MWANENGO: Kiungo Tabora United mwenye ndoto ya udaktari akiwataja Max, Fei Toto

Muktasari:
- Kiungo huyu mshambuliaji ambaye amekuzwa kisoka katika kituo cha kukuza vipaji cha LG Organisation, alianzia kucheza soka lake la kulipwa nje ya nchi kabla ya kurejea nchini na kutua kwa 'Wana Nyuki hao'.
UKIWA ndiyo msimu wake wa kwanza Ligi Kuu Bara, kiungo Emmanuel Mwanengo wa Tabora United tayari ameshatwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mechi, dhidi ya Tanzania Prisons akifunga bao la kusawazisha katika sare ya bao 1-1.
Kiungo huyu mshambuliaji ambaye amekuzwa kisoka katika kituo cha kukuza vipaji cha LG Organisation, alianzia kucheza soka lake la kulipwa nje ya nchi kabla ya kurejea nchini na kutua kwa 'Wana Nyuki hao'.
Mwanengo alipiga stori na Mwanaspoti akiwataja wachezaji Feisal Salum 'Feitoto na Max Mpia Nzengeli ni wachezaji wa aina gani pamoja na Eritier Makambo na Yacuba Sogne anaokipiga nao Tabora United.
ALIKOTOKEA.
Mwanengo anasema kabla ya kujiunga na timu ya Tanzania, alianzia soka lake la kulipwa katika Ligi Kuu ya Vysshaya ya nchini Tajikistani.
Alianza kucheza huko katika klabu ya Ravshan Kulob, kabla ya kusajiliwa na Vakhsh na msimu huu kujiunga na Tabora United inayokamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara huku akiwa amefunga bao moja hadi sasa.

AKUBALI YAISHE KWA MAKAMBO, SOGNE
Anasema ubora wa Makambo na Sogne umemhamisha namba kutoka kucheza kama mshambuliaji na kushuka chini hadi kiungo mshambuliaji. Hata hivyo, anasema wakati mwingine amekuwa akitumiwa kama winga wa kushoto au kulia kwani kote huko anapamudu.
"Nafasi niliyokuwa nakuja kucheza katika timu hii ina watu ambao ni nyota wa kigeni, ambao pia tayari wana uzoefu wa ligi ya Tanzania, Heritier Makambo na Yacouba Sogne."
"Ni wachezaji wenye ubora na wazoefu, hata hivyo sikuwa na hofu, niliamini nitakuja kupambania nafasi."
"Pia kocha aliona nafasi hiyo sitaweza, sikupinga. Mimi ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani hivyo sikuwa na uhakika wa kuja kucheza moja kwa moja kikosi cha kwanza, lakini niliamini nitapambana na nitapata nafasi nashukuru imekuwa hivyo."
Anasema yeye ni mzuri kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji kwa sasa kutokana na kupata nafasi ya kucheza eneo hilo, lakini kwa upande wake amekuwa bora kwenye maeneo matatu tofauti, mshambuliaji, winga zote mbili na eneo mama analocheza sasa kutokana na uwepo wa Makambo na Yacouba.

MAXI, FEITOTO NI VIPAJI
Ni nadra sana kwa wachezaji kukubali uwezo wa wao kwa wao, lakini kwa Mwanengo, humwambii kitu kwa Maxi na Fetoto na kukiri wanamvutia kwa aina yao ya uchezaji.
"Ligi ya Tanzania ina vipaji vingi, ukiondoa nyota wa kigeni kuna wazawa wanafanya vizuri na ni bora kutokana na aina yao ya uchezaji. Mfano Fei Toto, mimi nafurahi kumtazama na najifunza mambo mengi kutoka kwake," anasema na kuongeza;
"Ni mchezaji mzuri sana ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi, ana utulivu mguuni, pia anacheza mpira wa akili, siyo nguvu.Mimi navutiwa kumtazama na nimekuwa nikijifunza vingi kutoka kwake."
Kwa upande wa Maxi anasema; "Kuna wachezaji wengi wanacheza eneo lake (mawinga au viungo washambuliaji) ni bora na navutiwa nao kama Clatous Chama na Stephane Aziz Ki, hata hivyo, kwa Nzengeli wanagonga mwamba, ni mchezaji mzuri sana. Anacheza vizuri kwenye nafasi, hatumii nguvu, ana kipaji kikubwa sana. Kuna wachezaji wenye vipaji na wachezaji wa mazoezi, mimi naamini Nzengeli ni kipaji."

KAGOMA MTU KAZI
Mwanengo anasema Yusuph Kagoma anajua mpira na ni kiungo mgumu ambaye alimpa sana kashikashi walipokutana kwenye michezo yao yote na ana heshimu ubora wake.
Utakumbuka nyota huyu wa Simba, aliwahi kuziingiza vitani watani ikiwamo Yanga iliyozidiwa kete. Kagoma amepita timu za Keita Gold na Fountain Gate na Mwanengo anasema kwa viungo wazawa hadoi sasa Ligi Kuu Bara, hajaona kama yeye.
"Kagoma anacheza vizuri. Ni mchezaji mgumu sana kumkaba. Kwa timu ambazo nimekutana nazo hadi sasa, huyo ndio mchezaji aliyenipa wakati mgumu kumpita, naweza kusema ni kiungo wangu bora wa chini ligi kuu," anasema na kuongeza;
"Wengine nimekuwa nikiwatazama tu wakicheza, naheshimu uwezo wao, lakini sijajua nikikutana nao itakuwaje. Kwa ambao tayari tumekutana kwangu Kagoma ni kiungo bora ambaye ili uweze kumpita unatakiwa kujiandaa kiakili na kimwili kwani ni mzuri akiwa na mpira na hata akipoteza unaona namna anavyohangaika kuutafuta."

