NINACHOKIAMINI: Nyota wa Yanga wanapocheza chai maharage Yombo!
Muktasari:
- Umewahi kujiuliza kwanini mashabiki wa Ulaya, wanapenda kuwapapatikia wachezaji wao nyota kiasi kwamba ikitokea mchezaji akapita mtaani huwa ni balaa!
NIMEKUWA najiuliza kwa muda mrefu kama Watanzania wanadharau au wanasingiziwa tu? Sijui, itatokana na mtazamo wa kila mmoja baada ya mjadala huu.
Umewahi kujiuliza kwanini mashabiki wa Ulaya, wanapenda kuwapapatikia wachezaji wao nyota kiasi kwamba ikitokea mchezaji akapita mtaani huwa ni balaa!
Wayne Rooney akipita katika mitaa ya Manchester, atazungukwa na watu mbalimbali wakitaka wapige naye picha na wengine wakitaka awasainie katika vitabu vyao.
Santi Cazorla akipita mitaa ya London itakuwa ni balaa kubwa, mashabiki watamsumbua kiasi kwamba safari yake inaweza kuishia hapo. Kuna ambao watataka kumuuliza maswali na wengine kupiga naye picha na kusaini vitabu.
Kutokana na wimbi hilo la nyota wa soka wa nchi za Ulaya kupapatikiwa na mashabiki wao mitaani ndio maana maisha ya nyota hao yamekuwa ni ya kificho.
Wanaendesha magari ambayo vioo vyake havionyeshi watu waliomo ndani, wanakwenda kwenye klabu za starehe za gharama kubwa ambako watu wengine hawawezi kufika, wanakwenda kwenye maduka makubwa kununua nguo zao na kwa ujumla wanafanya mambo yao kwa makini na kwa kificho. Hiyo ndiyo hasara ya kuwa supastaa. Wanaishi maisha ya nidhamu fulani, hawaonekani hovyo mitaani kwa sababu wanalinda hadhi zao.
Kwa sababu hawaonekani mara kwa mara ndio maana ikitokea wakaonekana mtaani kwa bahati mbaya huwa ni vurugu tupu, kwa sababu mashabiki huwa na hamu ya kuwaona. Na ndio maana wanapata matangazo mengi ya biashara.
Nenda hapo Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, utaona maisha ya Mbwana Samata. Haonekani hovyo mtaani, anaishi maisha kama ya mastaa wa Ulaya na ndivyo inavyotakiwa.
Ndio maana Samata akionekana mtaani Lubumbashi, mashabiki wengi hutaka asaini katika vitabu vyao, hutaka wapige naye picha na wengine husikia raha tu wakimuuliza maswali.
Njoo hapa nyumbani Tanzania. Nauliza Watanzania wana dharau au? Mbona Mrisho Ngassa akipita mtaani hakuna mtu ambaye anahangaika au hata kumtazama?
Mbona Emmanuel Okwi akipita mtaani ni watu wawili au watatu tu wataomba wapige naye picha, wengine wote wataendelea na shughuli zao? Kwanini? Ina maana Watanzania wana dharau?
Sidhani kama Watanzania wana dharau, ila wachezaji wenyewe wameshindwa kuheshimu kazi yao. Wengi wanakunywa katika baa za mtaani na tena wakiwa huko hawanunui vinywaji vyao wenyewe, wanaomba kwa mashabiki. Mashabiki wamewachoka.
Nimetumia majina ya Ngassa na Okwi si kwamba wana tabia hizo, la hasha ila nimetaka kuweka uwakilishi wa wachezaji wetu ambao wanacheza Ligi Kuu Bara.
Wachezaji wetu wanajiachia mno mtaani, wanajichanganya mno na mashabiki, kiasi kwamba kunakuwa hakuna tofauti kati ya shabiki na mchezaji.
Mbaya zaidi wachezaji hawa wakiwa mtaani wanacheza mechi za chai maharage ambazo kila mmoja hulipwa kuanzia sh 20,000 mpaka 50,000 kutegemeana na ukubwa wa mechi.
Bila shaka unajua jinsi nyota wa Yanga; Jerry Tegete, Haruna Niyonzima, David Luhende, Oscar Joshua na Hamis Thabiti walivyoichezea Liverpool ya Dar es Salaam katika mechi ya fainali ya ligi ya Mwenyekiti wa mtaa wa Mtakala Makangarawe, Yombo katika Wilaya ya Temeke. Ni aibu tupu!
Kama mchezaji wa Yanga anayelipwa fedha kubwa, mwenye mkataba mzuri na ambaye anachezea timu ya taifa anaweza kuchezea timu ya vichochoroni, unatarajia kuna Mtanzania atataka kupiga naye picha? Watanzania wana dharau? Tunawaonea.