Prime
Okello ataja ‘mtego’ unaoitesa Simba!
KABLA ya Ligi Kuu Bara kusimama, kama kuna staa wa Yanga alikuwa amewakosha mashabiki wa timu hiyo basi lilikuwa jina la Allan Okello ambaye kwa sasa yupo kwenye kiwango bora akiendelea kuibeba timu yake mabaegani.
Okello alisajiliwa na Yanga akitokea Vipers ya Uganda akiingia kupitia usajili wa dirisha la Januari lakini baada ya kuanza taratibu sasa kiungo huyo anayetumia hasa mguu wa kushoto amefanikiwa kubadilisha upepo akifunga na kutenegeneza mabao muhimu.
Baada ya kuanza kuonyesha moto wake akiwa amefunga mabao 11 na kutoka asisti saba hadi sasa akishika nafasi ya pili kwa ufungaji nyuma ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ Mwanaspoti limepata nafasi ya kufanya naye mahojiano maalumu akieleza mambo mbalimbali juu ya safari yake ndani ya klabu hiyo huku akisisitiza kwamba licha ya mbio za ubingwa kuwa kali lakini taji hilo lipo kwenye mikono yao.
ALIANZAJE YANGA?
Okello aliyezaliwa miaka 25 iliyopita, Kaskazini mwa Uganda Wilaya ya Lira, anaanza kwa kueleza namna alivyoanza taratibu ndani ya Yanga huku akiwashukuru wachezaji wenzake na makocha na hata mashabiki kwa namna walivyokuwa na subira na kumpa imani wakati akijitafuta.
“Sidhani kama nahitaji kueleza sana juu ya namna nilivyoanza hapa Yanga, kila mtu anajua, kiukweli haikuwa rahisi, wachezaji wenzangu walinisaidia sana kuzoea kwa haraka maisha ya hapa kuhusu soka la Tanzania, kila wakati walikuwa wananipa nguvu ya kujiamini na unajua kwanini walikuwa wananihamasisha kila siku kuwa kuna siku nitafanya vizuri.
“Nawashukuru pia makocha wote, mashabiki wetu kila wakati walikuwa wana imani na mimi, hata pale ambapo sikuwa sawa lakini bado waliendelea kunipa nafasi ya kucheza kila mchezo, hii ilinijenga na kuwa imara zaidi kama mchezaji.”
KIPI KILIKUWA KIGUMU MWANZO?
“Naweza kusema hakukuwa na tatizo lolote kuchelewa kwangu kuanza kuonyesha uwezo, kama mchezaji unakuwa huwezi kujua kipi kitatokea, unaendelea kufanya kazi yako ukisubiri wakati ambao utaweza kuonyesha kile kilichokuwa kinasubiriwa, wakati huo ukifika, unajua kuna wakati unaweza kuona unafanya kitu sahihi lakini kumbe hufanyi kitu sahihi sasa wakati ukigundua hilo hapo utaanza kufanya kile kilicho sahihi, kwa hiyo kama mchezaji ili uweze kuzoea, kawaida unatakiwa kusubiri ule wakati sahihi na utaendelea kufanya vizuri.”
UAMUZI WA KUTUA YANGA ULIKUWA RAHISI?
“Siwezi kusema ilikuwa rahisi, nilipowasiliana na Rais (Rais wa Yanga Hersi Said) na menejimenti yangu ilikuwa pia imewasiliana naye, kwanza ilinibidi niongee na Aucho (Khalid), tukajadiliana na baada ya hapo nikaongea na rais wa klabu yangu ya zamani, ili aweze kuniruhusu, hakuwa tayari kuniachia kuondoka wakati wa Januari, ilihitajika nifanye kazi ya ziada kumshawishi kukubali baadaye alikubali na hapo ndio nikapata nafasi ya kuwa mch ezaji wa Yanga. “Nadhani pia akili ya rais wa klabu (Hersi) alifanya kazi kubwa sana kumshawishi rais wa Vipers, kuna wakati unatakiwa kuwa na uthubutu wa ushawishi Hersi hilo analo.’’
YANGA NI TIMU YA AINA GANI?
“Ni timu kubwa, yaani kubwa, kama unavyoona kila mtu hapa anawaza ushindi tu, hawa wachezaji wote unaowaona hapa wanataka kushinda tu, hata kama ukija kujiunga hapa na ukawa hauna hiyo akili utajikuta na wewe unakuwa kama wao kwa haraka kwa sababu wanataka kushinda kila mchezo, hawataki kupoteza, hawataki kupata sare, kila mchezo wanauchukulia kwa umakini mkubwa.”
NAFASI IPI UNAPENDA KUCHEZA UWANJANI?
“Mimi napenda kucheza pale ambapo kocha atanitaka nicheze, unajua kila kocha ana mfumo wake, kitu muhimu kwangu kama mchezaji ni kuwa uwanjani na kucheza bila kujali kama kocha atanitaka nicheze kama beki siku hiyo, kwa kuwa nipo uwanjani nitakuwa nafuraha, unajua nikiwa uwanjani nitapata nguvu ya kutumikia nafasi ambayo natakiwa kuichezea.
“Kama nitakuwa nacheza sehemu ninayopenda nitafanya vizuri zaidi, sio kila wakati utacheza sehemu ambayo unaitaka, unafanya vizuri kwa ajili ya timu, kwangu mimi kama mchezaji kitu muhimu ni kuwa uwanjani na kucheza.”