NDOTO YA UDAKTARI
Mwanengo anasema haikuwa rahisi kwake kucheza soka kutokana na wazazi wake kutaka awekeze jitihada zake katika elimu. Anasema baba yake sio kwamba haamini katika kile anachokifanya bali ni kutokana na kuona katika familia yao hakuna aliyefanikiwa kutokana na mpira, ingawa yeye ana imani kubwa na anamshukuru Mungu soka limemlipa kwa kiasi chake.
"Wazazi wangu hawakuwahi kuamini katika soka. Walinihimiza zaidi kupambana na masomo. Nimesoma hadi kidato cha sita na baada ya hapo nilimshawishi baba aniache nifanye kile ninachokipenda, ndiyo ukawa mwanzo wangu wa kucheza. Hata hivyo, bado nina ndoto ya kurudi chuo kwenda kutimiza ndoto ya kuwa daktari," anasema.
"Mbali na kutamani kucheza mpira, isingekuwa hivyo, ndoto yangu ilikuwa ni kuwa daktari kitu ambacho naamini muda wowote naweza kukitimiza kwani nina matokeo mazuri ambayo yanaweza kutimiza malengo yangu hivyo ni suala la muda tu," anasema Mwanengo ambaye haamini katika ushirikina katika soka na hajawahi kukutana na mambo kama hayo akiwa nje tofauti na alivyorudi Bongo na kuona kuna wanaoamini mambo hayo.
KWA NINI NAMBA 16?
Kila mchezaji anachagua kuvaa namba ya jezi kutokana na sababu zake. Wapo wanaochagua kutokana na matukio mbalimbali au mapenzi na nyota waliowahi kuvaa namba hizo.
Hata hivyo, kwa Mwanengo anasema yeye kuvaa namba 16 ni kwasababu moja tu, bahati.
"Napenda kuvaa jezi hiyo kwa sababu nikivaa nakuwa na bahati nayo, pia nakuwa na furaha. Haina maana nyingine yoyote.
"Jezi namba 16 ni namba ya bahati kwangu, imenipa ubingwa wa Ndondo Cup. Nakumbuka msimu wangu wa kwanza nacheza nikiwa na Madenge FC nilibeba kombe hivyo najihisi nakuwa na bahati nikiivaa hiyo ndio sababu kubwa."
KUHUSU NAHODHA, HIVI NDIVYO ANAVYOWAJUA
"Nahodha ni kiongozi wa wachezaji katika timu. Mechi inapochezwa uwanjani, yeye ndiye msemaji mkuu wa timu. Hata ikitokea shida yoyote kwa wachezaji wenzake, atakuwa wa kwanza kuongea na mwamuzi au mchezaji. Pia ana jukumu la kutengeneza ari ya kupambana na hamasa kwa wenzake pindi wanapokua kwenye hali ya kukata tamaa uwanjani," anasema na kuongeza;
"Kuna watu wamezaliwa kuwa viongozi, lakini sifa kubwa ni kujitolea kwa ajili ya timu na kuwa mfano na mtekelezaji wa mambo yanayotakiwa kutekelezwa," anasema Manengo ambaye ni mtoto wa nne kwenye familia ya watoto watano akiwa ni wa kiume pekee.
UWEKEZAJI MUHIMU
Nyota wengi wamekuwa wakisubiri kumaliza kucheza soka ndipo wafundishe au kusaidia katika kukuza vipaji vya chipukizi. Hata hivyo, anasema baada ya kusajiliwa na kupata pesa, aliamua kurudi na kuwekeza katika kitua ambacho kilimkuza kiuchezaji ili kuendeleza vipaji vya walio mitaani.
"Siwezi kusema ni kiasi gani nilipata kwenye usajili wangu wa kwanza, lakini ni fedha nzuri na ndefu. Nilichokifanya ni kuwekeza kwenye kituo kilichonilea ili kiendelee kukuza wachezaji wengine bora ambao pia watatimiza malengo yao," anasema na kuongeza;
"Nimekuzwa katika kituo kinachoitwa LG Organisation, kinachosimamiwa na bosi wangu ambaye aliona uwezo wangu na kuniamini kwa kunipa nafasi ya kupita hapo. Hadi sasa nimekuwa mchezaji ambaye najulikana. Ndiyo maana nikaona bora na mimi niwekeze huko."
Mwanengo anasema ana imani katika kuwasaidia wengine ili na wao waweze kufikia malengo waliyojiwekea kama ambavyo na yeye alikuwa anatamani kucheza mpira na kuonekana.