Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NYUMA YA PAZIA: ‘The Genius’ Kevin de Bruyne, mambo hufika mwisho

PAZIA Pict

Muktasari:

  • Kevin de Bruyne. Ametangaza kuondoka Manchester City mwishoni mwa msimu huu.

KWANINI rangi nyeusi huwa inaashiria vitu vibaya? Wakati mwingine inaashiria msiba. Mtoto kutoka Drongen, Ubelgiji wiki iliyopita alichukua peni na karatasi na kuandika kitu katika karatasi nyeusi akijua kwamba taarifa yake ingeashiria msiba.

Kevin de Bruyne. Ametangaza kuondoka Manchester City mwishoni mwa msimu huu. Mambo hufika mwisho. Mapema mwanzo wa wiki hii KDB alishika peni na karatasi na kuandika kuwa utakuwa msimu wake wa mwisho Manchester City. Nadhani utakuwa msimu wake wa mwisho pia Ligi Kuu England.

Sitendi haki ninapomzungumzia Kevin de Brune. Siangalii pande mbili. Naangalia pande moja. Sijawahi kuona upungufu wake. Mmoja kati ya wachezaji wachache wenye akili kubwa ya mpira ambao nimewahi kuwaona katika uso wa dunia. Natamani kupeana naye mkono siku moja.

Tuanzie wapi? Tuanzie katika ukweli wa hayo maswali ambayo wachezaji wa sasa au wa zamani wamekuwa wakiulizwa kuhusu ubora wa wachezaji mbalimbali. Mastaa wa zamani na wa sasa wataulizwa kuhusu mchezaji mwenye kasi, mwenye nguvu, anayetumia mguu wa kushoto vizuri na mengineyo.

PAZ 01

Wengine wanapoulizwa kuhusu mchezaji mwenye akili kubwa ya mpira huwa wanajibu ‘Kevin de Bruyne’. Ndio, De Bruyne amejaaliwa kuwa na akili kubwa ya mpira. Anajua ni wakati gani aufanyie nini mpira hasa katika uamuzi wa eneo la mwisho.

Nadhani De Bruyne atakuwa anaelekea Saudi Arabia au Qatar kuchukua noti za Waarabu ama Marekani kutafuta pensheni ya mwisho na kina Lionel Messi. Ninachojua ni kwamba ameniacha mambo manne ya msingi.

Jambo la kwanza ni kubadilisha dhana ya nafasi ya kiungo wa juu. Hatuwezi kumkumbuka De Bruyne kwa chenga, tobo wala kanzu. Tutamkumbuka kwa kuwaambia watoto wetu wafanye mambo ya msingi katika mpira wa kisasa. De Bruyne sio Zinedine Zidane, sio Ronaldinho wala sio Andrea Pirlo, lakini ametukosha katika uamuzi wake na mpira. Bahati nzuri ameishi katika zama ambazo mpira wa kisasa wenyewe unataka jambo hilo. Makocha wengi wanataka zaidi jambo hilo kuliko kanzu na tobo.

PAZ 02

Katika dunia hii ya namba kwa wachezaji, De Bruyne ameweza kuishi nayo. Wakati mwingine katika dunia ya kisasa kuna mchanganyiko wa kile tunachokiona halafu kuna kile ambacho kipo katika namba. De Bryune ameweza kuishi na vyote. Unakiamini unachokiona kutoka kwake na unaamini katika namba zake.

Mfano wa pasi za mwisho tu, De Bruyne anaondoka katika Ligi Kuu England akiwa ni mchezaji wa pili kwa kuwa na pasi nyingi zilizozaa mabao nyuma ya Ryan Giggs. Wakati Giggs akiwa na pasi 162 za mwisho, KDB ana pasi 118. Papo hapo kumbuka kwamba Giggs amecheza zaidi ya misimu 22 ya Ligi Kuu England wakati De Bruyne amecheza misimu 10.

Kitu kingine tofauti kwa De Bruyne ni namna ambavyo amekuwa alama ya kiungo wa kisasa katika mahitaji ya hawa makocha wetu wapya kina Pep Guardiola. Hawa makocha wanataka kila mtu awajibike wakati timu ikiwa haina mpira uwanjani.

Kevin alikulia katika ubora huu. Wakati akiwa ana mpira alikuwa bora. Wakati akiwa hana mpira alikuwa bora. Hii ya pili kwa maana ya kukaba wapinzani kwa kiasi kilekile, jasho lile lile kama vile wakati una mpira. Nawajua viungo wengi wa zamani ambao walipishana na zama hizi. 

