Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mohamed Abdul Wahab, gwiji aliyetunga nyimbo za taifa za mataifa ya kiarabu

MAND 01

Muktasari:

  • Msanii huyu anaheshimiwa sio kwa nyimbo za mapenzi tu bali pi kwa uzalendo na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa nchi nyingine za Kiarabu na kupelekea kutunga wimbo wa taifa wa Palestine, Libya, Misri, Tunisia, Algeria na Iraq.

NCHI nyingi za Kiarabu wakati wa sikukuu ya Idd el Fitr baada ya kumalizika mwezi wa Ramadhani zitakuwa na maonyesho ya mtunzi na muimbaji maarufu wa Misri Mohamed Abdul Wahab aliyefariki 1991 akiwa na miaka 89.

Msanii huyu anaheshimiwa sio kwa nyimbo za mapenzi tu bali pi kwa uzalendo na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa nchi nyingine za Kiarabu na kupelekea kutunga wimbo wa taifa wa Palestine, Libya, Misri, Tunisia, Algeria na Iraq.

Kwa mashabiki wa  nyimbo za Kiarabu katika nchi nyingi nyimbo za Abdul Wahab zimetoa mafunzo mengi na sauti yake ilipendwa kwa vile ililiwaza wale waliokuwa na majonzi..

Miaka imepita  tangu kung’ara kwa jina, nyimbo na michezo ya msanii huyu wa Misri aliyeanza kuimba akiwa na miaka 13, akaendelea kwa miaka 40 na pia kutunga nyimbo, kupiga  ala na kutia muziki katika nyimbo alizotunga na za wengine.

MAND 02

Alipokuwa mcheza sinema wa michezo aliyoitunga alikuwa kivutio cha watu wengi Misri, nchi za Kiarabu na mwambao wa Afrika ya Mashariki.

Kifo cha Mohammed Abdulwahab aliyejulikana kama baba wa muziki wa Misri aliyeiaga dunia 1991 kilizusha huzuni kubwa Misri na nchi za Kiarabu.

Hali hii ilitokana zaidi na kwamba katika nyimbo  nyingi alisikitika namna mapenzi yalivyousumbua moyo wake ambao aliulaumu kwa kumshawishi kumpenda mtu ambaye hakuthamini mapenzi yake.

Kila nilipotembelea Misri miaka ya 1960 na 1970 nilihakikisha ninahudhuria angalau onyesho lake moja au la waimbaji maarufu kama Farid el Atrash, Ummu Kulthum na Abdelhalim Hafidh ambao katika nyimbo zao upo mkono wa Abdulwahab kwa kuufanyia wimbo marekebisho au kuutia muziki.

Siku moja nilifika kwenye jumba la sanaa la Qasr Al-Tawzoq liliopo Alexandria ili kumuona Abdulwahab akifanya vitu vyake.

Nilifika saa moja kabla ya onyesho kuanza na kuambiwa tiketi zilimalizika mchana na juhudi zangu za kupatiwa tiketi ziligonga ukuta.

Nilipokuwa ninabembeleza kupata tiketi alikuja askari polisi kunitaka niondoke na kwa bahati nzuri akaniuliza ‘’Anta min Eiyn”, yaani Wewe unatoka wapi?

MAND 03

Nilipomwambia Zanzibar, Tanzania, na kumueleza kwamba baba wa taifa wa Misri, Rais Gamal Abdel Nasser alitembeea nchi yetu na anapendwa, askari aliniombea nafasi nijibanze kumuona Abdulwahab.

Nilifurahia onyesho, hasa kwa vile lugha ya Kiarabu hainipigi chenga.

Kila nilipofika Misri nilinunua rekodi za santuri au mikanda ya kunasia sauti ya nyimbo zake kwa matumizi yangu au zawadi.

Kati ya michezo ilionivutia ni ‘Uwa Jeupe la Waridi’, ‘Risasi Iliyochoma Moyo’, ‘Mimi Siyo Malaika’ na ‘Mapenzi Hayaruhusiwi,’ ambayo ndani yake aliimba nyimbo za kusikitisha na kulamikia mapenzi kumuumiza moyo.

Miongoni mwa nyimbo zilizonisikitisha zaidi ni ule wa ‘Aziza’ ambao ulifanya watungaji nyimbo za taarab wa Zanzibar hapo zamani pia kutunga nyimbo za ‘Aziza’. Mojawapo ni ile yenye beti isemayo “Aziza katoka kwangu kwa nadhafa na weupe.”

Wimbo huu ulisimulia majonzi ya mtu aliyekimbiwa na mpenzi wake.

