Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Serengeti Boys iwashtue TFF, wadau

NIONAVYO Pict

Muktasari:

  • Ni matokeo mabaya sana katika hatua ya makundi kwa timu hiyo katika miaka ya karibuni. Serengeti Boys ilifungwa goli 4-1, 3-0, 3-0 kutoka kwa Zambia, Uganda na wenyeji Morocco mtawalia katika michezo yake ya kundi A. Ndoto za kuwania nafasi ya kufuzu kwenda Kombe la Dunia litakalofanyika Novemba 2025 nchini Qatar zikawa zimefikia mwisho.

TIMU ya taifa ya Tanzania ya wavulana chini ya umri wa miaka 17, maarufu kama Serengeti Boys, imetolewa mapema sana katika michuano ya Mataifa ya Afrika chini ya miaka 17 ambayo itafikia tamati mwishoni mwa juma hili.

Ni matokeo mabaya sana katika hatua ya makundi kwa timu hiyo katika miaka ya karibuni. Serengeti Boys ilifungwa goli 4-1, 3-0, 3-0 kutoka kwa Zambia, Uganda na wenyeji Morocco mtawalia katika michezo yake ya kundi A. 

Ndoto za kuwania nafasi ya kufuzu kwenda Kombe la Dunia litakalofanyika Novemba 2025 nchini Qatar zikawa zimefikia mwisho.

Bila kubeza hatua waliyofikia kwa kufuzu kwa fainali hizi, bado ni muhimu kwa TFF kutafakari kilichotokea mpaka timu hiyo kuonekana kuwa haikufikia au hata kukaribia viwango vya wenzao katika kundi lao. 

Kumaliza mzunguko wa kundi bila hata alama moja huku wakifungwa goli 10 katika michezo mitatu ni jambo la kushtua.

Yawezekana timu yetu imeshuka kiwango. Hilo ni jambo la kawaida kwani timu haziwezi kuwa na kiwango kilekile na vipaji vilevile kila mwaka, hasa kwa timu za vijana ambazo zinabadilika kila vijana wanapokua wakubwa na kuvuka umri wa chini ya miaka 17. 

NIONA 01

Hata hivyo, bado hilo ni jambo lisilo zuri kwani tayari Tanzania imejiwekea viwango vyake tangu kufuzu kwa Serengeti Boys ya mwaka 2017 kule Gabon tena ikifuzu miongoni mwa timu 8. Kwa mantiki hiyo, Tanzania si kwamba inashindana na mataifa mengine tu, inashindana pia na rekodi zake.

Yawezekana pia wenzetu wamepanda viwango sisi tukibaki palepale. Wakati mwingine usipochungulia kwa jirani wanafanya nini unaweza kujikuta uko nyuma ya kinachoendelea duniani.

Kwa kuangalia michuano inayoendelea Morocco, unaweza kuona jinsi kila siku timu za vijana zinapiga hatua na kucheza mpira wa ufundi ambao hauna tofauti sana na mpira wa wakubwa.

Sina hakika sana na namna na utaratibu wa kuwapata wachezaji wa Serengeti Boys. Hilo nalo ni la muhimu sana katika kuhakikisha vipaji vinakusanywa kuanzia shule za msingi, sekondari, akademi na mashindano mengine yaliyo rasmi na yasiyo rasmi. 

NIONA 02

Baada ya vipaji kupatikana ni muhimu wakawa pamoja kwa muda wa kutosha na kupata michezo mingi ya kujipima nguvu. Bila shaka wahusika wanaweza kujipima katika hilo.

Kumekuwa na maneno kuhusu benchi la ufundi la Serengeti Boys kutokuwa na uzoefu wa kutosha. Hili kwa namna moja au nyingine linaweza kuathiri ufanisi wa timu. Bila shaka idara ya ufundi ilijiridhisha na timu ya ufundi iliyokwenda Morocco.

Ufanisi wa kikosi cha timu za vijana unaweza kukupa mwelekeo wa nchi katika miaka ijayo. Hii Serengeti ya sasa inatakiwa kutengeneza uti wa mgongo wa timu ya taifa chini ya miaka 20 ifikapo 2027. 

Timu hii inatakiwa kuwa na mchango katika timu ya taifa itakayocheza Afcon 2029 na pia kampeni ya kufuzu kwenda Kombe la Dunia 2030.

Ni kweli kwamba kuna wachezaji wanaoibuka humu katikati bila kupitia kwenye timu za vijana. Kuna wanaoweza kutokea mtaani au kutoka nje ya nchi na kutumika katika timu za taifa. Hata hivyo, kwa mpira wa sasa chanzo kikuu cha wachezaji wa timu za taifa ni timu za vijana.

NIONA 03

Unaweza kuangalia wachezaji wa Serengeti Boys wa huko nyuma walivyoweza kuingia kwenye klabu kubwa kama Yanga, Simba na hata wengine kupata nafasi za kucheza nje ya nchi kutokana na uzoefu na ushindani walioupata kupitia mfumo wa timu za vijana.

Tunaelekeza kidole kwa TFF kama mmiliki wa Serengeti Boys. Kwa upande mwingine TFF ina wajibu wa kuweka kanuni sahihi za kuhakikisha klabu za madaraja yote zinakuwa na mifumo sahihi ya timu za vijana. 

Mtazamo mkubwa wa timu zetu nyingi hasa za Ligi Kuu ni kutafuta fedha na kununua wachezaji waliolelewa kwingine. Huwezi kutegemea kuwa na Serengeti Boys shindani ikiwa haipati wachezaji ambao angalau wanacheza hata vikosi vya pili vya timu ya Ligi Kuu.

Serengeti Boys ni Taifa Stars ya miaka michache inayokuja. Ni muhimu sana kwa TFF na wadau wote kuweka macho yote na rasilimali za kutosha linapokuja suala la kuandaa timu hii. 

Tofauti na hapo tuandae fedha za kuwabadili uraia wachezaji wa kigeni. Kuijenga Serengeti Boys ni kuijenga Taifa Stars. Samaki akunjwe angali mbichi. Kumbuka, tuko nje ya 100 bora katika viwango vya ubora wa timu za taifa za wanaume.

Tathmini ya kilichoipata Serengeti Boys ni muhimu kufanyika iwapo iko nia ya dhati ya kuijenga Serengeti Boys imara na kesho nzuri kwa timu zetu za taifa.

Mwandishi wa Makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Unaweza kutuma maoni yako kupitia namba yake hapo juu.