PAZ 03

Zidane na Ronaldinho hatukuwahi kujua kama wangeweza kuwa bora wakiwa hawana mpira. Hatujui kama wangewafurahisha makocha wa kisasa wakati wakiwa hawana mpira. Na hata zama hizi zilipowadia ungeweza kuona kabisa kuna mafundi wengine walishinda. Mfano ni Mesut Ozil.

KDB anabaki kuwa mmoja kati ya viungo wa kizazi kipya ambao licha ya kuwa mafundi mguuni, lakini walikuwa na uwezo mkubwa wa kukaba wakati wakiwa hawana mpira. Kucheza mpira wa Pep kunahitaji mateso makubwa. Usione kwamba tunafurahia timu yake au tulifurahia mpira wa Jurgen Klopp ukweli ni kwamba kuna mateso makubwa kucheza timu zao kama ukiwa mchezaji goigoi hata kama ukiwa fundi. Mafundi wanahitajika kufanya kazi kubwa wakiwa hawana mpira.

Leo unapoiona Arsenal inamchapa Real Madrid 3-0 pale Emirates ni kwa sababu wale mafundi wengi wa Santiago Bernabeu ambao tunawaimba midomoni huwa hawafanyi kazi nzuri wakati timu ikiwa haina mpira. De Bruyne sio mchezaji wa aina yao.

PAZ 04

Kitu kingine ambacho De Bruyne anatuachia kumbukumbu ni ukweli kwamba alikuwa ni fundi ambaye alicheza timu isiyo na mashabiki wengi ndani na nje ya England, lakini wote tulikubaliana kumkubali. Wote sisi, mashabiki wa Liverpool, Arsenal, Manchester United, Chelsea tuliamua kumkubali De Bruyne.

Na nje ya England wote waliamua kumkubali De Bruyne. Mara nyingi wachezaji wanaopata sifa nyingi na kupambwa ni wale wanaocheza timu zenye historia kubwa. Manchester City ilianza kupata sifa baada ya noti za Waarabu kuingia na wala haikupendwa. Hata hivyo, wote tulikubaliana kumpenda De Bruyne na kukubali kwamba alikuwa bora kuliko viungo wetu.

Na katika hili hili tunakumbushwa namna ambavyo pesa za Waarabu zinafanya kazi. Zamani mchezaji kama De Bruyne kituo chake kikubwa cha kazi kingeweza kuwa Nou Camp, Emirates, Santiago Bernabeu, San Siro au Old Trafford. KDB ni kielelezo namna ambavyo kwa sasa pesa inaongea. 

Nguvu ya pesa imesababisha wachezaji wanaoweza kuwa wanasoka bora wa dunia wanatokea katika klabu ambazo awali hazikudhaniwa. Ni kama Rodri alivyobeba tuzo ya mwanasoka bora wa dunia akitokea Manchester City.

Kitu kingine ambacho De Bruyne ametukumbusha ni namna ambavyo mchezaji yeyote anaweza kutoka mahala popote. De Bruyne hakuwa Mbrazili, Muargentina, Mfaransa, Mhispaniola, Mwingereza wala Mjerumani. Ametoka taifa ambalo halijawahi kutwaa Kombe la Dunia wala Euro, lakini ametingisha dunia. Ubelgiji.

Vyovyote ilivyo, asante kwa kumbukumbu Kevin. Mmoja kati ya viungo bora kuwahi kutokea katika soka, lakini anaweza kuwa kiungo bora zaidi katika soka la kisasa. Amewafundisha vijana kutokuwa na mambo mengi zaidi ya kuwa na mambo ya msingi uwanjani. 

PAZ 05

Mambo yake ya msingi aliyafanya kwa ufasaha zaidi. Na hata hivyo kwa sasa anataka kufanya kitu cha ufasaha zaidi. Unafanya kazi ngumu kwa mshahara kwa Pauni 350,000 kwa wiki halafu unaenda kufanya kazi nyepesi kwa mshahara wa pauni 500,000 kwa wiki. Anakaribia noti nyingi za Waarabu.

Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa kwa sababu hatumdai Kevin. Ni tofauti na vijana wenye umri wa miaka 23 ambao wamekimbilia Riyadh bila ya kutuonyesha ubora wao wa mwisho katika soka. Wachezaji kama Lionel Messi, Cristiano Ronaldo walituonyesha ubora wao wa mwisho katika soka kabla ya kwenda kutafuta noti za bure.  Kila la heri kwake. 

Tunachotazamia cha mwisho ni kwamba labda kwa sababu amepita katika mikono ya Pep basi anaweza baadaye kidogo kujiunga na kundi la akina Arteta na Vincent Kompany ambao wamnepita katika mikono yake na wamefanya kazi nzuri.