Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NYUMA YA PAZIA: Historia na Jiografia pengo la Brahim Diaz na Tshabalala

PAZIA Pict

Muktasari:

  • Wao wapo katika na miji. Wanakupeleka moja kwa moja katika mji unaotaka kwenda. Kutoka mji fulani wa Morocco  hadi mji mwingine wa Ulaya unaotaka kwenda. Kutoka mji wa Tangier pale Morocco mpaka Madrid ni saa moja na dakika 13. Unaishia kutabasamu tu. Jiografia iliwabeba tangu dunia inaumbwa, halafu historia ikawabeba zaidi.

UWANJA wa Ndege wa Mohammed V pale Casablanca unakufungulia kila jambo kwa haraka. Ubao wa matangazo ndege zinazoondoka na kutua zinakuashiria kitu. Unaishia kutabasamu na kugeuka. Unaondoka ukiwa hauna siri kubwa moyoni wala machoni. Kengele za ukweli zinagonga katika ubongo wako.

Ubao unaonyesha miji ambayo ndege zao kubwa zinakwenda. Paris, Marseille, Madrid, Doha, Jeddah, Milan, Amsterdam, Barcelona, Venice,  Manchester,  Tunis. Unaishia kutabasamu tu. Ni tofauti na ubao wa uwanja wetu wa Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Sisi tunanyanyuka kutoka chini mpaka sehemu ya kuunganisha ndege. Doha, Dubai au Instabul. Basi.

Wao wapo katika na miji. Wanakupeleka moja kwa moja katika mji unaotaka kwenda. Kutoka mji fulani wa Morocco  hadi mji mwingine wa Ulaya unaotaka kwenda. Kutoka mji wa Tangier pale Morocco mpaka Madrid ni saa moja na dakika 13. Unaishia kutabasamu tu. Jiografia iliwabeba tangu dunia inaumbwa, halafu historia ikawabeba zaidi.

Vizazi kwa vizazi vikazamia Ulaya, hasa katika nchi hizi ambazo unasafiri saa moja au saa mbili kufika Madrid, Amsterdam, Brussels na kwingineko. Hapo yalitengenezwa mapengo makubwa na sisi huku Kusini mwa Afrika. Na hapo ndipo tukaona hata uwanjani kuna mapengo makubwa. Na hata pengo la Brahim Diaz na Mohamed Hussein Tshabalala likaonekana hapo.

PAZ 02

Diaz amezaliwa Malaga. Achraf Hakimi amezaliwa Madrid. Hakim Ziyech amezaliwa Uholanzi. Sofiane Amrabat amezaliwa Brussels. Kwao ni jambo la kawaida tu. Kile kikosi kimecheza na Tanzania Jumanne usiku baada ya futari kimesheheni wachezaji wa namna hii. Hawa akina Hakimi ni kwa sababu tunawafahamu tu lakini wapo zaidi ya 14 wamezaliwa Ulaya.

Halafu kwa sababu wapo wengi vizazi na vizazi basi wala hawana ushamba na Ulaya. Na kwa sababu wapo karibu na Ulaya basi wala hawana ushamba na Ulaya. Kwao Casablanca wanaichukulia kama miji iliyopo kando ya nchi ambazo wamezaliwa.

Na kwa sababu Morocco ni kuzuri basi wala hawana ushamba na Ulaya. Wanakulia katika jamii za Wamorocco na mwishowe inakuwa rahisi kwao kuamua kucheza Morocco. Kule wanakaa katika makundi ya Wamorocco wenzao, na wakienda Morocco hawaoni tofauti na walikozaliwa.

Hakimi na Diaz wasingekosa namba Hispania. Ziyech asingekosa namba Uholanzi. Amrabat asingekosa namba Ubelgiji. Hata hivyo waliamua kucheza kwao Morocco. Kwa aina yao ya maisha pale walipoamua kuwa 'serious' haikushangaza walipokuwa timu ya kwanza kutoka bara la Afrika kufika hatua ya nusu fainali ya kombe la dunia katika historia yetu.

PAZ 01

Nilimuona Mohamed Hussein 'Tshabalala' akiteseka kwa Diaz. Sikushangaa. Diaz anatesa wazungu itakuwa kwa kijana aliyeamua kujitafutia maisha kwa mpira pale Manzese na mpaka leo yupo nchini? Diaz anatesa wazungu wenzake wenye misingi pale La Liga na Ligi ya mabingwa barani Ulaya. Itakuwa kwa Tshabalala?

