubeba mashabiki 20,000 waliokaa.
“Tunapanga kwa hatua, hadi msimu mpya kuanza tutakuwa tumeshaweka majukwaa ambayo yataweza kufungwa viti 20,000,” anasema.
Ishu ya Yanga kususia ‘Dressing Room’
Meneja anasema mapema asubuhi ya siku ya mchezo aliwasilisha funguo kwa walinzi wa timu, bila kupokea malalamiko yoyote kutoka kwa timu yoyote.
“Niliwakabidhi funguo mapema, sikupokea malalamiko yeyote. Vyumbani kuna AC na feni. Madirisha makubwa, futi sita kwa saba, waliamua tu hivyo na hatuwezi kuwazuia. mamlaka zimeona,” anasema.
Maboresho makubwa
Mpuche anasema maboresho makubwa yanaendelea kwenye majukwaa, vyumba na maeneo ya kuegesha magari ili kufikia vigezo vya CAF.
“Tunaongeza vyumba; sasa tunapaswa kuwa na vinne, vipo tatu. Tuna eneo kubwa la parking, media room nzuri. Ujenzi wa uwanja una hatua tatu: kuweka majukwaa, kufunga viti, na kuweka paa kuzunguka uwanja mzima,” anasema Mpuche, ambaye amepokea tuzo sita kama meneja bora wa uwanja.
Utapokelewa kulingana na hadhi
Uwanja wa Isamuhyo ni wa JKT Tanzania, lakini unaruhusiwa kwa timu yoyote kuutumia kwa gharama tofauti kulingana na hadhi ya ligi yao.
“Tunapokea kila timu. Timu ya Ligi Kuu haitalipa gharama sawa na timu ya Championship au First League. Hata Yanga au Simba hawawezi kulipa sawa na Mtibwa au Fountain Gate. Milango iko wazi, yeyote anakaribishwa,” anasema.
Isamuhyo kuwa Complex
Ndoto ya viongozi wa JKT Tanzania ni kuwa na Complex inayoweza kuhost michezo mbalimbali, sio tu mpira wa miguu. “Viongozi wana mipango ya kujenga Arena, uwanja wa mpira wa kikapu, na uwanja wa Beach Soccer. Mambo mazuri yanakuja,” anasema Mpuche.
Ukifika Isamuhyo Cheza kwa ‘Stepu’
Meneja anasema mashabiki wanatakiwa kufuata taratibu uwanjani ili kuepuka fujo.
“Sisi tuna walinzi wetu wa kiraia ambao huenda majukwaani kulinda mashabiki na mali zao. Mashabiki wanatakiwa kufurahia mchezo bila wasiwasi na hatutaki mtu yoyote atoke kwetu akiwa ameumia, hivyo tutakulinda usiumie na wala usimuumize mwingine” anasema.
Uwanja wa Isamuhyo ulianza kutumika rasmi kwa michezo ya Ligi Kuu mwanzoni mwa 2024. Kutokana na maboresho, mechi zinachezwa hadi usiku na upo tayari kuandaa mashindano ya AFCON 2027 ambapo utatumia kama sehemu ya mazoezi ya timu.