Moja ya nyimbo zake zilizonipa mafunzo ni ule usemayo katika beti zake…”Unapokuwa pembeni mwangu huona raha kama ya mtu aliye peponi na unapokuwa mbali naona shaka na kujiuliza lini utakuja tena pembezoni mwangu.”

Katika nyimbo nyingine Abdulwahab alisema “…Unanionea kwa kukupenda… Mimi sistahiki lawama, kama unataka kulaumu unapaswa kulaumu macho yangu ambayo ndio yaliyokuona  na moyo ukapenda.”

Abdul Wahab hakuwa mkocho katika bahari ya sanaa tu, bali mzalendo kindaki ndaki wa kuhamasisha watu kupenda nchi zao, kupambana na wakoloni, kukataa ubaguzi, kuvumilianana na kupenda majirani.

Aliwaachia Wamisri usia wa hekima kwa kuwaambia unaweza kuchagua mume, mke au rafiki, lakini sio baba, mama, ndugu au jirani.

MAND 04
MAND 04

Aliwataka Wamisri wasijipe shida kwa kutofautiana na majirani kwa vile watakuwa nao wakati wote katika maisha yao.

Katika miaka ya nyuma nyumba ya kila Mwarabu  mwenye uwezo mzuri  wa maisha sahani za santuri za Abulwahab hazikukosekana.

Ilikuwa kawaida ukitembea katika barabara au kwenda kwenye masoko ya Misri, Lebanon, Algeria, Syria na Yemen kusikia nyimbo za Abdulwahab.

Hata wakulima waliona raha kufanya kazi huku wakiimba nyimbo zake na hivyo hivyo kwa madereva wa taxi au wanaosukuma mikokoteni.

Katika kipindi cha miaka 74 katika usanii Abdulwahab alitunga zaidi ya nyimbo 1,800 za mapenzi na masuala mengine, kama ya kushawishi watu kukataa ukoloni.

Vile vile aliwasaidia waimbaji chipukizi kwa kuwatungia nyimbo na kuwatilia muziki. Alimtungia nyimbo nyingi muimbaji maarufu wa Misri, Ummu Kulthoum.

Mbali ya mashairi kuwa  na mvuto sauti yake iliwacha hoi wapenzi wa muziki wa Kiarabu na hasa kwa alivyocharaza ala ya oud.

Siku moja alipoimba na huku akipiga oud aliwaliza marafiki zake, wakiwamo Rais Nasser na Makamu wake Zakaria Muhiddin, pale alipofyatua beti iliyowaambia viongozi wa Misri …Mtalaumiwa kaburini mkiusaliti umma uliowapa madaraka.Mchezo  wake wa kwanza wa sinema ulikuwa katika mwaka 1933 na alitunga mchezo mpya baada ya kila kipindi cha kati ya miezi sita na mwaka mmoja.

Baada ya mapinduzi ya Misri ya 1952 yaliyouondoa utawala wa mfame Farouk bin Ahmed Fuad, Abduwahab alisaidia kujenga mshikamano wa watu wa Misri.

Nyimbo zake kama “Mto Nile Usiokuwa na Mwisho’, ‘Damascus,’ na ‘Palestine’ zilikuza uzalendo Misri na nchi za jirani.

Haikushangaza kuona yeye ndiye aliyetunga nyimbo za taifa za Misri, Oman, Umoja wa Nchi za Ghuba, Tunisia na Libya.

Wimbo wake wa mwisho alioutunga miaka michache kabla ya kuiga dunia usemao “Min Gheir Ley” (Bila ya Kuuliza Kwanini), uliwaliza Waarabu na hasa alipoiaga dunia. Alifanyiwa mazishi yaliyokuwa na heshima za kijeshi.

Kwa mwezi mzima baada ya kifo chake magazeti, vituo vya radio na runinga vya Misri vilifanya uchambuzi wa maisha yake na urithi wa sanaa aliouacha.

Majengo, barabara, shule na vituo vya afya vingi Misri vimepewa jina lake kwa kumheshimu.

Katika eneo la Bab El-Sheriyah alipozaliwa 1920 limejengwa sanamu la makumbusho yake.

Misri na nchi za Kiarabu zimezalisha waimbaji wengi mashuhuri, lakini panga pangua huwezi kuliweka pembeni jina la Abdulwahab unapozungumzia nyota wa sanaa wa nchi za Kiarabu.

Umaarufu wake unajitokeza  hadi leo katika kampeni za uchaguzi au maandamano ya kuunga mkono au kupinga jambo kwa nyimbo zake kupigwa.