Saizi yake anaweza kuwa Lewis Myles-Skelly ambaye naye amezaliwa London na katika umri wa miaka 18 tu ya ukweli tayari ana namba katika kikosi cha Arsenal na anatazamiwa kucheza dakika 180 za Ligi ya mabingwa Emirates na Santiago Bernabeu ndani ya wiki mbili hizi hapa. Kwa haraka huyu wanaweza kupeana maswali ya haraka na Diaz

Lakini rafiki yetu Tshabalala na Diaz wanatenganishwa na mambo mengi. Historia, Jiografia, uchumi na kila kitu. Wapinzani wao halisi wapo huko huko walikozaliwa. Sisi kuweza kubishana nao tunahitaji mambo mengi. Tunahitaji ubishi mwingi wa makusudi na ambao hadi sasa akina Tshabalala huenda wakawa wameupoteza.

PAZ 04

Kubishana nao kwa uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na kitimu, inahitaji nguvu za ziada na jitihada za makusudi. Wachezaji waliozaliwa ndani ya Morocco na wale waliozaliwa nje wamekuzwa vema. Ukizurura katika viwanja vya Rabat, Casablanca, Oujda, Marreikh na kwingineko utaona. Vipi kwa wale waliozaliwa Madrid, Amsterdam, Brussels na kwingineko? Maisha hayatendi haki sana.

Hawa kina Diaz, Hakimi, Ziyech na wengineo wengi wamecheza katika timu za taifa za vijana za Wazungu. Ulipofika muda wa maamuzi ndio wakaamua kucheza timu za baba zao. Tayari walishakaa katika mfumo kwa muda mrefu tu. Misingi ilikuwepo. Na hata kama wangezaliwa Casablanca bado misingi ingekuwepo.

Ndugu zetu wa Afrika Magharibi ni weusi wenzetu lakini nao wana faida kama hii. Faida ya kijiografia na Kihistoria. Kiuchumi sio sana lakini hizi faida mbili hapa juu wamezitumia vema. Unajumlisha na ukweli kwamba mkoloni wao Mfaransa aliwatengenezea sera ya kujifanya wajione Wafaransa na wawe Wafaransa (assimilation policy). Hapa ndipo akina Didier Drogba walikochomokea. Lakini akina Patrick Vieira wakaamua kucheza kule kabisa.

Huku kwetu chini Kusini mwa Afrika na pale Afrika ya kati inabidi tupambane haswa kwenda sawa na hawa jamaa. Pengo ni kubwa. Huku Jiografia imetutupa lakini pia umaskini umetushika mkono. Ni pale Afrika Kusini tu ndio kuna miti lakini hakuna wajenzi. Wazungu wamegoma kucheza soka wamewaachia watu weusi.

PAZ 03

Baada ya kugawana kwa michezo, mzungu akacheza Rugby na mtu mweusi akacheza soka, tumeona namna ambavyo Mzungu anafanikiwa kuchukua hata kombe la dunia la Rugby. Wakati huo huo nakukumbusha kwamba Bafana Bafana haijawahi hata kuvuka katika hatua ya makundi ya kombe la dunia katika mara mbili ambazo wameshiriki. Huu ndio ukweli mchungu ambao inabidi tuumeze.

Usione Taifa Stars wameteseka sana pale Oujda. Pengo ni kubwa na pengo ni halisi. Sio maigizo. Inabidi tulizibe kwa mapambano ya machozi, jasho na damu. Mwamuzi wa pambano alionekana kuwabeba Wamorocco lakini mwisho wa mechi tulikubaliana kwamba maji na mafuta vilijitenga. Mpira ulikuwa umetoa maamuzi sahihi kwa usiku ule.

Hawa kina Tshabalala wana vipaji kama wale lakini bahati mbaya wamezaliwa katika misingi mibovu. Walau hata wangezaliwa pale Magharibi mambo yangeweza kuwa mazuri zaidi. Kwani Tshabalala anamuweka nani benchi pale Simba? Valentin Nouma kutoka Burkina Faso. Afrika Magharibi. Vipi na yeye angekuwa anatoka kule?

Tatizo ni kujilea kwa wachezaji wetu. Hawalelewi. Hawatunzwi. Uchumi wa mchezaji ni mbovu. Uchumi wa wazazi wake ni mbovu. Uchumi wa timu zake za utotoni ni mbovu. Uchumi wa taifa lake ni mbovu. Juzi CAG katuambia deni la taifa wote tumeinamisha vichwa katika meza. Mchezaji kama Tshabalala kutoka anahitaji vita vya peke yake na maarifa ya aina yake.

Tanzania, Malawi, Uganda, Zambia, Kenya. Huku kwetu kupenya na kula sahani moja na akina Diaz kazi ifanyike hasa. Tumeweza kuwatoa mmoja mmoja tu. Akina Mcdonald Mariga, Kalusha Bwalya, Mbwana Samatta, Victor Wanyama, Patson Daka, Dennis Oliech. Inahitajika nguvu ya ziada kweli kweli wakati wenzetu walipanda ndege dakika 80 tu kufika Ulaya.