Prime
NYUMA YA PAZIA: Salah, Van Dijk kama funda la mwisho katika soda Anfield

Muktasari:
- Anfield kuna kiwewe. Virgil van Dijik anakaribia kumaliza mkataba wake mwisho wa msimu. Mo Salah anakaribia kumaliza mkataba wake mwisho wa msimu. Trent Alexander-Arnold anakaribia kumaliza mkataba wake mwisho wa msimu.
KADRI soda inavyosogea kwenda chini ndani ya chupa yake ndivyo utamu unavyozidi. Lile funda la mwisho linapokaribia soda inazidi kuwa tamu zaidi. Wazungu wana Kiingereza chao. Wanasema ‘enjoy while it lasts’. Faidi kadri inavyokaribia kumalizika.
Anfield kuna kiwewe. Virgil van Dijik anakaribia kumaliza mkataba wake mwisho wa msimu. Mo Salah anakaribia kumaliza mkataba wake mwisho wa msimu. Trent Alexander-Arnold anakaribia kumaliza mkataba wake mwisho wa msimu.
Kuna chuki kubwa kati ya mashabiki wa Liverpool na Trent kwa sababu anatajwa kwenda Real Madrid mwishoni mwa msimu. Kinachowauma ni kwamba Trent ana umri wa miaka 26 tu. Anaondoka mapema.
Trent anafanya kile ambacho Steve McManaman aliwahi kufanya zaidi ya miaka 20 iliyopita. Aliondoka zake bure kwenda Real Madrid akiwa wa moto hasa. Alikuwa miongoni mwa wachezaji mahiri wa mwanzo mwanzo kutumia vyema sheria ya kuondoka bure baada ya mkataba kumalizika (Bosman Rule).

Anfield wana haki ya kumuona mtoto wao Trent ni msaliti. Nitalizungumza hili akishathibitisha kuondoka kwake. Lakini kwa Salah na Van Dijik watu wa Anfield hawana neno sana. Kwao wakiondoka ni sawa, wakibakia ni sawa. Wanachofanya kwa sasa mashabiki wa Anfield ni kuhakikisha wanafurahia ubora wa hawa watu wawili wakati utamu ukielekea mwisho.
Van Dijik atatimiza miaka 34 siku moja baada ya Tanzania kuadhimisha Sikukuu ya Sabasaba, Julai 8. Wakati huohuo Salah atakuwa anatimiza miaka 33 ifikapo Juni, mwaka huu. Nyakati zimekwenda na zama zinakaribia kufika mwisho.
Haijulikani kwanini wachezaji wote watatu hawajasaini mikataba mipya mpaka sasa. Naweza tu kufikiria kwamba kwa Trent ni wazi nguvu ya mawakala na wachezaji siku hizi imekuwa kubwa kiasi kwamba wana nguvu kuliko klabu husika.

Kuna wachezaji wengi kama Trent ambao hawana umri mkubwa na ni hodari lakini wamefanikiwa kutiririsha mikataba yao mpaka siku ya mwisho na kufanikiwa kuondoka bure klabuni. Hao wapo wengi kwa sababu nguvu ya wachezaji imekuwa kubwa siku hizi.
Lakini kwa Virgil na Salah kuna mawazo ya aina mbili. Labda klabu imeona haina haja ya kuwapa mikataba minono wakati huu miaka yao ikiwa imesonga mbele. Wazungu huwa wana akili zao tofauti. Badala yake wameona waendelee tu kuwafaidi wakati huu wakielekea mwisho.
Lakini pia inawezekana wachezaji wenyewe wameamua kumalizia mikataba yao Anfield kabla hawajaenda Saudi Arabia kuchota noti nyingi zaidi ambazo hazikatwi kodi. Kule mchezaji analipwa Pauni 500,000 kwa wiki na mshahara wake haukatwi kodi.

Kule unakwenda kupumzika kwa sababu mpira wake sio kama huu wa England ambao unatumia nguvu kubwa zaidi na mshahara wake unautolea jasho hasa. Haishangazi kuona wachezaji wengi wanakwenda zao kujificha Saudia kwa sasa wakiungana na Cristiano Ronaldo ambaye muda mwingi anacheza huku akitembea.
Vyovyote ilivyo, mashabiki wa Liverpool hawawezi kujali. Wanachofanya ni kufaidi utamu wa Van Dijik na Salah mpaka mwisho wa msimu huu. Ni msimu ambao mpaka sasa wanaongoza kwa tofauti ya pointi 12 dhidi ya Arsenal.
Ni msimu mwingine ambao wanakwenda kuwa mabingwa wa England baada ya ule wa 2019-20 ambao walirudisha ubingwa wa England kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30. Nani anajali kama Van Dijik na Salah wanaondoka ilimradi tu wanatwaa ubingwa mwingine wa England ndani ya miaka mitano baada ya kuishi kwa dhiki na ukame wa taji hilo kwa miaka 30 kabla ya hapo?

Hakuna atakayejali sana Van Dijik na Salah wakiondoka kwa sababu watakuwa wameondoka kwa heshima. Watakuwa wamewapa taji la 20 la Ligi ya England na hivyo kuifikia Manchester United. Haikuwa safari nyepesi sana.
Awali Liverpool walikuwa wanaongoza kwa mbali kwa kutwaa mataji mengi ya Ligi ya England. Walikuwa wametwaa mara 18 huku Manchester United wakiwa wametwaa mara saba tu kabla ya Sir Alex Ferguson kutua Carrington mwaka 1986.
Kuanzia hapo Sir Alex aliwapa United mataji 13 na hivyo kufikisha mataji 20 ambayo yaliipiku Liverpool mataji mawili zaidi. Liverpool walikuwa wamepotea kwa miaka 30 mpaka Jurgen Klopp alipowasogeza mwaka 2020 na kuwapa taji la 19, na sasa Arne Slot anaweza kusawazisha kwa taji la 20.
Kwa kufanya hivyo, Liverpool watakuwa timu yenye mafanikio zaidi katika soka la Kiingereza kwa sababu watakuwa na mataji sawa na Manchester United katika Ligi Kuu lakini pia watakuwa na mataji mengi zaidi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kuliko United.

Nani atajali kama Salah na Van Dijik wanaondoka baada ya kuwapatia mataji haya mawili. Wanachofanya sasa hivi ni kufaidi ubora wao tu. Wanakwenda Anfield au viwanja vya ugenini na kuwatazama mastaa ambao wameingia katika historia ya kuwa miongoni mwa wachezaji bora kuwahi kutokea Anfield.
Ikifika mwisho wa msimu kama watatangaza kuondoka basi hakuna ubaya. Watakachotaka watu wa Anfield ni kuona tu matajiri wao wanatumia pesa nyingi kusaka mastaa wa kuziba nafasi zao. Na kama lolote likitokea kati ya sasa hadi hapo baadaye na wakasaini mikataba mipya basi bado itakuwa heri tu kuendelea kuwa nao. Kati ya hawa wawili nadhani Salah ndo anaweza kuondoka zake akaungane na Waarabu wenzake kule Saudia. Labda Virgil anaweza kubakia kwa msimu mmoja zaidi lakini simuoni Salah akiendelea kuvaa jezi ya Liverpool msimu ujao.