Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ni muda mzuri wa kuwauza Domayo, Messi

Muktasari:

Ukingalia siri kubwa ya ushindi wa Yanga hapa nyumbani ni kushambulia kwa kasi katika dakika zote za mchezo na hiyo ndiyo silaha pekee kwao kesho watakapocheza mechi yao ya marudiano ya kusaka kufuzu kwa hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

MABINGWA wa soka wa Tanzania, Yanga kesho Jumapili watakuwa na kazi moja kubwa ya kulinda ushindi wao kwa kuhakikisha Al Ahly hawapati nafasi ya kucheza kama wanavyotaka.

Ukingalia siri kubwa ya ushindi wa Yanga hapa nyumbani ni kushambulia kwa kasi katika dakika zote za mchezo na hiyo ndiyo silaha pekee kwao kesho watakapocheza mechi yao ya marudiano ya kusaka kufuzu kwa hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Naamini kama Yanga wakiingia uwanjani wakiwa wameandaliwa vizuri kisaikolojia na wachezaji wakicheza kwa nidhamu kama ilivyokuwa hapa Dar es Salaam hakuna shaka kwamba wataivua ubingwa Al Ahly.

Naamini kitendo cha Yanga kuitoa Al Ahly kitawaongezea sifa viongozi wa Yanga kwani mashabiki wao wamesubiri kwa muda mrefu kuona timu hiyo ikirudia rekodi yake ya mwaka 1998, wakati walipofuzu kwa mara ya mwisho kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Pamoja na kufurahia mafanikio hayo ya Yanga, lakini bado nimeingiwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wa kikosi chetu cha timu ya taifa na hatima ya wachezaji wetu.

Yanga inafanya vizuri, lakini ukiangalia sehemu kubwa ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza si wachezaji wa Tanzania, ambao ni Haruna Niyonzima (Rwanda), Hamisi Kiiza na Emmanuel Okwi (Uganda), Didier Kavumbagu( Burundi), Mbuyu Twite (DR Congo).

Hali hiyo si kwa Yanga tu bali ni timu zote kubwa, washambuliaji wake wengi si Watanzania kwa Azam, Kipre Tchetche (Ivory Coast), Simba wanaye Amissi Tambwe (Burundi), Coastal Union, Yayo Kato (Uganda).

Ukiangalia orodha ya wafungaji utabaini bado Tanzania imepoteza washambuliaji, hatuna tena wale kina Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, Edward Chumila, Said Mwamba ‘Kizota’ na wengineo.

Hii yote ni kwa sababu dunia imebadilika sisi tumekalia uzamani na kujifungia ndani, klabu zetu zimeshindwa kuwapa miongozo wachezaji wetu chipukizi kwenda kucheza soka nje ya nchi.

Moja ya wasia wa kocha Kim Poulsen wakati akiwaaga Watanzania ni pale alipoitaka TFF pamoja na klabu kuhakikisha wachezaji wengi wanakwenda kucheza soka la kulipwa kama kweli Tanzania inataka kufanikiwa.

Ni kweli hatuwezi kufanikiwa kwa kutegemea wachezaji wanaocheza ligi ya ndani tu, kama kuna wachezaji wanatoka Uganda, Kenya, Burundi na Rwanda wanaocheza hapa, kwa nini wachezaji wetu wanashindwa kwenda huko.

Naamini sasa ni wakati wa Frank Domayo, Simon Msuva, Ramadhani Singano, Haruna Chanongo na chipukizi wengine wa Kitanzania kufanyiwa mipango ya kupata timu za kucheza nje ya nchi kwa lengo moja tu, baadaye waisaidie Taifa Stars.

Wenzetu Brazil baada ya kuona timu yao ya taifa imepwaya na wanajiandaa na Kombe la Dunia, walifanya mpango wa makusudi kwa kuunda timu ya taifa ya jina, pia walihakikisha kila kijana mwenye kipaji na klabu yoyote Ulaya inamtaka basi walihakikisha anauzwa huko haraka. Chipukizi waliouzwa kwa mpango huo ni Oscar kwa Chelsea, Lucas Moura (PSG), Bernard (Shakhtar Donetsk), wa mwisho ni Neymar ambaye aligoma kuuzwa hadi baada ya Kombe la Dunia, lakini alilazimika kuondoka Santos mwaka jana na kujiunga na Barcelona.

Ni lazima tuige mbinu hii ya Brazil kama kweli tunaka kupata mafanikio kwenye timu ya taifa. Ni lazima kina Domayo wauzwe sasa ili watusaidie fainali za Kombe la Dunia 2018 za Russia.