MAANA YA USHANGILIAJI WAKE
“Ni stori ndefu kidogo, ilikuwa ni wakati naangalia fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018, nilikuwa naangalia na kaka zangu kama ambavyo sasa tunavyokwenda kuangalia fainali za mwaka huu, kuna mambo mengi yatakwenda kutokea na vitu vingi vipya, sasa kama nitaanza kueleza sasa tunaweza tukachukua muda mrefu lakini kifupi ilitokana na fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018.”
CHAMA NI MCHEZAJI MKUBWA
Baada ya Okello kuanza kufanya vizuri mashabiki wa timu wa Yanga na wale wa Simba walianza kupambanisha nani bora kati yake na kiungo wa Wekundu hao Clatous Chama, hapa Okello anaeleza juu ya hilo kama ni sawa au siyo sawa.
“Kama nilivyosema kabla, Chama ni mchezaji mkubwa, alikuwa hapa kabla ana uzoefu mkubwa na Ligi ya Tanzania, alikuwa hapa kwa miaka mitano au nane nyuma, kwangu mimi sioni kama ni sawa kunilinganisha naye, kwangu mimi muhimu ni kushindana na mimi mwenyewe, napambana na mimi mwenyewe kipi nilifanya kwenye mechi zilizopita, kipi natakiwa kukifanya kwenye mechi inayokuja, hicho ndio kitu ninachotaka kukifanya kwa ajili yangu mwenyewe.’’
MECHI ZILIZOSALIA UMEJIPANGAJE?
“Yanga tunajua nini tunatakiwa kufanya ili tutwae huu ubingwa, tukishinda kila mchezo hapo tunafahamu kwamba tutakwenda kuwa mabingwa lakini tutakuwa tunaichukua mechi moja kwenda nyingine, Simba wanaweza kushinda mechi zao sisi tunaweza pia kushinda mechi zetu, hatujui kipi kitatokea mbele, tutakwenda na mechi moja hadi nyingine, tuna imani kubwa mwisho wa msimu tutakuwa mabingwa kama tutajiweka sawa na kushinda kila mchezo uliopo mbele yetu kwa kuwa kila kimoja kipo kwenye mikono yetu kwa sasa.”
NANI RAFIKI YAKO MKUBWA NDANI YA YANGA?
“Ndani ya timu rafiki yangu mkubwa ni Maxi (Nzengeli), kwa sababu ni mtu ninayekaa naye chumba kimoja wakati wote tukiwa kambini, ndio mtu ambaye alinipokea, alinisaidia kuzoea mambo mengi ndani ya timu.’’
KUFUNGA AU KUTOA ASISTI KIPI UNAPENDA?
“Mimi napenda kutoa asisti ni bora kwangu kwa sababu mimi kama kiungo na mchezaji mbunifu napenda kuwa mtengenezaji kwa ajili ya wenzangu, nikiwasaidia kufunga tunashinda mechi zetu hii ni nzuri sana kwangu imekuwa ikinifanya kuwa bora kila siku.”
MECHI GANI ILIKUWA NGUMU UKIWA YANGA?
“Sitaki kuanza kuonyesha hizo mechi kwa sasa, nitapenda ujue kipi tumefanikiwa mwisho wa msimu na hapo ndio nitaweza kuona hii mechi au mchezo huu ulikuwa kama hivyo, naweza kusema tusubiri mwisho wa msimu.’’
MCHEZAJI GANI UNAMPENDA DUNIANI?
“Kabla nilikuwa namuangalia David Silva, nimepata nafasi pia ya kumuangalia Messi (Lionel) kwa muda mrefu, Messi ni kipaji kikubwa sana hasa kwa sisi wachezaji ambao tunatumia mguu wa kushoto tunatamani sana kupata hata robo ya kipaji chake, kuna wakati napenda kuangalia alichokuwa anafanya Andres Iniesta au Kelvin De Bruyne hivyo wote ndiyo wale wanaonivutia.”
OKELLO NI SHABIKI WA MANCHESTER UNITED
“Mimi ni shabiki wa Manchester United, sikufurahi kabisa kama shabiki wa timu hii kusikia Arsenal imechukua ubingwa, sikuona shamrashamra za Arsenal kuhusu ubingwa sana hapa Tanzania lakini kule Uganda watu wanapenda sana Arsenal, kuna ushindani mkubwa sana kati ya mashabiki wa Arsenal na Machester United ni sawa na kusema nusu ya watu ni Arsenal, kwa hiyo sisi mashabiki wa Manchester United tunateseka sana, kweli sio habari nzuri kwetu hawa jamaa kuchukua ubingwa.
“Walipochukua ubingwa tu nikaanza kupokea simu zao na meseji, wengine ni marafiki zangu, nikajikuta mpaka nazima simu yangu lakini nawapongeza sana, umepita muda mrefu kwao hawajapata mafanikio hayo na sisi mashabiki wa Manchester United tunasubiri siku njema kwetu kufurahia ubingwa.’’
IMANI NA CARRICK
“Carrick (Michael) amefanya kazi nzuri kwa kipindi kirefu hatukuweza kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na sasa tunarudi kushindana tena huko, tusubiri tuone, kitu muhimu apewe muda wa kutosha na imani lakini apate nafasi ya kuleta wachezaji bora.’’